Tafuta

2024.11.28 Papa amekutana na Tume ya Kitaalimungu Kimataifa. 2024.11.28 Papa amekutana na Tume ya Kitaalimungu Kimataifa.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko:Ulimwengu unahitaji udugu na kumweka Yesu katikati

Akikutana na Tume ya Kitaalimungu Kimataifa,ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba katika Ulimwengu mgumu uliojaa vurugu,upendo wa Mungu katika Kristo unatoa mwaliko wa kuwa wajenzi wa amani na haki na kukabidhi udugu wa kweli wa maadili msingi.Mkutano kuhusu undelezaji wa Taalimungu ya Kisinodi unahusiana na watu wote wa Kanisa.Papa alieleza shauku ya kutaka kwenda Nikea 2025 kwa ajili ya Jubilei ya 1700 ya Mtaguso.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 28 Novemba 2024 amekutana na Tume ya Kitaalimungu ya Kimataifa mjini Vatican, akianza hotuba yake amesema kuwa “tunakaribia kufungua Mlango Mtakatifu wa Jubilei na hivi karibuni tumehitimisha Mkutano wa Kawaida wa XVI wa Sinodi ya Maaskofu. Kuanzia katika matukio haya mawili ndipo Papa amependa kuzungumzia mawazo mawili kwao: la kwanza ni kumweka Kristo tena katikati, la pili ni kuendeleza taalimungu  ya sinodi.” Papa alianza na kipengele cha  “Kumrudisha Kristo katikati.” Jubilei inatualika kuufunua upya uso wa Kristo na kujikita tena ndani Yake. Na katika Mwaka huu Mtakatifu, tutapata fursa pia ya kuadhimisha mwaka wa 1700 wa Mkutano Mkuu wa  kwanza la Kiekumene, wa  Nikea.

Papa Francisko amesema anavyofikiria kwenda huko. Mtaguso huu unajumuisha hatua muhimu katika safari ya Kanisa na pia ya wanadamu wote, kwa sababu imani katika Yesu, Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili kwa ajili yetu wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu, iliundwa na kudaiwa kuwa ni nuru inayoakisi maana ya ukweli na hatima ya historia yote. Kwa hiyo Kanisa liliitikia mwaliko wa mtume Petro: “Mwabuduni Bwana Kristo mioyoni mwenu, mkiwa tayari siku zote kumjibu mtu awaye yote awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu” (1 Pt 3:15). Papa amesisitiza kuwa  himizo hili, ambalo linaelekezwa kwa Wakristo wote, linaweza kutumika kwa namna ya pekee kwa huduma ambayo wataalimungu wameitwa kutekeleza kama huduma kwa Watu wa Mungu: inaweza kuhimiza kukutana na Kristo, kuimarisha maana ya fumbo lake, ili tuweze kuelewa vizuri zaidi “ulivyo upana na urefu na kimo na kina, na kuujua upendo wa Kristo upitao ujuzi wote” (Ef 3:18-19 ) .

Mtaguso wa Nikea, ukithibitisha kwamba Mwana ni kitu kimoja na Baba, unaakisi jambo muhimu: katika Yesu tunaweza kuujua uso wa Mungu na, wakati huo huo, pia uso wa mwanadamu, tukigundua kwamba sisi ni watoto,  wana na ndugu kati yetu. Udugu, wenye mizizi ndani ya Kristo, ambao unakuwa kazi ya kimsingi ya kimaadili kwetu. Ni muhimu, basi, kwamba katika mkutano wao sehemu kubwa imejitolea ya Mjadala kufanyia kazi hati inayolenga kuonesha maana ya sasa ya imani ya kule  Nikea. Na hati hii inaweza kuwa ya thamani, katika mwaka wa Jubilei, kulisha na kuimarisha imani ya waamini na, kuanzia sura ya Yesu, pia kutoa mawazo muhimu na tafakari kwa dhana mpya ya kiutamaduni na kijamii, iliyoongozwa hasa na ubinadamu wa Kristo.

