Tafuta

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 unanogeshwa kwa kauli mbiu: “Zungumzeni Ukweli Katika Upendo” Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 unanogeshwa kwa kauli mbiu: “Zungumzeni Ukweli Katika Upendo”  (Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni 2023

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 unanogeshwa kwa kauli mbiu: “Zungumzeni Ukweli Katika Upendo”: Veritatem facientes in caritate. “Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.” Efe 4:15. Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa sababu hii ni sehemu ya programu ya Mkristo!

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., Dar es Salaam.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 unanogeshwa kwa kauli mbiu: “Zungumzeni Ukweli Katika Upendo”: Veritatem facientes in caritate. “Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.” Efe 4:15. Hii ni sehemu ya mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayoongozwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” yatakayofikia kilele chake mwezi Oktoba 2023. Baba Mtakatifu anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ulimwenguni kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa upole na kwa hofu, wakitambua kwamba, wanapaswa kuwa ni madaraja ya kuwaunganisha watu na kawe wasiwe ni kikwazo na kuta za kuwagawa na kuwasambaratisha watu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ujumbe huu uguse pia maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo, ambako inaonekana kuibuka kwa mijadala ya chuki na uhasama na kwamba, huu ni mwaliko wa kurejea tena kwenye msingi wa maisha na utume wa Kanisa. Ni wakati wa kutangaza na kushuhudia ukweli unaosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili. “Zungumzeni Ukweli Katika Upendo” (Efe 4:15) Ndugu wapendwa, Baada ya kutafakari katika miaka iliyopita juu ya vitenzi "kwenda kuona" na "kusikiliza" kama masharti ya mawasiliano mazuri, kupitia ujumbe huu kwa Siku ya 57 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni ningependa kuzingatia "kuzungumza kwa moyo". Ni moyo uliotusukuma kwenda, kuona na kusikiliza, na ni moyo unaotusukuma kuelekea njia iliyo wazi na ya kukaribisha ya kuwasiliana. Tukishafanya mazoezi ya kusikiliza, ambayo yanadai kusubiri na subira, pamoja na kutafakari kwanza kabla ya kutoa maoni yetu kwa njia ya chuki, tunaweza kuingia katika mienendo ya mazungumzo na kushiriki, ambayo hasa ni ile ya kuwasiliana kwa njia ya ukarimu.

Papa Francisko: Zungumzeni ukweli katika upendo
Papa Francisko: Zungumzeni ukweli katika upendo

Baada ya kumsikiliza mwingine kwa moyo safi, tutaweza pia kusema, kuufuata ukweli kwa upendo (rej. Efe 4:15).  Hatupaswi kuogopa kutangaza ukweli, hata ikiwa wakati fulani inatufanya tujisikie vibaya. Kwa sababu "programu ya Mkristo" - kama Benedikto XVI alivyoandika - "ni 'moyo unaoona'". [1] Moyo unaofichua ukweli wa uwepo wetu kwa kudunda kwake, na kwa sababu hii, unapaswa kusikilizwa. Hili hupelekea wale wanaosikiliza kujiweka sawa kwa urefu wa wimbi, hadi kuweza kusikia ndani ya mioyo yao pia mapigo ya moyo ya mwingine. Kisha muujiza wa kukutana unaweza kutokea, ambao unatufanya tutazamane kwa huruma, tukikaribisha udhaifu wetu wa pande zote kwa heshima badala ya kuhukumu na kupanda mbegu ya mifarakano na migawanyiko. Yesu anatuonya kwamba kila mti hutambulikana kwa matunda yake (rej. Lk 6:44): “Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya hazina yake hutoa mabaya; kwa maana kinywa chake hunena yaujazayo moyo wake” (mstari 45). Hii ndiyo sababu, ili kuwasiliana ukweli kwa hisani, ni muhimu kuutakasa moyo wa mtu. Ni kwa kusikiliza tu na kuzungumza kwa moyo safi ndipo tunaweza kuona zaidi ya kuonekana nakushinda kelele isiyoeleweka ambayo, pia katika sekta ya habari, haitusaidii kupambanua katika ulimwengu mgumu tunamoishi. Wito wa kuzungumza na moyo unazipa changamoto nyakati tunazoishi kwa kiasi kikubwa, ambazo zina mwelekeo wa kutojali na kukasirika, wakati mwingine hata kwa msingi wa habari potofu ambayo inapotosha ukweli. 

