Tafuta

2025.02.03V iongozi wa Ulimwengu wahudhuria Kongamano la Haki za Watoto. 2025.02.03V iongozi wa Ulimwengu wahudhuria Kongamano la Haki za Watoto.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko afunga Mkutano:Waraka wa kitume utaandikwa kuhusu watoto!

Papa Francisko amefunga Mkutano wa kimataifa kuhusu Haki za Watoto uliofanyika mjini Vatican 2-3Februari 2025 na kutangaza nia ya kuendeleza jukumu lililoanzishwa kwa kuchapisha Hati ya Kipapa wakati ujao inayokita na Watoto:Papa aliwashukuru"watoa mada kwa kubadilisha Jumba la kitume kuwa wachunguzi wa hali halisi ya utoto uliojeruhia na kukanyagwa."

Na Angella Rwezaula - Vatican.

Jumatatu, jioni  tarehe 3 Februari 2025, Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya pili tena alishiriki kuhitimisha Mkutano wa Kimataifa uliofanyika Mjini Vatican kuanzia tarehe 2-3 Februari kuhusu Haki za Watoto, ukiongozwa na kauli mbiu: "Tuwalinde na kuwapenda." Akiwageukia washiriki kutoka Ulimwenguni kote alisema: “Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwenu  mwishoni mwa Mkutano huu wa Haki za Watoto. Shukrani kwenu wajumbe wa  Jumba la kitume ambao leo mmekuwa "wachunguzi" walio wazi kwa ajili ya ukweli wa utoto ulimwenguni kote, utoto ambao kwa bahati mbaya mara nyingi hujeruhiwa, kunyonywa, kukataliwa.”


Papa Fracisko aliendelea kusema kuwa: “Uwepo wenu, uzoefu wenu na huruma yenu imetoa uhai kwa uchunguzi na juu ya yote kwa "maabara": katika makundi mbalimbali ya mada ambayo mmetengeneza mapendekezo ya ulinzi wa haki za watoto, mkizingatia sio idadi lakini kama nyuso. Haya yote yanampa Mungu utukufu na tunayakabidhi kwake, ili Roho wake Mtakatifu aifanye kuzaa na kutoa matunda."

Papa Viongozi wa dunia katika Mkutano mjini Vatican
Papa Viongozi wa dunia katika Mkutano mjini Vatican

Papa alisema, "Padre  Faltas alisema neno, kifungu ambacho ninakipenda sana: "Watoto wanatutazama." Ilikuwa pia jina la filamu maarufu. Watoto hututazama: hututazama ili kuona jinsi tunavyosonga mbele maishani.” Kwa upande wangu, ili kutoa mwendelezo wa ahadi hii na kuikuza katika Kanisa lote, ninatarajia kutayarisha barua, Waraka ambao sijui...  utajikita kwa ajili ya watoto. Asante tena kwa kila mtu, asante kwa kila mmoja wenu," alihitimisha.

Mkutano mjini Vatican
Mkutano mjini Vatican

Barua ya watoto kwa Baba Mtakatifu Francisko 

Mpendwa Papa Francisko, tunakuandikia kwa niaba ya watoto wa Dunia nzima, tunataka kukushukuru kwa sababu unajali juu yetu na maisha yetu ya baadaye, unatupenda na unatulinda. Asante kwa yote unayotufanyia! Asante kwa kusikiliza maswali yetu na kuchukua muda kujibu, kama vile Siku ya Watoto Duniani, siku hiyo, tulijifunza mambo mengi na ilikuwa vizuri kusikia na kuelewa ulichokuwa ukituambia. Siku hiyo tulielewa kuwa unataka msaada wetu kubadilisha Ulimwengu: haupendi kama ilivyo sasa na sisi pia hatupendi!

Watoto wengi sana wanakabiliwa na njaa, vita, ubaguzi wa rangi na mikasa ya kimazingira. Tungependa ulimwengu wa haki zaidi, usio na migawanyiko kati ya watu, kati ya matajiri na maskini, kati ya vijana na wazee. Dunia ambayo pia ni safi zaidi, ambayo uchafuzi wa mazingira hauharibu misitu, unachafua bahari na kuua wanyama wengi, tumeelewa kuwa ni muhimu zaidi kuokoa Dunia kuliko kuwa na pesa nyingi.  Tungependa ulimwengu kwa kila mtu, mahali ambapo hakuna mtu aliyetengwa! Ulimwengu ambao watoto wote  wakue vizuri, wasome, wacheze na waishi kwa amani. Tunataka amani! Hatutaki kuishi katika ulimwengu wenye vita.

Vita haipaswi kupiganiwa, havitumiki kwa kusudi lolote: vinaharibu, vinaua na vinafanya kila mtu kuwa na huzuni, lakini baadhi ya watu wakuu bado hawajui hili! Pamoja na wewe tunataka kusafisha dunia kutokana na mambo mabaya, kuipaka rangi kwa urafiki na heshima, na kukusaidia kujenga mustakabali mzuri wa kila mtu! Je, ni vigumu? Lakini ukitusaidia inakuwa rahisi!

"Watoto wako." Ndivyo inavyohitimishwa barua hiyo ya watoto.

Hitimisho la mkutano wa haki za watoto
03 Februari 2025, 17:35