Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume uliowekwa kwenye mfumo wa Barua binafsi: “Motu proprio” wa "Ad theologiam promovendam" yaani “Kukuza Taalimungu.” Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume uliowekwa kwenye mfumo wa Barua binafsi: “Motu proprio” wa "Ad theologiam promovendam" yaani “Kukuza Taalimungu.”   (Vatican Media)

Papa Francisko Waraka Wa Kitume Motu Proprio: Kukuza Taalimungu

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume uliowekwa kwenye mfumo wa Barua binafsi: “Motu proprio” wa "Ad theologiam promovendam" yaani “Kukuza Taalimungu.” Lengo ni kutoa tafsiri ya kinabii mintarafu mwanga wa Ufunuo wa Kimungu, ili Taalimungu iweze kushughulikia mabadiliko makubwa ya kitamaduni kwa kufahamu kwamba, Zama za sasa zinapitia mabadiliko makubwa, kumbe kuna haja ya kuwa na fikra mpya pamoja na mbinu mkakati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume uliowekwa kwenye mfumo wa Barua binafsi: “Motu proprio” wa "Ad theologiam promovendam" yaani “Kukuza Taalimungu.” Lengo ni kutoa tafsiri ya kinabii mintarafu mwanga wa Ufunuo wa Kimungu, ili Taalimungu iweze kushughulikia mabadiliko makubwa ya kitamaduni kwa kufahamu kwamba, Zama za sasa zinapitia mabadiliko makubwa. Waraka huu kwa mfumo wa Barua Binafsi "Ad theologiam promovendam" yaani “Kukuza Taalimungu” unapitisha Katiba za Taasisi za Kipapa za Kitaalimungu, zilizoanzishwa kunako tarehe 23 Aprili 1718, ili kweli Taasisi hizi za Kitaalimungu ziweze kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa Kanisa na kwa Ulimwengu, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Katiba za Taasisi hizi zilifanyiwa mabadiliko makubwa kunako mwaka 1838 na baadaye tarehe 28 Januari 1999 na Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume “Inter munera Academiarum.” Mabadiliko ya sasa yanataka kuielekeza Taalimungu kujenga na kudumisha Kanisa la Kisinodi na Kimisionari na kamwe Kanisa haliwezi kuridhika na Taalimungu ya “Mezani.” Tafakari ya Kitaalimungu haina budi kuwaponya watu wa Mungu kwa mafuta ya faraja na kuwaganga kwa divai ya matumaini. Kumbe kuna haja ya kuwa na fikra mpya pamoja na mbinu mkakati. Haya yote yanaonesha uhitaji wa Mama Kanisa wa haraka ili kusonga mbele katika mageuzi thabiti ya kitamaduni kwa kuwa ni Taalimungu msingi inayomwilishwa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu.

Taalimungu ijenge na kudumisha Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Taalimungu ijenge na kudumisha Kanisa la Kisinodi na Kimisionari

Taalimungu inapaswa kusimikwa katika utamaduni wa majadiliano ya: kiekumene, kidini, kitamaduni na kimazingira ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kweli, huku yakionesha mwingiliano, tayari kutafsiri mawazo yanayoibuliwa, ili hatimaye kuwasilisha kweli za kiimani na Mafundisho ya Kristo Yesu. Kumbe, kuna haja kwa Taalimungu kujikita katika mchakato wa Kisinodi kwa kujenga na kuimarisha ushirika utakaokuza udugu wa kibinadamu, ushirika sanjari na kukoleza mchakato wa huduma ya uinjilishaji, ili iweze kugusa nyoyo za watu wengi zaidi. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza na kujadiliana; kutoa mang’amuzi na kuendelea kusoma alama za nyakati, ili hatimaye kuishi na kuendelea kujikita katika uzoefu wa urika na udugu wa kitaalimungu. Sayansi ya Kitaalimungu haina budi pia kuzingatia mwelekeo wake wa kihekima unaofumbatwa katika upendo wa kiakili kwa kutambua kwamba, “Ukweli na Upendo” ni sawa na chanda na pete pamoja na kuendelea kujielekeza zaidi katika hekima na hivyo kuonesha yenyewe kuwa maarifa ya kweli na ya uhakiki kama maarifa ya hekima na wala si yale ya kufikirika na ya kiitikadi; bali ya kiroho yaliyokuzwa kwenye magoti na matokeo yake ni: Ibada na Sala. Haya ni maarifa ya juu kabisa, lakini yanayofumbata sauti ya watu na hivyo kuifanya Taalimungu hii kuwa na umaarufu wa pekee kwani inashughulikia majeraha ya binadamu, yale ya kazi ya Uuumbaji na yale yanayofumbatwa katika historia ya mwanadamu ambayo inatabiri Injili ya matumaini na utimilifu wake nyakati za mwisho.

Taalimungu ijenge na kudumisha Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Taalimungu ijenge na kudumisha Kanisa la Kisinodi na Kimisionari

Yote haya ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kusoma alama za nyakati, tayari kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu “Dio-Agape” unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Kwa hiyo, kwanza kabisa, kipaumbele lazima kitolewe kwa ujuzi wa akili ya kawaida ya watu wa Mungu ambayo kwa kweli ni mahali pa kitaalimungu ambapo picha nyingi za Mwenyezi Mungu huishi, mara nyingi haziendani na uso wa Kikristo wa Mungu, pekee na daima upendo. Taalimungu inapaswa kujiweka yenyewe katika huduma ya uinjilishaji wa Kanisa na utangazaji wa imani, ili imani iweze kutamadunishwa kwa kujikita katika maadili ya hekima ya watu wa Mungu, pendekezo la uzuri wa kibinadamu kwa ajili ya binadamu wote. Taasisi za Kipapa za Kitaalimungu zinakabiliwa na utume huu na hivyo zinalazimika kuzingatia asili ya kisayansi ya tafakari ya kitaalimungu, majadiliano ya kisayansi na maarifa mengine ya kisayansi, kifalsafa, kiutu na kisanii ili kukuza majadiliano ya kiekumene kwa wale wanaoamini pamoja na majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali duniani. Mchakato huu unaweza kusaidia kuunda Jumuiya ya wasomi kwa ajili ya kushiriki imani na masomo, ambayo hutengeneza mtandao wa mahusiano na taasisi nyingine za mafunzo, elimu na kitamaduni na ambayo inatambua jinsi ya kupenya kwa uhalisi na roho ya mawazo katika maeneo yanayohitaji ufafanuzi wa maarifa, taaluma pamoja na Jumuiya za Kikristo. Ni katika muktadha wa sheria na kanuni mpya za Taasisi za Kipapa za Kitaalimungu zitaweza kutekeleza kwa urahisi zaidi malengo yake kwa wakati huu. Baba Mtakatifu anahitimisha Waraka wake wa Kitume uliowekwa kwenye mfumo wa Barua binafsi: “Motu proprio” wa "Ad theologiam promovendam" yaani “Kukuza Taalimungu” kwa kukazia ubora na kwamba, Sheria za Taasisi za Kipapa za Taalimungu, zimefafanuliwa kihalali na kusahihishwa tena na hivyo kupata nguvu za kibali cha Kitume.

Kukuza Taalimungu
02 November 2023, 15:24