Tafuta

2024.11.28 Papa amkutana na wawakilishi wa Watawa wa kike na Kiume wa Familia ya Calasanzi. 2024.11.28 Papa amkutana na wawakilishi wa Watawa wa kike na Kiume wa Familia ya Calasanzi.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa kwa Wakalasanzi:Saidieni vijana kujenga mahusiano ya kweli

Akikutana na watawa wa kike na kiume pamoja na walei kike na kiume waliounganishwa na karama ya Mtakatifu Joseph Calasanz,mwanzilishi wa Shule za Wacha Mungu na Shirika la Mapadre wa Piarist,katika maadhimisho ya miaka 75 kuundwa kwao,amewaalika kudumisha talanta yao katika utunzaji wa ukuaji fungamani wa mtu,katika ulimwengu unaosukuma vijana kuelekea mgawanyiko wa hisia na kuelekea ubinafsi.Papa amewataka kusisitiza mahusiano ya kawaida na siyo ya mitandaoni.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 28 Novemba 2024 alikutana na wajumbe wa Familia ya Calasanziani katika kuadhimisha miaka 75 tangu kuundwa kwake ambapo  familia hiyo inawaleta wao pamoja katika karama ya elimu ya Msimamizi wa Ulimwengu wa  shule zote maarufu za Kikristo, Mtakatifu Joseph Calasanz, na pia kwa kuzingatia miaka mia moja ya kifo cha waanzilishi wao, Mtakatifu Faustino Míguez na Mwenyeheri Celestina Donati. Bwana aliongoza Mtakatifu Joseph Calasanz kujitolea maisha yake kwa elimu ya vijana, hasa wadogo na maskini, kama “Malaika wao mlinizi,” kwa kutumia usemi ambao Yeye mwenyewe alipenda kufafanua utume wake kama  mwalimu ;Malaika mlinzi ni nzuri. Papa Fracisko aliendelea kusema kuwa wanaendeleza  kazi yake, ambayo wakati huo huo, kwa karne nyingi, imeenea katika mabara manne. Kwa hivyo Papa alipenda kusisitiza, katika hafla hiyo ya furaha, vipengele viwili vya asili yao ambavyo ameona kuwa muhimu kwao na kwa maisha yao ya baadaye: kipengele cha kwanza, unyenyekevu wa ujasiri kwa Mungu mpaji; kipengele cha pili, utunzaji wa ukuaji fungamani wa mtu.

Kwanza: unyenyekevu wa ujasiri kwa Mungu mpaji. Mwanzilishi wao, kutoka katika familia tajiri, labda aliyekusudiwa kwa kazi ya kikanisa na alikuja Roma na majukumu ya kiwango fulani, hakusita kupindua programu na mitazamo ya maisha yake kujitolea kwa watoto wa mitaani aliokutana nao mjini na ndivyo  Shule za Wacha Mungu zilivyozaliwa: sio kwa sababu ya mpango uliotanguliwa na kuhakikishwa sana, lakini kwa sababu ya ujasiri wa kuhani mwema ambaye alijiruhusu kuhusika katika mahitaji ya wengine, ambapo Bwana aliwaweka mbele yake.

Hili ni zuri sana, na Papa alipenda pia kuwaalika kudumisha uwazi na wepesi sawa katika uchaguzi wao, bila kuhesabu kupita kiasi, kushinda woga na kusitasita, hasa katika uso wa aina nyingi mpya za umaskini wa siku zetu (taz. .Waraka wa Kitume Evangelii gaudium, 210). "Umaskini mpya ... na itakuwa vizuri ikiwa leo au kesho, moja ya siku hizi, katika mkutano wao, wajaribu kuelezea umaskini mpya, yaani nini maana ya  umaskini mpya.”Papa amewaomba wasiogope kujitosa katika njia ambazo ni tofauti na zile ambazo tayari zilifuatwa zamani, ili kujibu mahitaji ya maskini, hata kwa gharama ya kupitia  mifumo mipya  na kupunguza matarajio. Ni katika kuachwa huku kwa ujasiri ambapo mizizi yao iko, na kwa kubaki waaminifu wataweka karama yao hai.

