Papa Francisko: Utakatifu Fungamanishi, Maisha ya Kifamilia na Mashuhuda wa Imani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” anasema, utakatifu ni mwaliko kwa waamini wote na wala si kwa watu wachache tu ndani ya Kanisa! Huu ni wito wa kuongeza jitihada za kukutana na Kristo Yesu katika maisha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata: huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Watakatifu ni watu wa kawaida kabisa, ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu, leo hii wamekuwa ni marafiki zake wa karibu! Watakatifu ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wamejichukulia dhamana ya kuanza safari ya utakatifu wa maisha! Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 16 Novemba 2023 limeendesha Kongamano la Kimataifa, lililonogeshwa na kauli mbiu “Kipimo cha Utakatifu wa Kijumuiya.”
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 16 Novemba 2023 alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na washiriki wa kongamano hili na kukazia mambo msingi yafuatayo: wito wa jumla wa utakatifu wa maisha; Utakatifu unaowafungamanisha waamini, Utakatifu wa maisha ya kifamilia pamoja na Utakatifu wa mashuhuda wa imani. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, utakatifu ni wito kwa watu wote wa Mungu, ili waweze kuwa wakamilifu kama Baba yao wa Mbinguni alivyo mkamilifu. Ili kufikia azma hii, wanapaswa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao Matunda ya Roho Mtakatifu sanjari na kuomba neema ya kusamehe na kusahau. Huu ni mchakato wa utakatifu unaosimikwa katika maisha ya kila mmoja, kwa kutumia vyema na kwa uaminifu karama na vipawa katika utekelezaji wa majukumu na hivyo kusonga mbele bila kusitasita katika safari ya imani iliyo hai, iamshayo matumaini na kutenda kwa mapendo. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa ni mfano na kielelezo cha utakatifu wote.
Ni katika muktadha huu, kumekuwepo na ongezeko kubwa la Mama Kanisa kuwatangaza waamini kutoka medani mbalimbali za maisha kuwa ni wenyeheri na watakatifu. Kuna majirani ambao ni watakatifu na wanatenda matendo ya huruma: kiroho na kimwili na kwamba, wanaendelea kumfuasa Kristo Yesu katika maisha yao ya kila siku. Utakatifu unaowafungamanisha waamini na kuitwa kufikia utimilifu wa maisha ya Kikristo na ukamilifu wa upendo na kwamba, kila mtu anaitwa kwa jina na kwa ajili ya utume maalum kama ilivyokuwa kwa Abrahamu, Mtume Petro na Paulo; na kwa Mathayo mtoza ushuru. Kumbe, kukutana na Kristo Yesu kunatoa mwelekeo wa kijumuiya. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume: “C'est la Confiance” yaani “Ni Uaminifu” uliotolewa kwa heshima ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwake huko Alençon nchini Ufaransa anasema, Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu anaonesha jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa: Upendo na imani katika huruma ya Mungu na kwamba, upendo uwasukume waamini kuwahudumia ndugu na jirani zao. Huu ni uinjilishaji wenye mvuto na mashiko unaosimikwa katika ushuhuda wa upendo unaowaunganisha waamini wote katika upendo, umoja na amani.
Pili, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu inaonesha ule Utakatifu wa maisha ya kifamilia na kwamba, hata leo hii, Mama Kanisa anaweka mbele ya macho ya waamini watu wa ndoa kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko; watu wanaojibidiisha kutakatifuzana. Mfano ni Watakatifu Luigi na Zelia Martin, Maria Beltrame Quattrocchi: Hawa ni mashuhuda wa utakatifu wa maisha ya ndoa na kwamba, kuna mchakato unaoendelea wa kuwatangaza kuwa wenyeheri Jozef na Wiktoria Ulma na watoto wao saba kutoka Poland waliouwawa kikatili wakati wa utawala wa Kinzai ni ushuhuda kwamba, utakatifu ni hija ya maisha ya kijumuiya. Tatu ni Utakatifu wa mashuhuda wa imani unaopata chimbuko lake tangu mwanzo wa Kanisa hadi nyakati hizi mfano ni Asia Bibi kutoka India, aliyekuwa amefungwa gerezani, lakini aliendelea kupelekewa Ekaristi Takatifu na binti yake kwa muda wa miaka tisa, hadi pale Mahakama ilipomwona kwamba, hana hatia. Huu ni ushuhuda wa imani na mapendo. Wapo pia waungama imani na mashuhuda wa imani kiekumene walioandikwa kwenye Kitabu cha Mashuhuda wa Imani wa Kirumi “Martirologio romano.” Kumbe hii ni hija ya pamoja na utimilifu wa upendo.