Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na washiriki wa Mkutano mkuu wa 25 wa Shirika la Watawa wa Shule ya Notre Dame. Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na washiriki wa Mkutano mkuu wa 25 wa Shirika la Watawa wa Shule ya Notre Dame.  (Vatican Media)

Mkutano Mkuu wa Shirika la Watawa wa Shule ya Notre Dame: Ushuhuda, Unabii na Ushirika

Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na washiriki wa Mkutano mkuu wa 25 wa Shirika kwa kugusia ushuhuda wa maisha ya Mwenyeheri Mama Maria Theresa wa Yesu Gerhardinger, Kuishi katika ushuhuda wa kinabii wa ushirika na ulimwengu wote; Mashauri ya Kiinjili sanjari na Mshikamano wa Kiinjili. Shirika linaadhimisha mkutano huu kwa kumbukizi la miaka 190 tangu kuanzishwa kwake na tarehe 17 Novemba tangu Muasisi wao atangazwe Mwenyeheri

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi maalum cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari, majadiliano na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu: Karama, maisha na utume wa mashirika yao kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ujenzi wa: Kanisa la Kisinodi na Kimisionari sanjari na udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Papa Francisko akisalimiana na Masista
Papa Francisko akisalimiana na Masista

Shirika la Watawa wa Shule ya Notre Dame “School Sister of Notre Dame” tarehe 24 Oktoba 2023 lilifungua Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 25 wa Shirika unaonogeshwa na kauli mbiu “Kuishi katika ushuhuda wa kinabii wa ushirika na Ulimwengu wote.” Hii ilikuwa ni kumbukumbu ya miaka 190 tangu kuanzishwa kwa Shirika hili lenye watawa tabribani 1900 walioenea sehemu mbalimbali za dunia. Mkutano mkuu utafungwa rasmi tarehe 17 Novemba 2023, kumbukizi ya kutangazwa kuwa Mwenyeheri Mama Maria Theresa wa Yesu Gerhardinger. Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na washiriki wa Mkutano mkuu wa 25 wa Shirika kwa kugusia ushuhuda wa maisha ya Mwenyeheri Mama Maria Theresa wa Yesu Gerhardinger, Kuishi katika ushuhuda wa kinabii wa ushirika na ulimwengu wote; Mashauri ya Kiinjili sanjari na Mshikamano wa Kiinjili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyeheri Mama Maria Theresa wa Yesu Gerhardinger, alikuwa na nguvu ya mageuzi katika imani, ujasiri wa kuanzisha njia mpya; kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutoa elimu kwa vijana wa kizazi kipya kwa kukazia maendeleo ya mtu mzima, taaluma, malezi na  huruma, huku Kristo Yesu akiwa ni kiini cha malezi na makuzi yao. Kama Shirika limeendelea kufuata nyayo za Muasisi wa Shirika kwa kujikita katika mchakato elimu, huduma na taalimungu inayowazamisha katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ufukara sanjari na Ibada kwa Bikira Maria, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu kwa uwepo wa imani, matumaini na upendo.

Papa amekazia umuhimu wa unabii, ushuhuda na unabii
Papa amekazia umuhimu wa unabii, ushuhuda na unabii

Kuishi katika ushuhuda wa kinabii wa ushirika na ulimwengu wote ni jambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo,  kwa kujibidiisha katika mchakato wa ujenzi wa ushirika miongoni mwa watu watakatifu wa Mungu, ili watambue mateso na mahangaiko yao tayari kujibu kwa pamoja Agano la Upendo wa Mungu, ili hatimaye, kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa ambalo limejengwa juu ya Kristo Yesu jiwe kuu la msingi anayetamani kuona umoja wa wafuasi wake. Mwenyeheri Mama Maria Theresa wa Yesu Gerhardinger, ni mwanamke wa shoka aliyejitahidi kuyaishi kikamilifu mashauri ya Kiinjili kama mtindo wa maisha, kumbukumbu hai inayoonesha mahusiano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu. Maisha haya ni sadaka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, lakini pia ni kielelezo cha sadaka na majitoleo yao kwa Bwana, tayari kuwahudumia jirani zao. Baba Mtakatifu anawatia shime kujikita ujasiri wa ushujaa wa Injili ya mshikamano, kwa kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Shirika ni kipindi cha kujenga utamaduni wa kumsikiliza kwa dhati kabisa Roho Mtakatifu, kujenga na kudumisha umoja na ushirika; kufanya mang’amuzi ya pamoja ya jinsi ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili hususan kwenye utume wao kwenye sekta ta elimu na huduma kwa watu wa Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza Watawa wa Shule ya Notre Dame “School Sister of Notre Dame” na kwamba, anawaombea mapaji mengi ya Roho Mtakatifu ili maamuzi yatakayofikiwa yaweze kuzaa matunda mengi katika Jumuiya zao. Kwa ulinzi, tunza na maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa awe ni mlinzi wao wa daima.

Notre Dame SRS

 

 

13 November 2023, 14:45