Tume ya Mashuhuda Wapya wa Imani: 2000-2023: Kuna Mashuhuda 550
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kazi ya Roho Mtakatifu ni kuwafundisha na kuwaongoza waamini katika: Ushirika na umoja unaofumbatwa kwenye utofauti. Roho Mtakatifu ni chemchemi ya uekumene wa sala, huduma, maisha ya kiroho sanjari na uekumene wa damu! Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani; wa kimisionari, shughuli za kichungaji na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita na kusimama dede: Kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kumbe, kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025, waamini wanahamasishwa kujikita katika sala, chemchemi ya baraka na neema zote. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Julai 2023 ameanzisha Tume ya Mashahidi Wapya, Mashuhuda wa Imani kwenye Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu.
Lengo ni kuandaa orodha ya majina ya waamini walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ikumbukwe kwamba, Wafiadini ndani ya Kanisa ni Mashuhuda wa matumaini yanayobubujika kutoka katika Injili ya Kristo Yesu na kukita mizizi yake katika upendo wa kweli. Tumaini upyaisha imani ya kina na kwamba, wema una nguvu kuliko uovu, kwa sababu Mwenyezi Mungu katika Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti. Tume ya Mashahidi Wapya, hivi karibuni imefanya kikao chake cha kwanza na kubainisha kwamba, kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2023 kuna mashuhuda wapya wa imani 550 ambao vifo vyao vinatambulikana sanjari na maisha na utume wao kwa watu wa Mungu. Kwa sasa Tume inaandaa wavuti itakayotoa habari muhimu kuhusiana na Mashuhuda wapya wa imani. Tume inajielekeza zaidi huko Mashariki ya Kati na Barani Asia, kwa kukazia uekumene wa damu, sala na huduma. Tume ya Mashahidi Wapya, Mashuhuda wa Imani kwenye Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu itaendeleza orodha ya wafia imani wanaotambulika rasmi na Mama Kanisa na shuhuda zao zilizohifadhiwa ili kwa pamoja waweze kutambulikana kuwa ni “Mashuhuda Wakristo” “Martyria.” Tume hii inatarajia kupata ushirikiano wa dhati kutoka kwenye Makanisa mahalia, Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume pamoja na ukweli unaobubujika kutoka kwa Makanisa yote ya Kikristo.
Katika ulimwengu mamboleo, uovu unaonekana kutawala zaidi! Kumbe Orodha ya Mashuhuda wapya wa imani katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, itakuwa ni msaada mkubwa katika mwanga wa Pasaka ya Bwana, wakichota kutoka huko uaminifu mwingi wa ukarimu kwa Kristo Yesu kwa sababu za maisha na wema. Askofu Fabio Fabene, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu akishirikiana na Professa Andrea Riccardi wamepitia tafiti mbalimbali na hivyo kuandaa dira na mwongozo kwa siku za usoni, kwa kuwasilisha majina ya waamini mashuhuda waliosadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Hawa ni mashuhuda wa Injili ya huduma na upendo; vyombo vya haki, amani na upatanisho, mwanga wa matumaini na sauti pevu inayowataka waamini kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kujenga na kuimarisha umoja na ushirika wa watu watakatifu wa Familia ya Mungu.