Kipengele cha pili: utunzaji wa ukuaji fungamani wa  mtu. Ubunifu mkubwa wa Shule za Wacha Mungu ulikuwa ni kufundisha vijana maskini, pamoja na ukweli wa imani, pia masomo ya elimu ya jumla, kuunganisha mafunzo ya kiroho na kiakili ili kuandaa watu wazima waliokomaa na wenye uwezo. Ilikuwa chaguo la kinabii wakati huo, halali kabisa hata sasa. Katika suala hilo Papa alipenda kuzungumza juu ya kuunda umoja, wa Kiakilini na kimwili kwa mtu yaani kuwa na akili tatu. Kuanzia mikono, kwa hivyo tunaweza kufanya na  mikono yetu kile tunachohisi na kufikiria, kuhisi kile tunachofikiria na kutenda, kufikiria kile tunachohisi na kutenda. Kuna uhitaji wa haraka sana leo hii kuwasaidia vijana kufanya aina hii ya awali, umoja wa usawa wa akili tatu, “kuunda umoja” ndani yao wenyewe na kwa wengine, katika ulimwengu unaowasukuma zaidi na zaidi katika mwelekeo wa kugawanyika hisia na utambuzi na ubinafsi katika mahusiano. Na kwa jambo hili, Papa ameomba wasisitize zaidi juu ya mahusiano ya “kawaida", ya kutazamana machoni na sio mahusiano ya mtandaoni kupitia simu za mkononi.

Papa aliongeza kusema “Askofu mmoja aliniambia kuwa binamu zake alikuja na kumwalika kwenye chakula cha mchana kwenye mgahawa mmoja. Dominika wakiwa  katika  meza,  karibu na meza hiyo kulikuwa na familia: baba, mama, mwana na binti, wote wanne na simu za mkononi, hawakuzungumza  pamoja. Yule Askofu asiye na subira  aliinuka, akakaribia na kusema: “Lakini, tazameni ninyi ni , familia nzuri, lakini kwa nini mnazungumza kwenye simu yenu ya mkono  na kwa nini hamzungumzo mmoja na mwingine kwa sababu ni vuzri zaidi? Walimsikiliza, lakini hawakujali na wakaendelea kuzungumza. Papa aliongeza kusema: “Hii ni mbaya, ukosefu wa ubinadamu. Kwa hiyo akili tatu. Na hii ni muhimu kwa watoto kufanya umoja huu ndani yao, na wengine na ulimwengu. Mtindo muhimu wa elimu ni "kipawa cha karama" muhimu sana ambacho Mungu amewakabidhi, ili waweze kukitumia kadiri ya uwezo wao kwa faida ya wote.

Papa Francisko alipenda kumalizia kwa kusisitiza kipengele kimoja cha mwisho cha uwepo wao hapo kile cha: kutembea pamoja. Hakika alifurahi sana kuona jinsi wao wote kama  wanaume kwa wanawake, waliowekwa wakfu pamoja na walei katika kumsikiliza Roho, walihisi hitaji la "kuunda familia", kuunganisha juhudi zao na kushiriki uzoefu wao katika mtandao wa upendo, kwa ajili ya huduma ya ndugu zao (Christus vivit, 222). Ni mtindo wa Yesu (Mk 3,14-15; Mt 18,20), na pia ni mtindo wa Kanisa (Lumen gentium, 7; Gaudium et spes, 92). Papa amewashukuru kwa hilo na kwa kile wafanyacho. Amewabariki kutoka dani ya moyo wake na kuwaomba pia wamwombee.

Papa kwa shirika la Clazanzi
28 November 2024, 16:59