Mawasiliano ya Jamii: Majiundo; Ulinzi Thabiti na Ushuhuda Makini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 23 Novemba 2023 amekutana na wajumbe wa Shirikisho la Majarida ya Kikatoliki, Umoja wa Wachapishaji wa Majarida Italia pamoja na Shirikisho la “Corallo na Aiart-Cittadini mediali.” Hawa ni wadau wa sekta ya mawasiliano wanaojikita zaidi katika kutayarisha vipindi kwenye TV, Radio pamoja na kutumia kikamilifu maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Dhamana yao kubwa ni kutaka kuwafunda wasikalizaji na watazamaji wao kielelezo cha ujirani mwema na Jumuiya inayowazunguka. Wamekuwa mstari wa mbele kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kujenga madaraja yanayowakutanisha watu; ili kukuza na kudumisha haki na ukweli; Utii wa sheria na uwajibikaji katika elimu. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia kuhusu umuhimu wa majiundo kwa vijana wa kizazi kipya, ulinzi thabiti katika matumizi ya mitandao ya kijamii hasa miongoni mwa watu dhaifu zaidi ndani ya jamii ili kukuza na kudumisha demokrasia ya mawasiliano na hatimaye ni ushuhuda. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia kuhusu umuhimu wa majiundo kwa vijana wa kizazi kipya yanayowawezesha kujenga uwezo wa kujadiliana katika ukweli na uwazi na wazee na kwamba, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kuna haja kwa vijana wa kizazi kipya “kuwa na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.” Lk 10:16.
Busara ni muhimu sana kama sifa msingi ya matumizi ya mitandao ya kijamii. Busara haina budi kumwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Majarida ya Kikatoliki yasaidie kuwafunda watu: kiroho na kimwili, kwa kuendelea kujikita katika ikolojia ya mawasiliano inayomwilishwa katika medani mbalimbali za maisha. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kujikita katika malezi na makuzi ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; ujenzi wa mahusiano na mafungamano bora ya kijamii kwani lengo kuu la mawasiliano ni kwa ajili ya kumfunda mwanadamu. Pili ni kuhusu ulinzi thabiti katika matumizi ya mitandao ya kijamii hasa miongoni mwa watu dhaifu zaidi ndani ya jamii ili kukuza na kudumisha demokrasia ya mawasiliano. Ni vyema kuibua na kudumisha sera na mbinu mkakati utakaowalinda watu dhaifu ndani ya jamii, watoto, wazee pamoja na walemavu dhidi ya vishawishi na kinzani za mitandao ya kijamii. Hii ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa demokrasia ya mawasiliano ya jamii. Huu ni ulinzi unaofumbatwa katika picha na katika maneno, daima utu, heshima na haki msingi za binadamu vikipewa msukumo wa pekee hususan katika ulimwengu wa kidigitali kwa ajili ya watoto wadogo na maskini kwani hawa wana upendeleo wa pekee mbele za Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko amemtumia Mwenyeheri Carlo Acutis kama shuhuda aliyebahatika kufahamu mengi kuhusu mawasiliano ya kijamii, matangazo ya biashara pamoja na mitandao ya kijamii ambayo inatumiwa vibaya. Lakini Mwenyeheri Carlo Acutis alifahamu fika matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii na wala hakutumbukia katika mtego wa matumizi ya ovyo! Alitumia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu bila kusahau tunu msingi za maisha. Ushuhuda wake umekuwa ni wa kinabii, uliosimikwa katika kipaji cha ubunifu unaomweka huru na hatimaye kumsukuma mtu kujisadaka bila ya kujibakiza tayari kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Huu ni mwaliko wa kujikita katika uaminifu kwa Injili hata kuthubutu kwenda kinyume cha mawimbi ya bahari, tayari kujikita katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu dhidi ya utandawazi unaosimikwa katika uchoyo na ubinafsi; kuwa ni wajenzi wa amani katika ulimwengu uliosheheni chuki, vita na mipasuko mbalimbali sanjari na kuendelea kutoa kipaumbele kwa maskini na wale wote wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia. Kwa hakika ushuhuda unapaswa kumwilishwa katika matendo. Kumbe, huu ni mwaliko wa kuendelea kujikita katika malezi na majiundo; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu na hatimaye, ushuhuda unaomwilishwa katika hali halli ya maisha ya mwanadamu.