Leo hii Papa amesema kiukweli, katika ulimwengu mgumu na ambao mara nyingi umechanganyikiwa, unaoakisiwa sana na migogoro na vurugu, upendo wa Mungu ambao umefunuliwa katika Kristo na kutolewa kwetu katika Roho unakuwa wito unaoelekezwa kwa kila mtu, ili tujifunze kutembea katika udugu na kuwa wajenzi wa haki na amani. Ni kwa njia hiyo tu tunaweza kueneza mbegu za tumaini mahali tunapoishi. Na kumweka Kristo katikati ina maana ya kuwasha upya tumaini hili na taalimungu inaitwa kufanya hivyo, katika kazi ya mara kwa mara na ya busara, katika mazungumzo na aina nyingine zote za ujuzi. Baba Mtakatifu Francisko akiendelea amedadavua sehemu ya pili ya tafakari kuhusu ‘kuendeleza taalimungu ya sinodi.’ Mkutano wa  Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu uliweka sehemu ya Hati ya Mwisho kwa kazi ya Taalimungu, katika muktadha wa “karama, miito na huduma kwa ajili ya utume”; na kuunda tumaini hili kwamba : “Mkutano unakaribisha taasisi za kitaalimungu kuendelea na utafiti unaolenga kufafanua na kuimarisha maana ya sinodi” (n. 67).

“Na haya yalikuwa maono ya Mtakatifu Paulo VI mwishoni mwa Mtaguso  alipounda Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu. Ukiwa na umri wa karibu miaka 60, taalimungu  hiyo ya sinodi ilisitawi, hatua kwa hatua. Na leo hii tunaweza kusema kwamba ni kukomaa. Na hatuwezi leo hii kufikiria huduma ya kichungaji bila mwelekeo huu wa sinodi.” Kwa hiyo, pamoja na ukuu wa Kristo, Papa amewaalika pia kukumbuka mwelekeo wa kikanisa, ili kuendeleza vyema madhumuni ya kimisionari ya sinodi na ushiriki wa Watu wote wa Mungu katika aina mbalimbali za tamaduni na mila. Papa amekazia kusema kwamba wakati umefika wa kuchukua hatua ya kijasiri: kuendeleza taalimungu ya sinodi, tafakari ya kitaalimungu inayosaidia, kutia moyo na kusindikiza mchakato wa sinodi, kwa ajili ya hatua mpya ya kimisionari, yenye ubunifu zaidi na ya kuthubutu, ambayo inaongozwa na kerygma na ambayo inahusisha vipengele vyote vya Kanisa.

Papa amefafanua kuhusu  shauku kwamba wawe kama mtume Yohane ambaye, kwa ujasiri wake kama mfuasi mpendwa, aliweka kichwa chake karibu na moyo wa Yesu (Yh 13:25). Kama alivyokumbuka katika Waraka wa Kitume wa Dilexit nos, Moyo Mtakatifu wa Yesu “ndiyo kanuni ya kuunganisha  ukweli, kwa sababu “Kristo ndiye moyo wa ulimwengu; Pasaka yake ya kifo na ufufuko ni kitovu cha historia, ambapo shukrani kwake ni historia ya wokovu” (n. 31). Kwa kubaki na huku wakiungwa mkono na Moyo wa Bwana, taalimungu yao itachota kutoka kwenye chanzo na kuzaa matunda katika Kanisa na ulimwenguni! "Na jambo la msingi sana kufanya taalimungu yenye matunda sio kupoteza hisia zao za ucheshi. Hii inasaidia sana. Roho Mtakatifu ndiye anayetusaidia katika hali hii ya furaha na ucheshi.” Papa Francisko kwa njia hiyo amewashukuru tena kwa huduma yao. Anawasindikiza kwa Baraka na tafadhali wamwombee. Amehitimisha.

Papa tume kimataifa ya Taalimungu
28 November 2024, 17:28