Papa atoa wito kwa watawala wakristo:katika Jubilei suluhisheni mizozo inayoendelea
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana Dominika tarehe 2 Februari 2025, Baba Mtakatifu Francisko alisema kuwa: Leo, nchini Italia, inaadhimisha Siku ya Maisha, yenye mada "Kusambaza maisha, matumaini kwa ulimwengu." Ninaungana na Maaskofu wa Italia katika kutoa shukrani kwa familia nyingi zinazokaribisha kwa hiari zawadi ya maisha na katika kuwatia moyo wanandoa vijana wasiogope kuzaa watoto duniani. Na ninasalimia Jumuiya ya Pro-Life ya Italia, ambayo inaadhimisha miaka 50 tangu ilipoanzishwa.” “Hongera!” Papa alisema.
Mkutano wa haki za Watoto
Baba Mtakatifu akiendelea alitangaza kuwa: “kuna Mkutano wa Kimataifa wa Haki za Watoto, wenye kichwa “Tuwapende na Tuwalinde,” ambao nilipata furaha kuu kuutangaza na ambao nitashiriki, utafanyika tarehe 3 Februari mjini Vatican. Ni fursa ya kipekee ya kuleta usikivu wa ulimwengu masuala ya dharura zaidi yanayoathiri maisha ya watoto. Papa Francisko amewaalika wote tushiriki kuombea mkutano huo mafanikio yake.”
Wito wa kuombea amani
Papa Francisko kama kawaidia kuhusu migogoro ya kidunia alisema “Na katika kuzungumza juu ya thamani ya msingi ya maisha ya mwanadamu, ninarudia kusema "hapana" yangu kwa vita, ambayo huharibu, kuharibu kila kitu, kuharibu maisha na kusababisha kudharau. Na tusisahau kwamba vita daima ni kushindwa.” Kwa kuongezea alisema “Katika Mwaka huu wa Jubilei, ninarudia ombi langu, hasa kwa viongozi wa Kikristo, kufanya kila juhudi kusuluhisha mizozo yote inayoendelea. Hebu tuombe kwa ajili ya amani katika mateso Ukraine, Palestina, Israel, Lebanon, Myanmar, Sudan, Kivu Kaskazini.”
Salamu mbali mbali kwa mahujaji
Salamu kwa wote, kutoka Italia na sehemu nyingine za dunia. Salamu hasa waamini wa Valencia, Barcelona, Seville; wanafunzi wa Taasisi ya “Rodríguez Moñino” ya Badajoz, Hispania, na zile za "École Wila ya Marseille; kundi la parokia kutoka Nanterre na wale kutoka Poland, Kroatia, Bulgaria na India. Salamu kwa Vijana wa Kutoka parokia ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili. Salamu kwa waamini wa Cantù, Vighizzolo, Seregno na Cologno Monzese; Unitalsi Jimbo la Camerino- Mtakatifu Severino Marche; Skauti wa Nola na wanachama Club ya Kimataifa ya wa Serra. Salamu kwa watumikiaji wa Altareni kutoka jJumuiya ya kichungaji Malkia wa Mitume jimbo Kuu la Milano, Italia. Na kwa Wote aliwatakia Dominika njema na tafadhali wasisahau kumuombea.