Tangazeni ukweli unaosimikwa katikaq tunu msingi za Kiinjili
Tangazeni ukweli unaosimikwa katikaq tunu msingi za Kiinjili

Kuwasiliana kwa ukarimu Kuwasiliana kwa njia ya upole kunamaanisha kwamba wale wanaotusoma au kutusikiliza wanaongozwa kukaribisha ushiriki wetu katika furaha, hofu, matumaini na mateso ya wanawake na wanaume wa nyakati hii. Wale wanaozungumza kwa njia hii wanampenda mwingine kwa sababu wanajali na kulinda uhuru wao bila kuuvunja. Tunaweza kuuona mtindo huu katika msafiri wa ajabu ambaye anazungumza na wanafunzi kuelekea Emau, baada ya mkasa uliotokea Golgotha. Yesu Mfufuka anazungumza nao kwa moyo, akiandamana na safari ya mateso yao kwa heshima, akijipendekeza mwenyewe na sio kujilazimisha, akifungua akili zao kwa upendo kuelewa maana ya kina ya kile kilichotokea. Kwa kweli, wanaweza kusema kwa furaha kwamba mioyo yao iliwaka ndani yao alipokuwa akizungumza nao njiani na kuwafafanulia Maandiko (rej. Lk 24:32). Katika kipindi cha kihistoria kilicho na migawanyiko na tofauti - ambayo kwa bahati mbaya hata jumuiya ya kikanisa haiwezi kinga - kujitolea kwa kuwasiliana "kwa moyo wazi" haihusu tu wale walio katika sekta ya mawasiliano; ni jukumu la kila mtu. Sisi sote tumeitwa kutafuta na kusema ukweli na kufanya hivyo kwa hisani. Sisi Wakristo tunahimizwa kila mara kuuzuia ulimi wetu na uovu (taz. Zab 34:13), kwa sababu kama Maandiko yanavyotufundisha, kwa ulimi huo huo tunaweza kumbariki Bwana na kuwalaani wanaume na wanawake walioumbwa kwa mfano wa Mungu. (taz. Yak 3:9). Neno lolote ovu lisitoke vinywani mwetu, bali “lililo jema la kuwajenga, kama lipasavyo, ili liwape neema wale wanaosikia” (Efe 4:29).

Vijana wa Jugo Media Network wakiwa kwenye utume!
Vijana wa Jugo Media Network wakiwa kwenye utume!

Wakati mwingine mazungumzo ya kirafiki yanaweza kufungua mioyo migumu zaidi. Pia tunao ushahidi wa jambo hili katika fasihi. Ninaufikiria ukurasa mmoja katika Sura ya XXI ya “The Betrothed” ambamo Lucia anazungumza kwa moyo na Innominato [asiyetajwa] hadi akaweka chini silaha kutokana na nguvu ya upendo. Tunapata uzoefu huu katika jamii, ambapo wema, sio tu ni swala la kistaarabu pekee bali pia ni dawa ya kweli ya ukatili, ukatili ambao kwa bahati mbaya unaweza kuharibu mioyo na kufanya mahusiano kuwa sumu. Tunauhitaji (Upendo) katika sekta ya vyombo vya habari, ili mawasiliano yasichochee uhasama unaotia hasira, kuzua ghadhabu na kusababisha migongano, bali usaidie watu kutafakari kwa amani na kutafsiri kwa moyo wa kukosoa na wenye heshima siku zote.  Kuwasiliana moyo kwa moyo: "Ili kuzungumza vizuri, inatosha kupenda vizuri" Moja ya mifano angavu na bado ya kuvutia ya "kuzungumza kwa moyo" inatolewa na Mtakatifu Francisko wa Sales, Mwalimu wa Kanisa, ambaye niliandika juu yake katika Waraka wa Kitume, Totum Amoris Est, miaka 400 baada ya kifo chake. Mbali na maadhimisho haya muhimu, ningependa kutaja kumbukumbu nyingine inayofanyika mwaka 2023: miaka mia moja ya kutangazwa kwake kama mlinzi wa waandishi wa habari wa Kikatoliki na Pius XI pamoja na Waraka wa Kitume wa, Rerum Omnium Perturbationem.  Francisko wa Sales alikuwa ni Askofu mahiri, mwenye akili timamu, mwenye kuzaa matunda na mwanatheolojia wa kina, alikuwa Askofu wa Geneva mwanzoni mwa karne ya XVII wakati wa miaka migumu iliyoambatana na mabishano makali na wafuasi wa Calvin. Mtazamo wake wa upole, ubinadamu na utayari wa kuzungumza kwa subira na kila mtu, hasa na wale wasiokubaliana naye, vilimfanya kuwa shahidi wa ajabu wa upendo wa huruma wa Mungu. 

