Vita Sudan ya Kusini Vinaendelea Kusababisha Madhara Makubwa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) linasema kwamba, takriban watu zaidi ya milioni 5.6 wamekimbia makazi yao Sudan ya Kusini baada ya kupamba moto kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo kwa mara nyingine tena mwezi Aprili mwaka 2023. Mapambano haya ni kielelezo cha uchu wa mali na madaraka. Ni vita kati ya Majenerali wawili Abdel Fattah al-Burhan, kiongozi wa Kikosi cha Wanajeshi wa Sudan (SAF), na Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti, mkuu wa Kikosi cha Dharura (RSF). Majenerali wawili hao walifanya kazi pamoja, na kufanya mapinduzi pamoja sasa vita vyao vya kuwania madaraka vinasaimbaratisha Sudan ya Kusini.
Vita hii ya wenyewe kwa wenyewe ni ya waasimu wawili. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 12 Novemba 2023 amesema hali ya vita nchini Sudan ya Kusini kwa sasa ni tete na kwamba, anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wahanga wa vita hii na anapenda kutoa wito kwa wahusika wakuu wa vita hii ya wenyewe kwa wenyewe, kuwajibika barabara ili kuhakikisha kwamba misaada ya kiutu inawafakia waathirika wa vita. Na kwa msaada wa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waweze kupata suluhu ya amani.
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema: Amani ya kweli ni chachu ya maendeleo ya watu na kwamba, kinzani, misigano na utaifa usiokuwa na mashiko ni mambo yanayotishia amani. Kumbe, vita, migogoro na kinzani mbalimbali zinaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kujikita katika: sheria, haki, usawa, upendo; ukweli na uhuru, tunu ambazo zinaonesha umuhimu wa pekee hata katika ulimwengu mamboleo. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia kutotumia nguvu kuwa ndio unaopaswa kuwa ni mtindo wa maisha ya kisiasa ili kujenga na kudumisha amani duniani na anamwomba Mwenyezi Mungu awasaidie watu kuchota tunu hizi msingi kutoka katika undani wa maisha yao.
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amezungumzia kuhusu hali tete kati ya Israel na Palestina na kwamba, anasali huku akiwakumbuka wahanga wote wa vita hii. Amewasihi Waisraeli na Wapalestina kuachana na vita na hivyo kuanza kujikita katika mazungumzo yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Iwe ni fursa ya kuwaachilia huru wafungwa na mateka wa vita na kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu na watu wana haki ya kuishi katika mazingira ya haki na amani. Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wenye mapenzi mema kutokata tamaa, bali waendelee kusali kwa ajili ya kuombea amani.