Papa aonesha uchungu kufuatia na tetemeko kubwa la ardhi nchini Morocco
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 9 Septemba 2023 ameeleza uchungu wake kwa mamia ya waathrika wa tetemeko la ardhi lenye nguvu sana ambalo liligonga vibaya eneo la Marrakech nchini Morocco. Katika tetemeko hilo watu karibu 820 wamekufa hadi sasa na zaidi ya 600 kujeruhiwa kadiri ya masaa yanasonga mbele. Katika telegramu iliyotiwa saini na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, Papa anasema amehuzunishwa na janga hilo la asili na amehakikishia ushirika wake wa sala na mshikamano wa kina kwa wale wanaoguswa katika mwili na kiroho kutokana na janga hilo. Papa Francisko anawaombea marehemu, na majeruhi wapone na kuwafariji wale wanaoomboleza kwa kuondokewa na wapendwa wao na nyumba zao. Aidha Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu awaunge mkono Watu wa Morocco katika majaribu haya na kwa mamlaka ya kiraia na huduma za misaada. Zaidi ya yote, Papa anaombea baraka za Mungu kama ishara ya faraja.
Mtikisiko wa kwanza wa tetemeko la ardhi ulirekodiwa saa 5.11 usiku wa Ijumaa tarehe 8 Septemba kuamkia Jumamosi. Kitovu hicho kilipatikana kilomita 16 kutoka kijiji cha Tata N'Yaaqoub, katika eneo la Marrakech. Idadi ya vifo imeongezeka saa baada ya saa na kufikia 820, kulingana na idadi ya muda mfupi iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani. Hdi sasa watu 672 walijeruhiwa, ambapo 205 wako katika hali mbaya. Picha na video za nyumba zilizoharibiwa na watu mitaani zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii na tovuti za habari. Wakati huo huo, miito ya uchangiaji wa haraka wa damu inatolewa nchini humo.
Maandamano mengi ya mshikamano kutoka kwa serikali za nchi zote ulimwenguni Kanisa pia mara moja liliingia katika mchakato huo kupitia Caritas. Baraza la Maaskofu wa Italia (CEI) pia limetangaza kwamba limeamua kama njia ya haraka ya msaada kutenga euro elfu 300 kutoka kwenye mfuko wa fedha uitwao 8x1000 ambazo wananchi hutenga kwa ajili ya Kanisa Katoliki. “Rambirambi zetu na ukaribu wetu ziende kwa dada na kaka wa Moroko. Kwa kuwa karibu na idadi ya watu walioathiriwa na tukio hili la kutisha, tunawaombea waathiriwa na familia zao. Pia tunahakikisha uungwaji mkono wa Makanisa yetu, tukikusanyika karibu na wale wote ambao wameathiriwa na janga hili na kwa jumuiya ya Morocco nchini Italia ambao mioyo yao imejeruhiwa,” alisema hayo Kardinali Matteo Zuppi, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu katoliki la Bologna na rais wa Baraza la Maaskofu Italia CEI.
Mgao wa msaada kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia ( CEI,) kupitia Caritas Italiana, utasaidia kukidhi mahitaji ya kimsingi, kwa mujibu wataarifa kwa vyombo vya habari. Caritas Italia ambayo imeshirikiana kwa miaka mingi na Caritas nchini Morocco katika miradi mbalimbali kwa ajili ya watu wanaoishi katika mazingira magumu, kama vile wahamiaji na watoto wadogo wasio na wazazi - inafuatilia mara kwa mara habari zinazowasili kutoka nchi ya Kaskazini mwa Afrika kufuatilia hali na kutathmini hali ya dharura zaidi.