Papa anasubiriwa sana kwa Mkutano!
Na Fr. Paul Samasumo - Marseille
Katika mwisho wa Juma yaani Ijumaa na Jumamosi tarehe 22 na 23 Septemba 2023, Baba Mtakatifu Francisko anafanya Ziara ya Kitume ya siku mbili katika mji wa kusini mwa Ufaransa wa Marsiglia. Ni katika hitimisho la Mikutano ya Mediterania. Hii ni mipango au makongamano yanayoongozwa na Kanisa yanayofanyika kila mwaka katika jiji au mji tofauti katika nchi za zinazopakana na Mediterania. Mnamo 2020 na 2022 zilifanyika katika mji wa Firenze na Bari nchini Italia.
Mkutano unawaleta maaskofu na vijana pia
Mwaka huu 2023 huko Marsiglia, Mikutano ya Mediterania imewaleta pamoja Maaskofu wa Kikatoliki wapatao 70 na vijana 120 wenye umri wa miaka 20 hadi 35 kutoka pande zote za Bahari ya Mediterania. Pia kuna Waislamu kadhaa na washiriki wa madhehebu ya imani nyingine. Kwa upande wa Baba Mtakatifu, ziara hii inatoa fursa ya kukuza udugu katika Bahari ya Mediterania. Kwa njia hiyo ziara hiyo itawahimiza viongozi wa kidini kubuni njia yao ya kipekee katika nia yao ya kuwatumikia watu wa eneo linalopendwa sana na Papa Francisko.
Vikwazo vya vifaa
Kuhusu vifaa, Papa Francisko anawasili katikati ya Kombe la Dunia la Raga ya 2023 huko Marsiglia. Kwa hiyo ni juma nzito katika jiji hili lenye shangwe. Timu yetu ya Vatican News inayohabarisha ziara ya upapa ilikumbana na changamoto ya kupata Taxi mara tu baada ya kufika na tulishangaa jinsi ambavyo michezo ya Raga na ziara ya Papa vimekwenda pamoja. Hatimaye, tulipopata Taxi na tulimwuliza dereva wetu maoni yake kuhusu Papa Francisko kuja jijini humo. Jibu lake lilikuwa la kufundisha sana, kwa sababu alisema: "Sote tunaamini katika Mungu mmoja. Yeyote anayeamini katika Mungu na kufanya kazi kwa ajili ya amani katika Mediterania, anataka kumsikiliza. Nimevutiwa na ziara hii," lilikuwa jibu lake.
Watashiriki misa zaidi ya watu 50,000
Kwa upande wa Kardinali Jean-Marc Aveline, Askofu Mkuu wa Marsiglia alisema moja ya mambo muhimu zaidi yatakuwa Misa ambayo Papa Francisko ambayo ataadhimisha katika uwanja wa Vélodrome. Misa hiyo imepangwa kufanyika Jumamosi tarehe 23 Septemba 2023 mchana kabla ya Papa kurejea mjini Vatican. Zaidi ya watu 50,000 wanatarajiwa kuhudhuria. Misa hii, alisema Kardinali Aveline, "italeta pamoja Marsiglia katika utofauti wake wote." Katika fursa hiyo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia anatarajiwa kuhudhuria. Mara ya mwisho Papa kutembelea Marsiglia ilikuwa mnamo mwaka 1533 wakati Papa Clement VII wa Firenze alipotembelea jiji hilo. Kwa njia hiyo karne tano baadaye, ziara ya Mwisho wa Juma 22 -23 Septemba, Papa Francisko tayari anaweka historia nyingine mpya.