Papa Francisko:Mkristo ni yule aliye na upendo huru unaojua kujitoa kwa ajili ya Mungu
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwa waamini karibu 2000 waliunganika katika Uwanja wa Nyika wa Ulaanbataar nchini Mongolia Dominika tarehe 3 Septemba 2023 katika Ziara yake ya 43 ya Kitume nchini Mongolia, kwa kuongozwa na Neno la Mungu la masomo ya siku amesema kuwa: “Kwa maneno ya Zaburi ya Kiitikio, tuliomba: “Ee Mungu... nafsi yangu inakuonea kiu; mwili wangu unazimia kwa ajili yako, kama katika nchi kavu na iliyochoka, isiyo na maji” (Zab 63:2). Ombi hili zuri sana linaambatana na safari yetu katika maisha, katikati ya majangwa yote tunayoitwa kuyavuka. Ni katika majangwa hayo ndiyo tunasikia habari njema kwamba hatuko peke yetu katika safari yetu; nyakati hizo za ukavu haziwezi kuyafanya maisha yetu kuwa tasa milele; na wala kilio chetu cha kiu kutosikika. Mungu Baba amemtuma Mwanawe ili kutupatia maji ya uzima ya Roho Mtakatifu ili kuridhisha nafsi zetu (rej. Yn 4:10). Yesu, kama tulivyosikia katika Injili, anatuonesha njia ya kukata kiu yetu. Ni njia ya upendo, ambayo aliifuata hata msalabani, na ambayo anatuita tumfuate, tukipoteza maisha ili tuyapate (rej. Mt 16:24-25).
Kwa njia huyo Papa amependa tutafakari pamoja mambo haya mawili: kuhusu kiu iliyo ndani yetu, na upendo unaozima kiu hiyo. Kwanza kabisa tunaitwa kukiri kiu iliyo ndani yetu. Mtunga Zaburi anamlilia Mungu katika ukame wake, kwa maana maisha yake yamekuwa kama jangwa. Maneno yake yana sauti fulani katika nchi kama Mongolia: kubwa, tajiri katika historia na utamaduni, lakini pia alama ya ukame wa nyika na jangwa. Papa ameongezea “Wengi wenu mnajua kuridhika na uchovu wa safari, ambayo inaibua kipengele cha msingi cha hali ya kiroho ya kibiblia inayowakilishwa na Ibrahimu na, kwa maana pana, na watu wa Israeli na kiukweli kila mfuasi wa Bwana.” Kwa sisi sote ni ‘wahamiaji wa Mungu’, yaani mahujaji wanaotafuta furaha, wasafiri wenye kiu ya upendo. Jangwa ambalo Mtunga Zaburi anazungumzia, basi, ni maisha yetu. Kwa njia hiyo “Sisi ni ile nchi kavu yenye kiu ya maji safi, maji ambayo yanaweza kukata kiu yetu kuu.
Mioyo yetu inatamani kugundua siri ya furaha ya kweli, furaha ambayo hata katikati ya ukame wa kuwepo, inaweza kutusindikiza na kututegemeza. Ndani yetu, tuna kiu isiyotosheka ya furaha; tunatafuta maana na mwelekeo katika maisha yetu, sababu ya yote tunayofanya kila siku. Zaidi ya yote, tuna kiu ya upendo, kwa kuwa upendo pekee ndio unaoweza kututosheleza, kutuletea utimilifu, kutia moyo uhakikisho wa ndani na kuturuhusu kufurahia uzuri wa maisha.” Baba Mtakatifu Francisko amekazia kusema kwamba “imani ya Kikristo ni jibu la kiu hii; inachukuliwa kwa uzito, bila kutupiliwa mbali au kujaribu kuibadilisha na dawa za kutuliza au mbadala. Kwa maana katika kiu hiyo liko fumbo kuu la ubinadamu wetu: inafungulia mioyo yetu kwa Mungu aliye hai, Mungu wa upendo, ambaye anakuja kukutana nasi na kutufanya kuwa watoto wake, kaka na dada mmoja kwa mwingine. “
Papa amesema “Hili linatuleta kwenye jambo la pili ambalo ni upendo unaokata kiu yetu. Huu ndio moyo wa imani ya Kikristo kwani Mungu, ambaye ni Upendo, anakukaribia katika Mwanawe Yesu, na anataka kushiriki katika maisha yako, kazi yako, ndoto zako na kiu yako ya furaha. Ni kweli kwamba, nyakati fulani, tunajisikia kama “nchi kavu na yenye uchovu, isiyo na maji”, lakini ni kweli vile vile kwamba Mungu anatujali na anatupatia maji safi, yenye kuburudisha, maji ya uzima ya Roho, yenye kububujika ndani yetu ili kutufanya upya na kutuweka huru kutokana na hatari ya ukame. Yesu anatupatia maji hayo. Kama Mtakatifu Agostino anavyotuambia, “…ikiwa tunajitambua wenyewe katika wale walio na kiu, tunaweza pia kujitambua wenyewe katika wale wanaokata kiu hiyo” (taz. Zaburi, 63:1).
