Tafuta

Dominika tarehe 3 Desemba 2023 Mama Kanisa anaanza Kipindi cha Majilio, kama Maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Dominika tarehe 3 Desemba 2023 Mama Kanisa anaanza Kipindi cha Majilio, kama Maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu.  

Kipindi cha Majilio Ni Maandalizi ya Sherehe ya Noeli, Kuzaliwa Kwa Kristo Yesu!

Dominika tarehe 3 Desemba 2023 Mama Kanisa anaanza Kipindi cha Majilio, kama Maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Mwaliko wa Baba Mtakatifu kwa waamini ni kujiimarisha zaidi katika maisha ya kiroho tayari kumfungulia Kristo Yesu malango ya nyoyo zao ili aweze kuingia na kuwakirimia mwanga wake angavu na uwepo wake unaoganga na kuponya udhaifu na mapungufu ya kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 29 Novemba 2023 amewakumbusha waamini kwamba, Dominika tarehe 3 Desemba 2023 Mama Kanisa anaanza Kipindi cha Majilio, kama Maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Mwaliko wa Baba Mtakatifu kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ni kujiimarisha zaidi katika maisha ya kiroho tayari kumfungulia Kristo Yesu malango ya nyoyo zao ili aweze kuingia na kuwakirimia mwanga wake angavu na uwepo wake unaoganga na kuponya udhaifu na mapungufu ya kibinadamu. Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mfalme wa amani. Hakuna sababu ya kukata wala kukatishwa tamaa na vita, kinzani na mipasuko mbalimbali ya kijamii inayoendelea kujionesha sehemu mbalimbali za dunia, bali kutua nanga ya matumaini yao kwa Kristo Yesu ambaye amewahakikishia waja wake kwamba, atakuwa pamoja nao hadi mwisho wa nyakati. Rej. Mt 28: 20. Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma na mapendo kwa kuwawezesha watu wenye shida na mahangaiko mbalimbali kumwona Kristo Mfufuka kwa njia yao. Mama Kanisa huchukulia wajibu wake kuadhimisha kwa kumbukumbu takatifu ya ukombozi ya Bwana arusi wake aliye Mungu katika siku zilizopangwa katika mwenendo wa mwaka mzima, anapolikunjua Fumbo la Kristo Yesu, tangu Fumbo la Umwilisho na Pasaka hadi kungojea kwa tumaini lenye heri kurudi kwake Bwana Yesu, kuwahukumu wazima na wafu. Waamini wawasaidie jirani zao kutunza ndani mwao kiu ya kutaka kukutana na Mwenyekezi Mungu anayeongoza mapito na hatimaye kuwasindikiza waamini hatua kwa hatua katika njia ya uzima milele.

Majilio ni Kipindi cha Kujiimarisha kiroho.
Majilio ni Kipindi cha Kujiimarisha kiroho.

Na kwa njia hii, Mama Kanisa huwafungulia waamini utajiri wa uweza na mastahili ya Bwana wake na hivyo waamini huweza kuchota na kujazwa na neema ya wokovu. Mama Kanisa katika huruma na upendo wake wa daima anapenda kuwakomaza waamini kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; Mafundisho, Sala pamoja na matendo ya toba na huruma. Rej. Sacrosanctum concilium, 102-111. Kipindi cha Majilio: “Kwa kuadhimisha kila mwaka liturujia ya majilio, Kanisa linahuisha kule kumngojea Masiha, likijiweka katika ushirika wa maandalizi marefu ya ujio wa kwanza wa mwokozi, waamini wakipyaisha tamaa ya ujio wake wa pili.” (KKK 524). Majilio ni kipindi cha upendo, matumaini, furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Waamini wawe ni mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu
Waamini wawe ni mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu

Mishumaa minne inawakilisha Majuma manne ya Kipindi cha Majilio. Kwa kadiri ya Mapokeo ni kwamba kila juma linawakilisha miaka elfu moja, kumbe majuma manne ni sawa na miaka 4,000 kutoka kwa wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva hadi Kuzaliwa kwa Mwokozi. Mishumaa mitatu ni ya rangi ya zambarau na moja ni wa rangi ya waridi. Mishumaa ya zambarau hutukumbusha kuwa kipindi cha majilio ni kipindi cha sala, toba, na matendo ya huruma: kiroho na kimwili ili kujitayarisha vema kumpokea Mkombozi wetu katika hali zote mbili, ujio wa kwanza na wa pili. Mshumaa wa rangi ya waridi huwashwa Dominika ya tatu, Dominika ya furaha “Gaudete” kwa sababu waamini wamefika katikati ya Kipindi cha Majilio, utimilifu wa ahadi ya kuzaliwa Mwokozi ukaribu zaidi. Mwanga wa mishumaa unaashiria matarajio na tumaini linalozunguka ujio wa kwanza wa Bwana wetu ulimwenguni na matarajio ya ujio wake wa pili kuwahukumu wazima na wafu. Kila wakati Mama Kanisa anapouanza Mwaka wa Liturujia ni lazima watoto wake kusahihisa kasoro za mwaka uliopita na kuanza upya, kwa kuiga mfano mzuri wa maisha ya wahusika wakuu katika Kipindi hiki cha Majilio ambao ni: Nabii Isaya, Yohane Mbatizaji, Zakaria na mkewe Elizabeti Wengine wanaopamba kipindi hiki ni: Wachungaji wa kondeni, Mamajusi, watu wa kawaida lakini kwa namna ya pekee, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu wawe ni mifano bora ya kuigwa katika kipindi hiki cha Majilio! Hawa ni watu walioguswa kwa namna ya pekee na maandalizi ya ujio wa Masiha. Bwana wetu Yesu Kristo ndiye nguzo kuu ya tafakari katika kipindi hiki.

Papa Majilio
29 Novemba 2023, 15:17