Tafuta

Papa:Afrika sio mgodi wa kunyonywa au kuporwa inatosha kuisonga!

Ushuhuda wa Mtakatifu Daniel Comboni,mmisionari katika Bara la Afrika,uliotolewa na Fransisko kwa washiriki wa katekesi yake Jumatano Septemba 20 ni fursa ya kusisitiza kwamba katika kazi ya uinjilishaji kila mtu anahusika na wahusika wote:basi ukoloni wa kiuchumi ambao leo hii unafanya utumwa kwa bara la Afrika ukome,Ameonya Papa.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 20 Septemba 2023, ameendelea na katekesi yake kuhusu ari ya kitume ambao amegeukia bara la Afrika na mada Mtume Mtakatifu Daniel Comboni, na nabii wa utume. "Kwa kipindi cha katekesi juu ya shauku ya uinjilishaji, tuchukue muda leo hii kwa kutazama ushuhuda wa Mtakatifu Daniel Comboni. Alikuwa mtume aliyejawa na bidii kwa ajili ya Afrika. Aliandika juu ya watu hawa kuwa wameumiliki moyo wangu unaoishi kwa ajili yao peke yake (Maandiko, 941). ‘Nitakufa na Afrika midomoni mwang’ (Maandiko, 1441). Na aliwaandikia hivi: “Siku zangu zenye furaha zaidi zitakuwa nitakapotoa maisha yangu kwa ajili yenu” (Maandiko, 3159). Baba Mtakatifu kwa kuongezea amesema “ Huu ni usemi wa mtu ambaye yuko katika upendo na Mungu na pamoja na kaka na dada aliokuwa akiwahudumia katika utume, ambaye hakuchoka kuwakumbusha kwamba: “Yesu Kristo aliteswa na kufa kwa ajili yao pia” (Maandiko yake, 2499; 4801).

Baba Mtakatifu aidha amesema kuwa alithibitisha hili katika muktadha wenye sifa ya kutisha ya utumwa, ambayo alikuwa shahidi wake. Utumwa hunamlenga mwanadamu, ambaye thamani yake imepunguzwa kuwa ya manufaa kwa mtu au kitu. Lakini Yesu, Mungu alimuumba mwanadamu, aliinua hadhi ya kila mwanadamu na kufichua uwongo wa utumwa. Katika nuru ya Kristo, Comboni alifahamu ubaya wa utumwa. Zaidi ya hayo, alielewa kwamba utumwa wa kijamii una mizizi katika utumwa wa kina zaidi, ule wa moyo, ule wa dhambi, ambao Bwana hutuweka huru kutoka kwake.  Kwa hiyo, kama Wakristo, tumeitwa kupambana na kila aina ya utumwa. Kwa bahati mbaya, hata hivyo, utumwa, kama ukoloni, si kitu cha zamani, Papa amebainisha.

Kwa Afrika ambayo Comboni aliipenda sana, ambayo leo  hii imekumbwa na migogoro mingi, unyonyaji wa kisiasa ulitoa nafasi kwa ukoloni wa kiuchumi ambao ulikuwa utumwa sawa. (…) Hili ni janga ambalo ulimwengu ulioendelea zaidi kiuchumi mara nyingi hufunga macho, masikio na mdomo wake”. Kwa hivyo Papa Francisko ametoa wito wake akirudia maneno aliyosema wakati yuko ziarani DRC kwamba “Ninarudia ombi langu: “Acheni kuisonga Afrika: si mgodi wa kuvuliwa au eneo la kuporwa”(Hotuba yake kwa Viongozi wa Kuu huko, Kinshasa, 31 Januari 2023). Papa baadaye amesema “Hebu turudi kwenye maisha ya Mtakatifu Danieli. Baada ya kipindi cha kwanza barani Afrika, ilimbidi aondoke katika utume wa kimisionari kutokana na sababu za kiafya. Wamisionari wengi sana walikuwa wamekufa baada ya kuugua malaria, jambo lililochangiwa na ufahamu wa kutosha wa hali ya mahali hapo. Ingawa wengine waliiacha Afrika, Comboni hakufanya hivyo. Baada ya muda wa utambuzi, alihisi Bwana alikuwa akimtia moyo katika njia mpya ya uinjilishaji, ambayo alijumlisha kwa maneno haya: “Iokoe Afrika na Afrika” (Maandiko yake 2741).

