Tafuta

Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 16 Novemba 2023 linaendesha Kongamano la Kimataifa, linalonogeshwa na kauli mbiu “Kipimo cha Utakatifu wa Kijumuiya.” Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 16 Novemba 2023 linaendesha Kongamano la Kimataifa, linalonogeshwa na kauli mbiu “Kipimo cha Utakatifu wa Kijumuiya.”  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kongamano Kuhusu Kipimo cha Utakatifu wa Kijumuiya! Ushuhuda wa Imani Tendaji

Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 16 Novemba 2023 linaendesha Kongamano: Kauli mbiu “Kipimo cha Utakatifu wa Kijumuiya.” Kardinali Marcello Semeraro, anazungumzia kipimo cha utakatifu wa Kijumuiya, umuhimu wa waamini walei kutangaza na kushuhudia utakatifu wa maisha ya kijumuiya; kuna uwezekano mkubwa kwa wanasiasa kuwa ni watakatifu na kila fursa inaweza kutumika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, utakatifu ni wito kwa watu wote wa Mungu, ili waweze kuwa wakamilifu kama Baba yao wa Mbinguni alivyo mkamilifu. Ili kufikia azma hii, wanapaswa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao Matunda ya Roho Mtakatifu sanjari na kuomba neema ya kusamehe na kusahau. Huu ni mchakato wa utakatifu unaosimikwa katika maisha ya kila mmoja, kwa kutumia vyema na kwa uaminifu karama na vipawa katika utekelezaji wa majukumu na hivyo kusonga mbele bila kusitasita katika safari ya imani iliyo hai, iamshayo matumaini na kutenda kwa mapendo. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa ni mfano na kielelezo cha utakatifu wote. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” anasema, utakatifu ni mwaliko kwa waamini wote na wala si kwa watu wachache tu ndani ya Kanisa! Huu ni mwaliko wa kuongeza jitihada za kukutana na Kristo Yesu katika maisha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata: huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Watakatifu ni watu wa kawaida kabisa, ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu, leo hii wamekuwa ni marafiki zake wa karibu! Watakatifu ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wamejichukulia dhamana ya kuanza safari ya utakatifu wa maisha!

Ubatizo ni mwanzo wa safari ya utakatifu wa maisha
Ubatizo ni mwanzo wa safari ya utakatifu wa maisha

Watakatifu walikuwa na mapungufu na dhambi zao binafsi, lakini wakathubutu kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Utakatifu ni hija ya maisha mbele ya Mwenyezi Mungu inayofumbatwa katika ujasiri, matumaini na uthubutu kwa kuamini kwamba, neema ya Mungu inaweza kuwaongoza kufikia hatima yake, yaani kuonana na Mwenyezi Mungu uso kwa uso! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujizatiti katika utakatifu wa maisha, hata wanapokuwa wagonjwa kitandani hawawezi kitu! Wanapokuwa kazini wakichakarika kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa uaminifu, uadilifu huku wakiwajibika barabara kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Watakatifu ni mashuhuda na wandani wa matumaini na unyenyekevu wa moyo! Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 16 Novemba 2023 linaendesha Kongamano la Kimataifa, linalonogeshwa na kauli mbiu “Kipimo cha Utakatifu wa Kijumuiya.” Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Wenyeheri na Watakatifu anazungumzia kipimo cha utakatifu wa Kijumuiya, umuhimu wa waamini walei kutangaza na kushuhudia utakatifu wa maisha ya kijumuiya; kuna uwezekano mkubwa kwa wanasiasa kuwa ni watakatifu na kwamba, kila nafasi ikitumiwa vyema ni fursa ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Utakatifu unamwilishwa katika medani mbalimbali za maisha
Utakatifu unamwilishwa katika medani mbalimbali za maisha

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, utakatifu ni hija inayofumbatwa pia katika maisha ya kijumuiya na Mama Kanisa anayo mifano kede kede ya Jumuiya za watakatifu. Baba Mtakatifu anaendelea kusema, utakatifu unafumbatwa katika maisha ya sala kama sehemu ya mchakato wa kutaka kujenga uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu, kumbe, sala endelevu ni chachu ya utakatifu wa maisha! Ukimya na tafakuri ni nyenzo zinazojenga uhusiano mwema na Kristo! Lakini, sala ya kweli inamwilishwa katika uhalisia wa maisha yanayofumbatwa katika upendo. Waamini wajenge utamaduni na sanaa ya kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika medani mbali mbali za maisha kwani hiki ni kiini na utambulisho wa Kanisa. Waamini wajitahidi kukutana na Kristo Yesu katika Neno na Sakramenti za Kanisa zinazomwilishwa katika uhalisia wa maisha ili waweze kuwa ni chachu ya utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo, changamoto ni utakatifu wa watu wa Mungu katika ujumla wao, ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu. Dhamana na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa kwa namna ya pekee, ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican unaobainisha: wito, utume na dhamana ya waamini walei katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Kongamano Kuhusu Kipimo cha Utakatifu wa Kijumuiya
Kongamano Kuhusu Kipimo cha Utakatifu wa Kijumuiya

Kimsingi waamini walei wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo mintarafu uhalisia wa maisha yao. Waamini walei daima wajibidishe kuchota utajiri na amana ya maisha yao ya Kikristo kutoka katika: Neno la Mungu, Sala, Sakramenti za Kanisa pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa, dira na mwongozo wa jinsi ya kuyatakatifuza malimwengu. Waswahili wanasema, “kitu kizuri na chema, kula na ndugu yako”. Waamini walei watambue kwamba, amana na utajiri huu wanapaswa kuwashirikisha pia jirani zao kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; katika kuyatakatifuza maeneo ya kazi pamoja na utume wa familia. Waamini walei wakiwa wamepyaishwa kutoka katika undani wa maisha yao, wanaweza sasa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu; watu wenye wenye uwezo wa kusikiliza kwa makini na kujibu kilio cha maskini wanaowazunguka; watu wanaoweza kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi; ukarimu na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Waamini walei wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu
Waamini walei wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu

Wanasiasa wanahimizwa kujenga na kudumisha umoja na urafiki na Kristo Yesu pamoja na kutambua nguvu na udhaifu wao kama binadamu. Mchakato wa kuingia katika masuala ya kisiasa unapania pamoja na mambo mengine kujenga urafiki wa kijamii, ili kuleta mageuzi yanayokusudiwa kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Mtakatifu Oscar Arnulfo Romero katika maisha na utume wake, alipenda kuwahimiza waamini walei kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji wa kina katika mazingira yao, kama kielelezo cha imani tendaji. Siasa ni wito na si kila mwamini ana wito wa kuwa ni mwana siasa! Ikumbukwe kwamba, siasa si njia pekee inayoweza kuwahakikishia watu haki, amani, ustawi na maendeleo fungamani, kumbe, medani mbali mbali za maisha, ziwe ni mahali ambapo patawasaidia waamini kuweza kuyatakatifuza malimwengu, kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha haki, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Waamini wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani ni katika muktadha huu, hata wanasiasa wanaweza kuwa ni watakatifu. Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Wenyeheri na Watakatifu anasema, utakatifu unaweza kushuhudiwa katika kila medani ya maisha ya mwanadamu.

Kongamano Utakatifu
14 November 2023, 15:25