Hakika, ikiwa katika maisha haya mara nyingi tunapitia jangwa na upweke, uchovu na utupu, tunapaswa kukumbuka, pamoja na Agostino kwamba, “ili tusije tukazimia katika jangwa hili, Mungu hutuburudisha kwa umande wa neno lake ... hutufanya tuhisi kiu, lakini huja kukidhi kiu hiyo… Mungu ameturehemu; ametufungulia njia kuu jangwani: Bwana wetu Yesu Kristo ametupatia chanzo cha faraja katika jangwa hilo: wahubiri wa neno lake. Ametupatia maji katika jangwa hilo, kwa kuwajaza wahubiri hao na Roho Mtakatifu, ili kuumba, ndani yao, chemchemi ya maji yakibubujikia uzima wa milele” (Zab 61. 1, 6).
Maneno haya, Papapa amekazia kuwa “yanazungumza nanyi juu ya historia yenu wenyewe. Katikati ya majangwa ya maisha na matatizo yanayohusiana na kuwa jumuiya ndogo, Bwana amehakikisha kwamba hamkosi maji ya neno lake, shukrani hasa kwa wahubiri na wamisionari ambao, kwa kutiwa mafuta na Roho Mtakatifu, walipanda mbegu kati yenu ya uzuri wake. Neno hilo daima hurudisha kwenye moyo wa imani yetu ili kujiruhusu wenyewe kupendwa na Mungu na kufanya maisha yetu kuwa sadaka ya upendo. Kwa maana upendo pekee hukata kiu yetu kweli.”Papa amesisisitiza. Hivyo ndivyo Yesu anamwambia mtume Petro katika Injili iliyosomwa. Petro hawezi kukubali ukweli kwamba Yesu lazima ateseke, ashtakiwe na viongozi wa watu, apate mateso yake na kisha afe msalabani. Petro anajibu, anapinga, anajaribu kumshawishi Yesu kwamba amekosea, kwa sababu, katika mawazo ya Petro kama ilivyo hata sisi mara nyingi tuna wazo sawa kuwa Masiha hawezi kuishia kwa kushindwa, kufa msalabani kama mhalifu aliyeachwa na Mungu.
Lakini Bwana alimkemea Petro kwa sababu anafikiri “kama ulimwengu unavyofikiri”, na si kama Mungu anavyofikiri (taz. Mt 16:21-23). Ikiwa tunafikiri kwamba mafanikio, mamlaka, au vitu vya kimwili vinatosha kutosheleza kiu katika maisha yetu, basi tunafikiri kama ulimwengu unavyofikiri. Ulimwengu wa namna hiyo hauelekezi popote; hakika, unatuacha na kiu zaidi kuliko hapo awali. Badala yake Yesu anatuonesha njia: “Ikiwa yeyote anataka kuwa mfuasi wangu, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa maana wale wanaotaka kuokoa maisha yao wataipoteza, na wale wanaopoteza maisha yao kwa ajili yangu watayapata” (Mt 16:24-25). Papa Francisko ameongeza kusema hiyo, hakika ndiyo njia bora zaidi: kukumbatia msalaba wa Kristo. Katika moyo wa Ukristo kuna ujumbe wa ajabu na wa kushangaza. Ukipoteza maisha yako, ukiitoa sadaka ya ukarimu, ukiihatarisha kwa kuchagua kupenda, ukiyafanya kuwa zawadi ya bure kwa wengine, yatarudi kwako kwa wingi, na utakuwa na furaha isiyo na mwisho, amani ya moyo,na nguvu za ndani na usaidizi. Huu ndio ukweli ambao Yesu anataka tuuvumbue, ukweli anaotaka kuwafunulia watu waliokuwapo hapo na kwa nchi hii ya Mongolia, alisisitiza Papa.
“Huhitaji kuwa maarufu, tajiri au hodari ili kuwa na furaha. Upendo pekee ndio unaokidhi kiu ya mioyo yetu, upendo pekee ndio unaoponya majeraha yetu, upendo pekee ndio hutuletea furaha ya kweli. Hii ndiyo njia ambayo Yesu alitufundisha; hii ndiyo njia aliyofungua mbele yetu. Na sisi pia tusikilize kile ambacho Bwana alimwambia Petro kwa kujibu: “Nenda nyuma yangu” (Mt 16:23). Kwa maneno mengine, uwe mfuasi wangu, tembea katika nyayo zangu na acha kufikiria kama ulimwengu unavyofikiri. Tukifanya hivyo, tutaweza, kwa neema ya Kristo na Roho Mtakatifu, kusafiri katika njia ya upendo.” Hata wakati upendo unahitaji kujikana wenyewe, kupambana na aina zetu za kibinafsi na za kidunia za ubinafsi, na kuchukua hatari ya kuishi maisha ya udugu wa kweli. Kwa maana ingawa ni kweli kwamba mambo haya yote yanahusisha juhudi na sadaka, na wakati mwingine kuchukua msalaba, ni kweli zaidi kwamba, tunapopoteza maisha yetu kwa ajili ya Injili, Bwana huturudishia kwa wingi, utimilifu wa upendo na furaha kwa milele yote. Amehitimisha mahubiri.