Papa Francisko:Nyakati zetu zisizo na amani zinahitaji Mama ambaye huleta familia pamoja
Na Angella Rwezaula - Vatican.
Katika Ibada ya Misa Kuu Takatifu ya Siku Kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, sambamba na Siku ya 57 ya Amani Kardinali, Pietro Parolin, Katibu wa Vatican katika Kanisa Kuu la Petro na kuudhuriwa na waamini, majujaji na viongozi kadhaa kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, baada ya kusomwa masomo na Injili ya Siku inayofafanua kuzaliwa kwa Bwana amesema "Maneno ya mtume Paulo yanaangazia mwanzo wa mwaka mpya: “Hata utimilifu wa wakati ulipowadia, Mungu alimtuma Mwanawe aliyezaliwa na mwanamke” (Gal 4:4). Usemi wa “mtimilifu wa wakati” unashangaza. Katika nyakati za kale ilikuwa ni desturi ya kupima muda kwa kumwaga na kujaza vyungu: wakati vilikuwa vitupu kipindi kipya kilianza, ambacho kiliisha wakati vilikuwa vimejaa. Huu ndio utimilifu wa wakati: wakati chungu cha historia kimejaa, neema ya kimungu inafurika: Mungu anakuwa mwanadamu na hufanya hivyo kwa jina la mwanamke, Maria.
Yeye ndiye njia iliyochaguliwa na Mungu; yeye ni hatua ya kuwasili kwa watu wengi na vizazi ambao, "tone kwa tone", wametayarisha ujio wa Bwana ulimwenguni. Kwa hivyo Mama yuko katikati ya wakati: Mungu alifurahi kufanya historia igeuke kupitia yeye, mwanamke. Kwa neno hili, Maandiko yanatuelekeza kwenye asili, katika Mwanzo, na kupendekeza kwamba Mama aliye na Mtoto anaashiria uumbaji mpya, na mwanzo mpya. Kwa hiyo mwanzoni mwa wakati wa wokovu kuna Mama wa Mungu, Mama yetu mtakatifu. Ni vizuri basi mwaka unafunguliwa kwa kumwomba; Inapendeza kwamba watu waamini, kama ilivyokuwa huko Efeso - Wakristo hao walikuwa na ujasiri ... - walitangaza kwa furaha Mama Mtakatifu wa Mungu. Maneno ya Mama wa Mungu kiukweli yanaonesha uhakika wa furaha kwamba Bwana, Mtoto mpole aliye katika mikono ya mama yake, ameungana milele na ubinadamu wetu, kwa uhakika kwamba si wetu tena, bali ni wake. Mama wa Mungu: maneno machache kwa kukiri muungano wa milele wa Bwana pamoja nasi. Mama wa Mungu: ni fundisho la imani, lakini pia ni "dogma ya matumaini": Mungu ndani ya mwanadamu na mwanadamu ndani ya Mungu, milele. Mama Mtakatifu wa Mungu.
Katika utimilifu wa wakati Baba alimtuma Mwanawe aliyezaliwa na mwanamke; lakini andiko la Mtakatifu Paulo linaongeza utume wa pili kuwa: “Mungu alituma mioyoni mwetu Roho wa Mwana wake, ambaye analia: “Abba! Baba!” (Gal 4:6). Na hata katika kutumwa kwa Roho, Mama ndiye mhusika mkuu: Roho Mtakatifu anaanza kutulia juu yake katika Matamshi (taz Luka 1:35), kisha mwanzoni mwa Kanisa alishuka juu ya Mitume waliokusanyika katika maombi “na Maria, Mama” (Mdo 1:14). Kwa hivyo ukaribisho wa Maria ulituletea zawadi kuu zaidi: “alimfanya Bwana wa ukuu kuwa ndugu yetu” (TOMMASO WA CELANO, Maisha ya pili, CL, 198: FF 786) na kumruhusu Roho alie mioyoni mwetu: “Abba, Baba!. ” Umama wa Maria ni njia ya kukutana na huruma ya ubaba wa Mungu, njia ya karibu zaidi, ya moja kwa moja na rahisi zaidi. Papa amerudia kusema: “Tusisahau hili... Umama wa Maria ni njia ya kukutana na huruma ya Ubaba wa Mungu, njia ya karibu zaidi, ya moja kwa moja, iliyo rahisi zaidi, na hii ambayo ni mtindo wa Mungu: ukaribu, huruma, na huruma.”