Huu ulikuwa ufahamu wenye nguvu ambao ulisaidia kufanya upya ufikiaji wake wa umisionari: watu ambao walikuwa wamehubiriwa hawakuwa vitu, bali mafunzo  ya utume. Mtakatifu Danieli alitaka kuwafanya Wakristo wote washiriki katika shughuli ya uinjilishaji. Akiwa na roho hiyo, aliunganisha mawazo na matendo yake, akiwahusisha makasisi wa mahali hapo na kuendeleza huduma ya walei ya katekista. Pia alifikiria maendeleo ya mwanadamu kwa njia hii, kukuza sanaa na taaluma, kukuza jukumu la familia na la wanawake katika mabadiliko ya utamaduni na jamii. Ni jinsi gani ilivyo muhimu hata leo hii, kufanya imani na maendeleo ya binadamu kusonga mbele ndani ya muktadha wa utume, badala ya kupandikiza mifano kutoka nje au kuwawekea mipaka kwenye ustawi wa tasa!” Papa amesisitiza. Shauku kuu ya umisionari ya Comboni, hata hivyo, haikuwa tunda la jitihada za kibinadamu. Hakuongozwa na ujasiri wake mwenyewe, au kuhamasishwa na tunu muhimu kama vile uhuru, haki na amani. Bidii yake ilitokana na furaha ya Injili, iliyotokana na upendo wa Kristo ambao uliongoza kwa upendo wa Kristo! Mtakatifu Daniel aliandika, kuwa “Utume mgumu na ugumu kama wetu hauwezi kufumbiwa macho, wanayoishi watu wenye shingo potofu waliojawa na ubinafsi na kujipenda wenyewe, ambao hawajali afya zao na wongofu wa roho inavyopaswa”.

Na kwa upande wake  akaongeza, “Inapaswa kuwatia moto mapendo ambayo chanzo chake ni Mungu na upendo wa Kristo; mtu anapompenda Kristo kiukweli, basi ufukara, mateso na mauaji ya imani huwa matamu” (Maandiko 6656). Alitamani kuona wamisionari wenye bidii, wenye furaha, waliojitolea na aliandika kuwa wamisionari, watakatifu na wenye uwezo. (…)”Kwanza kabisa watakatifu, yaani, huru kabisa na dhambi na kosa kwa Mungu na wanyenyekevu. Lakini hii haitoshi: tunahitaji upendo unaowawezesha raia wetu” (Maandiko 6655). Papa amesisitiza kuwa  upande wa Comboni, chanzo cha uwezo wa kimisionari, kwa hiyo, ni upendo, hasa, bidii ambayo yeye aliyafanya mateso ya wengine kuwa yake, akiyahisi katika mwili wake mwenyewe, na kujua jinsi ya kuyapunguza, kama Mkrene mwema wa ubinadamu. Kwa kuongezea, shauku yake ya uinjilishaji kamwe haikumpelekea kutenda kama mwimbaji peke yake, lakini daima katika umoja na  katika Kanisa. “Nina uhai mmoja tu wa kutoa kwa ajili ya wokovu wa roho hizo: Laiti ningalikuwa na elfu moja ya kuteketezwa kwa ajili hii” (Maandiko, 2271).

Uzima ni moja au elfu moja: sisi ni nani peke yetu na maisha yetu mafupi, ikiwa sio Kanisa zima linalofanya utume? Je! ni bidii gani inayofanya kazi ndani yetu, kwa hakika Comboni aonekana kutuuliza, ikiwa sio ya kikanisa? Papa amesema. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu amesisitiza kuwa  Mtakatifu Danieli anashuhudia upendo wa Mchungaji Mwema anayekwenda kumtafuta aliyepotea na kutoa maisha yake kwa ajili ya kundi. Bidii yake ilikuwa ya nguvu na ya kinabii katika kupinga kutojali na kutengwa. Katika barua zake, alialika kwa bidii Kanisa lake pendwa ambalo lilikuwa limesahau Afrika kwa muda mrefu sana. Ndoto ya Comboni ni ile ya Kanisa linalofanya mambo ya kawaida na wale waliosulubishwa na historia, ili kupata ufufuko pamoja nao. Ushahidi wake unaonekana kutaka kurudia kwetu sote, wanaume na wanawake wa Kanisa: “Msiwasahau maskini, wapendeni kwa maana Yesu aliyesulubiwa yumo ndani yao, akingojea kufufuka tena.”

Katekesi ya Papa 202 Septemba

 

20 September 2023, 11:37