Sherehe ya Watakatifu Wote, Tarehe Mosi, Novemba: Ushuhuda wa Utakatifu wa Maisha
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Utakatifu wa maisha ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo, kwani utakatifu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko ni chemchemi ya furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Utakatifu ni hija ya mapambano dhidi ya dhambi kwa kuendelea kupyaisha ile neema ya utakaso ambayo waamini wameipokea katika Sakramenti ya Ubatizo! Utakatifu unawawezesha waamini kuguswa na mahangaiko ya jirani zao, kwa kutambua na kuthamini utu na heshima yao kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waamini wanaitwa kuwa watakatifu kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Mtakatifu na ni kiini na utimilifu wa utakatifu wenyewe. Utakatifu ni changamoto inayopaswa kupaliliwa kila kukicha na kamwe haitoshi kuwa Mkristo na mwamini kuanza kubweteka, bali daima ajitahidi kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Mama Kanisa kila mwaka tarehe Mosi, Novemba, anaadhimisha Sherehe ya Watakatifu wote: “Sollemnitas Omnium Sanctorum” iliyoanzishwa na Papa Gregori IV (827-844). Katika Sherehe hii, Mama Kanisa anataka kumsifu na kumtukuza Mungu kwa njia ya watakatifu wake ambao wametambuliwa rasmi na Mama Kanisa: “Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao.” Ufu 7:9. Pamoja nao ni kundi lote la wabatizwa si kadiri ya matendo yao bali ni kadiri ya neema, kuhesabiwa haki na imani inayowafanya kuwa watakatifu na hivyo wanaonywa kuishi iwastahilivyo watakatifu. LG 40.
Sherehe ya watakatifu wote ni utambuzi wa utakatifu wa Kanisa unaosimikwa katika upendo, kwa kutimiza mashauri ya Kiinjili na ushuhuda bora wa utakatifu wa maisha. Rej. LG 39. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanapozungumzia kuhusu Fumbo la Kanisa wanakazia umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa. Wanasema waamini kwa kuimarika na misaada mingi ya wokovu namna hii na ya ajabu, waamini wote wa kila hali na hadhi wanaitwa na Kristo Yesu kila mmoja kwa njia yake, kwenye ukamilifu wa utakatifu kama Mwenyezi Mungu alivyo Mtakatifu! Baba Mtakatifu Francisko anakazia pamoja na mambo mengine, mapambano ya maisha ya kiroho, kukesha na kusali pamoja na kufanya mang’amuzi ya maisha. Lakini neema ya Mungu inaweza kuleta mabadiliko ya kweli kwani watakatifu ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu! Ni watu waliopambana na ubinafsi pamoja na mapungufu yao ya kibinadamu, leo hii ni marafiki wapendwa wa Mungu, wandani katika hija ya imani, matumaini na mapendo. Kanisa ni Sakramenti ya wokovu inayowajalia waamini kusikiliza Neno la Mungu, kushiriki Sakramenti za Kanisa; kusimika maisha yao katika kanuni maadili na utu wema pamoja na kuonja shuhuda za watakatifu mbalimbali.
Changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo ni utakatifu wa Jumuiya ya waamini, dhamana na utume ambao unapaswa kutekelezwa kwa ari na moyo mkuu: kwa kukubali mahusiano na mafungamano mapya yanayoletwa na Kristo Yesu; kwa kuondokana na woga usiokuwa na mvuto wala mashiko; kwa kujenga utamaduni wa kukutana na kushirikiana na wengine; kwa kumwilisha imani katika matendo; vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Waamini wajitahidi kuwa wamisionari katika hali na mazingira yao! Waamini wajifunze kuteseka na kufurahi pamoja na jirani zao ili kujenga umoja, udugu na mshikamano wa dhati! Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu kwa kuishi kiaminifu kweli za Kiinjili! Mambo yote haya ni kielelezo cha mapambano ya maisha ya kiroho, yanayohitaji kufanyiwa mang’amuzi ya kina, ili kusonga mbele katika hija ya utakatifu wa maisha! Ni mwaliko wa kukumbatia neema ya Mungu, ili aweze kuwakoa waja wake kutoka katika vishawishi na mitego ya shetani, Ibilisi. Waamini wawe wepesi kusoma alama za nyakati, kuchunguza dhamiri zao mbele ya Mwenyezi Mungu na kukimbilia huruma na upendo wake, pale wanapoelemewa na dhambi pamoja na udhaifu wa moyo!
Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anasema, Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Anataka waja wake kuwa kweli ni wakamilifu na watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha katika sehemu mbali mbali za Maandiko Matakatifu. Wosia huu wa kitume umegawanyika katika sura kuu tano: Sura ya kwanza ni Wito wa utakatifu; Sura ya Pili ni Adui wa utakatifu; Sura ya tatu: Mwanga katika maisha ya Mwalimu, Sura ya nne: Alama za Utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo na Sura ya tano: Mapambano ya maisha ya kiroho; kukesha na kufanya mang’amuzi! Baba Mtakatifu Francisko katika sura ya pili anagusia: Maadui wa imani: Mitindo potofu ya utakatifu wa maisha unaoelea katika ombwe; akili bila ya kumtegemea Mungu wala kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Hawa ndio wale watu wanaomtafuta Mungu bila ya Kristo Yesu; wanaomtaka Kristo Yesu bila Kanisa, au kulipenda Kanisa bila watoto wake! Haya ni mawazo yanayoendelea kusumbua vichwa vya watu wa nyakati hizi. Ni watu wanaotaka mafundisho ambayo kamwe hayana Fumbo ndani mwake, kwani wanayo majibu ya maswali yote yanayomtatiza mwanadamu! Hawa ni watu wanaodhani kwamba, wanaweza kumweka Mwenyezi Mungu “mfukoni mwao” na kumtumia kama wanavyotaka! Waamini wanapaswa kutambua kwamba, uwezo wa mwanadamu kufikiri una ukomo wake! Hawawezi kuhalalisha kweli za Kiinjili ili kukidhi matakwa yao binafsi na kwamba, Mafundisho tanzu ya Kanisa yanaendelea kufafanuliwa daima katika maisha na kwamba, taalimungu na utakatifu wa maisha ni mambo yasiyopingana wala kusigana!
Hekima na busara ya Kikristo inafumbatwa pia katika huruma na upendo kwa jirani! Waamini waendelee kupambana na maadui wa utakatifu wa maisha kwa kwa kujikita katika Ibada ya kweli inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Baba Mtakatifu anasema, hata leo hii bado kuna wazushi na wakanimungu kwani wanadhani kwamba, kila jambo linategemea utashi wa binadamu na kusahau huruma na upendo wa Mungu, ambaye aliwapenda binadamu kwanza! Hawa ni watu wanaoshindwa kutambua karama, mchango na nafasi ya kila mwamini katika maisha na utume wa Kanisa. Hakuna mtu aliyebarikiwa kufanya yote kwa ukamilifu, bali watu wanategemeana na kukamilishana katika unyenyekevu! Watu wakiri na kutambua: karama, uwezo na mapungufu yao katika maisha kwani neema inajikita katika asili ya binadamu! Mama Kanisa anaendelea kufundisha kwamba, watu wanahesabiwa haki si kwa matendo yao bali kwa njia ya neema inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu! Lakini ikiwa ni kwa neema, haiwi kwa matendo tena, au hapo neema isingekuwa neema. (Rej. Rum. 11:6). Wito huu wa uzima wa milele ni wa Kimungu. Wote kabisa twategemea kazi ya Mungu, kwani Yeye peke yake anajifunua na anajitoa mwenyewe; Wapita maweza ya akili na nguvu za utashi wa kibinadamu! (Rej. KKK. Namba 1999). Watakatifu walijitahidi kutenda haki mbele ya Mungu na jirani zao, wakamwilisha upendo huo katika uhalisia na vipaumbele vya maisha yao! Wazushi mamboleo na wakanimungu wanaendelea kujionesha kwa kujikita katika Sheria kanuni za Kanisa, Liturujia na Mafundisho Tanzu ya Kanisa, kwa ajili ya kutaka kujikweza, “kujimwambafai” pamoja na kujitafutia umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko! Badala ya kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu katika unyenyekevu na upendo, ili hatimaye, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uzuri na furaha ya Injili, ili kuzima kiu na matamanio halali ya watu wa Mataifa! Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna itifaki ya karama na tunu msingi zinazowaunganisha waamini ili kuambata mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa. Tunu hizi ni: imani na upendo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuzitafakari tunu hizi na kufanya mang’amuzi mbele ya Mwenyezi Mungu.