Tafuta

Jumamosi tarehe 25 Novemba 2023 Ukraine imefanya kumbukizi ya miaka 90 tangu kulipotokea mauaji ya kimbari ya “Holodomor,” Jumamosi tarehe 25 Novemba 2023 Ukraine imefanya kumbukizi ya miaka 90 tangu kulipotokea mauaji ya kimbari ya “Holodomor,”   (AFP or licensors)

Kumbukizi ya Miaka 90 ya Mauaji ya Kimbari ya Holodomor Ukraine

Papa amekumbuka mauaji ya “Holodomor” kwa kusema kwamba, donda ndugu la mauaji ya kimbari ya “Holodomor” badala ya kupona linaendelea kusababisha machungu na ukatili mkubwa kutokana na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine. Mwaliko kwa waamini kuendelea kusali bila kuchoka kwa sababu sala ni nguvu ya amani ambayo huvunjilia mbali: chuki, tabia na mzunguko wa kulipizana kisasi na hivyo kufungua njia zisizotarajiwa za upatanisho. Amani na Haki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mauaji ya kimbari yanatambulikana na Umoja wa Mataifa kuwa ni uhalifu wa Kimataifa. Jumamosi tarehe 25 Novemba 2023 Ukraine imefanya kumbukizi ya miaka 90 tangu kulipotokea mauaji ya kimbari ya “Holodomor,” yani kuanzia mwaka 1932 hadi mwaka 1933. Inasadikiwa kwamba, watu kati ya milioni tatu hadi tano walipoteza maisha kutokana na baa la njaa, lengo kubwa la Stallin lilikuwa ni kuwatisha wananchi wa Ukraine wasisimame kidete kudai uhuru wao kutoka kwa Umoja wa Soviet sanjari na kufyekelea mbali idadi ya wasomi waliokuwa mstari wa mbele kudai uhuru wao.

Kumbukizi ya Miaka 90 ya Mauaji ya Kimbari ya Holodomor
Kumbukizi ya Miaka 90 ya Mauaji ya Kimbari ya Holodomor

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 26 Novemba 2023 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana amekumbuka mauaji ya kimbari ya “Holodomor” kwa kusema kwamba, donda ndugu la mauaji ya kimbari ya “Holodomor” badala ya kupona linaendelea kusababisha machungu na ukatili mkubwa kutokana na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali bila kuchoka kwa sababu sala ni nguvu ya amani ambayo huvunjilia mbali: chuki, tabia na mzunguko wa kulipizana kisasi na hivyo kufungua njia zisizotarajiwa za upatanisho.

Majadiliano katika ukweli na uwazi ni chanzo cha amani ya kudumu.
Majadiliano katika ukweli na uwazi ni chanzo cha amani ya kudumu.

 Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kumshukuru Mungu kwa sababu hatimaye kuna suluhu kati ya Israeli na Palestina na baadhi ya mateka wameanza kuachiliwa. Baba Mtakatifu amezisihi pande zote mbili kufanya kwa haraka iwezekanavyo kuwaachilia mateka wa vita kwa kufikiria zaidi familia zao. Iwe ni fursa ya kuruhusu misaada zaidi ya kiutu iweze kuingia Ukanda wa Gaza na kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi ndiyo njia pekee ya kujenga na kudumisha amani. Kwa watu ambao hawataki mazungumzo kwa hakika hawataki amani.

Mauaji ya Kimbari
27 November 2023, 14:39