Waraka wa "Desiderio Desiderati": Majiundo ya Kiliturujia ya Watu wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, tarehe 29 Juni 2022 alizindua Waraka wa Kitume wa “Desiderio desideravi hoc Pascha manducare vobiscum, antequam patiar (Lk 22:15)” kwa kifupi “DESIDERIO DESIDERAVI”: Kuhusu Majiundo ya Kiliturujia ya Watu wa Mungu. Ni Waraka unaopata chimbuko lake kutoka katika maneno ya Kristo Yesu aliyewaambia Mitume wake: “Nilitaka sana kula mlo huu wa Pasaka pamoja nanyi kabla sijafa.” Lk 22:15. Baba Mtakatifu anasema, Waraka huu wa Kitume unasheheni tafakari kuhusu Liturujia, jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mwendelezo wa Barua Binafsi: Kuhusu Liturujia “Motu Proprio “Traditionis custodes” yaani Walinzi wa Mapokeo ya Kanisa: Juu ya Matumizi ya Liturujia ya Kirumi Kabla ya Mageuzi ya Mwaka 1970. “Sheria Mpya Kuhusu Ibada ya Misa Takatifu, Maaskofu mahalia wanawajibika zaidi.” Makundi ya waamini yanayotumia “Missale Romanarum” yaani Misale ya Kirumi ya Mwaka 1962 iliyorekebishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI miaka kadhaa iliyopita imefanyiwa marekebisho na Baba Mtakatifu Francisko na anatoa sababu msingi zilizompelekea kuandika Barua Binafsi “Motu Proprio “Traditionis custodes” yaani Walinzi wa Mapokeo ya Kanisa: Juu ya Matumizi ya Liturujia ya Kirumi Kabla ya Mageuzi ya Mwaka 1970. Papa Francisko anasema, ni wajibu wa Askofu mahalia kuhakikisha kwamba hata makundi ya waamini yanayotumia Misale hii kuyatambua na kuheshimu mabadiliko ya Kiliturujia yanayofanywa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Liturujia na kadiri ya mwanga angavu wa Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, yaani “Magisterium.”
Waraka wa Kitume wa Papa Francisko “DESIDERIO DESIDERAVI”: Kuhusu Majiundo ya Kiliturujia ya Watu wa Mungu” umegawanyika katika vipengele 65 na unahitimishwa na barua ya kichungaji kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa ajili ya Shirika lake. Kwa ufupi Baba Mtakatifu Francisko anazungumzia kuhusu Liturujia ya “leo” katika historia ya wokovu. Liturujia ni mahali muafaka pa kukutana na Kristo Yesu. Kanisa ni Sakramenti ya Mwili wa Kristo Yesu, maana, kutoka ubavuni mwa Kristo akilala Msalabani ilitoka Sakramenti ya ajabu ya Kanisa lote. Baba Mtakatifu anafafanua maana halisi ya Liturujia Kitaalimungu; Liturujia kama dawa ya kutibu magonjwa ya malimwengu kiroho. Mama Kanisa anatamani sana waamini wote waongozwe kwenye kuyashiriki maadhimisho ya kiliturujia kwa utimilifu, ufahamu na utendaji. Waamini wanaalikwa kugundua tena, kutunza na hatimaye, kuishi ukweli na nguvu za maadhimisho ya Liturujia ya Kikristo, kwa kukazia ushirika wa waamini wote. Huu ni mwaliko kwa waamini kila siku kugundua uzuri wa ukweli wa maadhimisho ya Liturujia ya Kikristo. Anakazia mshangao wa Fumbo la Pasaka kama sehemu muhimu ya tendo la maadhimisho kiliturujia, linalo dai mwendelezo wa majiundo makini ya Kiliturujia kwa upande wa watu watakatifu wa Mungu. Hapa Baba Mtakatifu Francisko anachota amana na utajiri mkubwa unaobubujika kutoka katika Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Liturujia kwani tendo la wokovu linaloendelezwa na Mama Kanisa hutimizwa katika Liturujia.