Mama kwa hakika, atuongoza kwenye mwanzo na moyo wa imani, ambayo si nadharia au ahadi, lakini imani ni zawadi kubwa, ambayo inatufanya kuwa watoto wapendwa, nyumba za upendo wa Baba. Kwa hiyo kumkaribisha Mama katika maisha ya mtu si chaguo la ibada, bali ni hitaji la imani: "Ikiwa tunataka kuwa Wakristo, lazima tuwe wa Maria”, yaani, watoto wa Maria.”(Mtakatifu PAULO VI, Mahubiri huko Cagliari, 24 Aprili 1970). Kanisa linamhitaji Maria ili kugundua tena sura yake ya kike: kuwa zaidi kama yeye ambaye, kama mwanamke, Bikira na Mama, anawakilisha kielelezo chake na umbo kamilifu (taz. Lumen gentium, 63); kutoa nafasi kwa wanawake na kuwa na tija kwa njia ya huduma ya kichungaji inayojumuisha utunzaji na kujali, uvumilivu na ujasiri wa kina wa mama. Lakini ulimwengu pia unatakiwa kuwatazama akina mama na wanawake ili kupata amani, waepuke kutoka katika mizunguko ya jeuri na chuki na kurejea kuwa na mtazamo na mioyo ya kibinadamu inayoona.
Na kila jamii inahitaji kukaribisha zawadi ya mwanamke, ya kila mwanamke: kumheshimu, kumlinda, kumthamini, kujua kwamba yeyote anayemdhuru mwanamke mmoja anamkufuru Mungu, aliyezaliwa na mwanamke. Baba Mtakatifu Francisko ameeleza kuwa Maria, mwanamke, kama vile alivyostahiki katika utimilifu wa wakati, ndivyo anavyoamua katika maisha ya kila mtu; kwa sababu hakuna ajuaye nyakati kuliko Mama na anajua dharura za watoto wake. Hii inaoneshwa kwetu kwa mara nyingine tena na “mwanzo,” ishara ya kwanza iliyofanywa na Yesu, kwenye harusi ya Kana. Hapo ndipo Maria anayeona kwamba divai haipo na kumgeukia (taz.Yh 2:3). Mahitaji ya watoto wake ndiyo yanayomsukuma, Mama, kumsukuma Yesu kuingilia kati. Na huko Kana Yesu alisema: “Jazeni maji mabarasi; wakayajaza hadi pomoni”(Yn 2:7). Maria, ambaye anajua mahitaji yetu, pia anaharakisha kufurika kwa neema kwa ajili yetu na kuleta maisha yetu kuelekea utimilifu.
Baba Mtakatifu amesisitiza kuwa sisi sote tuna mapungufu, tuna upweke, mapengo ambayo yanaomba kujazwa. Kila mmoja wetu anajua yake. Ni nani awezaye kuyajaza kama sio Maria, Mama wa utimilifu? Tunapojaribiwa kujifungia ndani, tumwendee; wakati hatuwezi kujinasua kutoka katika mafundo ya maisha, tutafute kimbilio kwake. Nyakati zetu, zisizo na amani, zinahitaji Mama anayeleta familia ya kibinadamu pamoja. Tumtazame Maria kuwa wajenzi wa umoja, na tufanye hivyo kwa ubunifu wake kama Mama, anayewatunza watoto wake: anawakusanya pamoja na kuwafariji, anasikiliza huzuni zao na kukausha machozi yao. Na tunapotazama Picha iliyowekwa mbele, ya Mama anayenyonyesha, hivyo ni mama... Ni kwa kiasi gani cha huruma anachotuangalia na yuko karibu nasi. Anatutunza na yuko karibu nasi." Papa amesisitiza.
Tuukabidhi mwaka mpya kwa Mama wa Mungu. Tuweke wakfu maisha yetu kwake. Yeye, kwa huruma, ataweza kufunua utimilifu wake. Kwa sababu atatuongoza kwa Yesu na Yesu ndiye utimilifu wa wakati, wa wakati wote, wa wakati wetu, wa wakati wa kila mmoja wetu. Kiukweli, kama ilivyoandikwa, “si utimilifu wa wakati uliosababisha Mwana wa Mungu kutumwa, bali kinyume chake, kwa kutumwa Mwanae kulileta utimilifu wa wakati” (taz M. LUTHER, M. Vorlesung über den Galaterbrief 1516-1517, 18). Papa Francisko kwa njia hiyo amesema mwaka huu uwe umejaa faraja ya Bwana; mwaka huu ujazwe na huruma ya uzazi ya Maria, Mama Mtakatifu wa Mungu. Na hivyo amewaalika kusema kwa pamoja mara: Mama Mtakatifu wa Mungu! Pamoja: Mama Mtakatifu wa Mungu! Mama Mtakatifu wa Mungu! Mama Mtakatifu wa Mungu!" Amehitimisha.