Papa amemshukuru Kardinali Ladaria kwa huduma yake
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 5 Septemba 2023 amefanya ziara ya kushtukiza katika Baraza la Kipapa Mafundisho Tanzu ya Kanisa kabla ya masaa 24 baada ya kurejea kutoka katika ziara yake ya Kitume nchini Mongolia. Msemaji wa vyombo vya habari Vatican Dk. Matteo Bruni, alitangaza katika taarifa yake kwamba Baba Mtakatifu Francisko alitembelea Baraza hilo Jumanne mara baada ya saa 3.00 asubuhi, ambapo alikutana na kumshukuru Kardinali Luis Francisco Ladaria kwa kazi yake yote katika miaka yake akihudumu kama Msimamizi wa Baraza hilo.
Baada ya kukutana na Kardinali huyo Mjesuit, Baba Mtakatifu Francisko pia alisalimiana na viongozi mbalimbali ndani ya Baraza hilo. Mnamo Julai 2008, Baba Mtakatifu Benedikto XVI, alimteua Ladaria, Mjesuit na Mtaalimungu kutoka Hispania, kuwa Katibu wa Baraza hilo wakati huo na kumfanya kuwa Askofu Mkuu. Na Papa Francisko alimteua kuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo wakati wa upapa wake, akimrithi Kardinali Gerhard Ludwig Muller.
Kadinali Ladaria aliyeteuliwa mnamo mwaka wa 2018, kuwa Kadinali alihudumia kama Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa tangu 2017 hadi 2023. Kadinali mteule Victor Manuel Fernández wa La Plata, nchini Argentina, anaye mrithi Kadinali Ladaria mwenye umri wa miaka 79, kama Mwenyekiti wa Baraza hilo hivi karibuni atachukua madaraka katikati ya mwezi Septemba 2023. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha ziara yake ya siku nne ya Kitume katika nchi ya Asia ya Mongolia kwa kutembelea jumuiya ya Wakatoliki yenye watu 1,500, wengi wao wakiwa wamejikita kukaa katika mji mkuu wa taifa hilo Ulaanbaatar. Ziara hiyo imekuwa ni ziara ya 43 ya kitume ya Papa kuwa Nje ya Nchi kwa kuzitembelea nchi 61 akiwa kama Papa.