Waamini watambue kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya Kristo; wajenge na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu kama chemchemi ya furaha na matumaini na kwamba, hiki ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha Kanisa la Kisinodi. Kristo Yesu yupo daima katika Kanisa lake, kwa jinsi ya pekee katika katika maadhimisho ya kiliturujia. Yupo kwenye Sadaka ya Misa Takatifu katika nafsi ya Kasisi. “Yeye ambaye alijitoa mara moja Msalabani, anajitoa tena mwenyewe kwa huduma ya Mapadre, yupo chini ya maumbo ya Ekaristi. Yupo kwa nguvu yake katika Sakramenti zake, Neno la Mungu, katika Sala na Zaburi. Baba Mtakatifu anahimiza majiundo makini ya sanaa kwa ajili ya maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Altare katika maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa inapata umuhimu wa pekee kabisa, kwani Altare hai ni Kristo Yesu mwenyewe. Naye Kristo Yesu akiwa ametundikwa pale Msalabani alitobolewa ubavuni kwa mkuki na mara ikatoka Damu na Maji chemchemi ya Sakramenti za Kanisa na kiini cha masifu na shukrani kwa Mwenyezi Mungu. Maji hayo ndiyo ilikuwa ishara ya Sakramenti ya ubatizo, ambayo kwayo waamini wanapata kuondolewa dhambi ya asili na dhambi binafsi pamoja na adhabu zake. Kwa njia na mastahili ya Mwana wa pekee wa Mungu, kwa Ubatizo waamini wanapokea hadhi ya kuwa wana wa Mungu na warithi wa Ufalme wa Mungu. Zaidi sana kwa ubatizo waamini wanampokea Roho Mtakatifu, Roho wa Kristo mwenyewe. Hii ndiyo sababu ya msingi ya wao kuitwa Wakristo.
Hivyo basi, Wakristo wanapoiangalia Altare wamwone Kristo aliyejitoa sadaka Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Vivyo hivyo kama mwamini ni kiungo cha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, anapaswa kutambua kuwa yeye ni sehemu ya Altare. Ndiyo maana kila mmoja anapaswa kuwa sadaka, kwa Mungu na kwa jirani yake. Aidha, chochote kinachotabarukiwa kinapaswa kutumika kwa ajili ya Mungu tu, kama vile kila mbatizwa anavyopaswa kuwa ni kwa ajili ya Mungu, kinyume chake ni kujiteketeza. Altare ina maana sana katika maisha ya mwamini. Altare ni kielelezo makini cha Kristo Yesu katika hali yake yote. Ni Kristo Yesu: anayeganga na kuponya, anayesamehe na kutakasa; Kristo anayefundisha, kuonya na kuongoza. Waamini wajifunze kuwa na fadhila ya unyenyekevu na toba wanapoijongea Altare ya Bwana, ili kweli sadaka yao iweze kumpendeza Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa kwa kuzingatia maneno na vitendo wakati wa maadhimisho. Watunze kimya kikuu, wanapotakiwa kufanya hivyo, waitikie kwa sauti nyofu. Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu, alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, yaani Mwili na Damu yake Azizi, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. “Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, Twaeni; huu ndio mwili wangu. Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote. Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu.” Mk 22-25. Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa yanapaswa kupyaisha maisha na utume wa Padre kila mara anapoyaadhimisha. Baba Mtakatifu anawaalika watu watakatifu wa Mungu kuchota amana na utajiri unaobubujika kutoka katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, kabla hata ya kujikita katika tasaufi ya maisha ya Kikristo.
Ni wakati wa kufanya rejea katika Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Liturujia Takatifu, daima sala na ushirika wa Kanisa vikipewa kipaumbele cha kwanza. Waamini watambue umuhimu wa Mwaka wa Liturujia, Dominika, siku ambayo waamini wanajumuika: kusikiliza Neno la Mungu, Kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kuadhimisha ukumbusho wa mateso, ufufuko na utukufu wa Kristo Yesu. Hii ni siku ya shukrani. Dominika ni msingi na kiini cha mwaka mzima wa Liturujia. Kumbukumbu za watakatifu na mashuhuda wa imani; Vipindi cha Majilio na Kwaresima viadhimishwe kwa ibada na uchaji. Rej. SC 102-111. Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa yanogeshe umoja, ushiriki na utume wa Kanisa. Kwa nguvu ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu, waamini waweze kuwa ni mashuhuda amini wa Habari Njema ya Wokovu, tayari kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ukarimu na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anawaalika waamini wote kutupilia mbali kinzani na misigano ya maadhimisho ya Kiliturujia na kuanza kujizatiti zaidi kumsikiliza Roho Mtakatifu anachosema kwa ajili ya Kanisa la Kristo; wajenge na kudumisha ushirika wa Kanisa na kuendelea kushangaa kuhusu ukuu, uzuri na utakatifu wa Liturujia ya Kanisa. Kristo Yesu amewaachia wafuasi wake kumbukumbu endelevu ya tamaa yake ya kula Pasaka pamoja na wafuasi wake.