Tangazeni ukweli katika upendo
Tangazeni ukweli katika upendo

Mtu anaweza kusema juu yake: "Sauti ya kupendeza huongeza marafiki, na ulimi wa neema huongeza adabu" (Sira 6: 5). Baada ya yote, moja ya kauli zake maarufu zaidi, "moyo huzungumza na moyo", iliongoza vizazi vya waamini, kati yao Mtakatifu John Henry Newman, ambaye aliichagua kama kauli mbiu yake, “Cor ad cor loquitur.” Aliamini kwamba "Ili kuzungumza vizuri, inatosha kupenda vizuri". Inaonyesha kwamba, kwake, mawasiliano hayapaswi kamwe kufanywa kuwa kitu bandia, kuwa mbinu ya kimasoko, kama inavyosemwa siku hizi, lakini badala yake ni onyesho la roho, uso unaoonekana wa kiini cha upendo kisichoonekana kwa macho.  Kwa mtazamo wa Mtakatifu Francisko wa Sales, "moyoni na kupitia moyo, kunatokea mchakato mdogo ila mkali wenye kutuunganisha unaotufanya tupate kumjua Mungu". [2] Kwa "kupenda vyema", Mtakatifu Francisko alifaulu kuwasiliana na Martin, bubu-kiziwi, na kuwa rafiki yake. Hii ndiyo sababu anajulikana pia kama mlinzi wa watu wenye matatizo katika kuwasiliana. Ni kutokana na "kigezo hiki cha upendo" kwamba, kwa njia ya maandishi na ushuhuda wake wa maisha, Askofu mtakatifu wa Geneva anatukumbusha kwamba "sisi ni kile tunachowasiliana". Hii ni kinyume na tunachoona leo, wakati ambapo - kama tunavyopitia hasa kwenye mitandao ya kijamii - mara nyingi mawasiliano yanatumiwa ili ulimwengu utuone jinsi tungependa kuwa na si kama tulivyo.  Mtakatifu Francisko wa Sales alisambaza nakala nyingi za maandishi yake kati ya jumuiya ya Geneva. Akili hii ya "kiuandishi" ilimletea sifa ambayo ilikwenda mbali zaidi ya mipaka ya jimbo lake na bado inadumu hadi leo. Maandishi yake, Mtakatifu Paulo wa Sita aliona, yanatoa usomaji “wa kufurahisha sana, wenye kufundisha na wenye kusisimua”. [3] Tukiangalia leo katika nyanja ya mawasiliano, je, hizi si sifa haswa ambazo makala, ripoti, kipindi cha televisheni au redio au chapisho la mitandao ya kijamii linapaswa kujumuisha? Watu wanaofanya kazi katika sekta ya mawasiliano na wahisi kuhamasishwa na mtakatifu huyu wa huruma, kutafuta na kusema ukweli kwa ujasiri na uhuru na kukataa jaribu la kutumia maneno ya kusisimua na ya kupinga. 

Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu
Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu

Kuzungumza kwa moyo, katika mchakato wa Sinodi Kama nilivyosisitiza, “Katika Kanisa pia, kuna haja kubwa ya kusikiliza na kusikilizana. Ni zawadi ya thamani zaidi na ya uzima tunayoweza kupeana sisi kwa sisi”. [4] Kusikiliza bila ubaguzi, kwa uangalifu na kwa uwazi, huzaa kuzungumza kulingana na mtindo wa Mungu, unaokuzwa na ukaribu, huruma na upole. Tuna hitaji kubwa katika Kanisa, la mawasiliano ambayo huwasha mioyo, ambayo ni mafuta kwenye majeraha na ambayo yanaangazia safari ya kaka na dada zetu.  Nina ndoto ya kuona mawasiliano ya kikanisa ambayo yanajua jinsi ya kujiruhusu kuongozwa na Roho Mtakatifu, ya upole na wakati huo huo, ya kinabii, ambayo yanajua jinsi ya kutafuta njia mpya na njia bora za kutangaza kama yanavyotakiwa kufanya katika milenia ya tatu. Mawasiliano ambayo huweka katikati uhusiano na Mungu na jirani, hasa mhitaji zaidi, na ambayo yanajua jinsi ya kuwasha moto wa imani badala ya kuhifadhi majivu ya ubinafsi. Njia ya mawasiliano iliyosimikwa kwenye unyenyekevu katika kusikiliza na ambayo kamwe haitenganishi ukweli na upendo.   Kuondoa silaha rohoni kwa kusambaza lugha ya amani “Ulimi laini huvunja mfupa,” kinasema kitabu cha Mithali (25:15). Leo kuliko wakati mwingine wowote, kuzungumza kwa moyo ni muhimu ili kukuza utamaduni wa amani mahali ambapo kuna vita; kufungua njia zinazoruhusu mazungumzo na upatanisho mahali ambapo kuna chuki na uadui. Katika muktadha wa kushangaza wa mzozo wa kimataifa tunaopitia, ni muhimu kudumisha aina ya mawasiliano ambayo sio ya chuki. 

Waamini wajenge utamaduni wa majadiliano ya kidini na kiekumene
Waamini wajenge utamaduni wa majadiliano ya kidini na kiekumene

Ni muhimu kuondokana na tabia ya "kuwadharau na kuwatukana wapinzani badala ya kufungua mazungumzo ya heshima". [5] Tunahitaji wawasilianaji ambao wako tayari kwa mazungumzo, wanaohusika katika kukuza upokonyaji silaha na waliojitolea kuondoa saikolojia ya kivita ambayo imejikita mioyoni mwetu, kama Mtakatifu Yohane XXIII alivyohimiza kinabii katika Waraka wake wa Kitume “Pacem In Terris”: “Amani ya kweli inaweza tu kujengwa kwa kuaminiana” (Na. 113).  Imani ambayo haihitaji mawasiliano yaliyofungwa na masharti bali yaliyonyooka kutoka kwa wabunifu ambao wako tayari kujitoa kutafuta misingi ya makubaliano. Kama ilivyokuwa miaka sitini iliyopita, sasa tunaishi pia katika saa ya giza ambayo wanadamu wanaogopa kuongezeka kwa vita ambavyo lazima vikomeshwe haraka iwezekanavyo, pia katika sekta ya mawasiliano. Inatisha kusikia jinsi maneno ya kuangamiza watu na maeneo yanavyosemwa kwa urahisi.  Maneno, kwa bahati mbaya, ambayo mara nyingi hugeuka kuwa vitendo vya kivita vya vurugu mbaya. Hii ndiyo sababu maneno yote ya kivita lazima yakataliwe, pamoja na kila aina ya propaganda inayopotosha ukweli, na kuuharibu kwa malengo ya kiitikadi. Badala yake, kinachopaswa kukuzwa ni aina ya mawasiliano ambayo husaidia kuunda mazingira ya kutatua mizozo kati ya watu. Kama Wakristo, tunajua kwamba hatima ya amani huamuliwa kwa uongofu wa mioyo, kwa kuwa virusi vya vita hutoka ndani ya moyo wa mwanadamu. [6] Kutoka moyoni hutoka maneno sahihi ili kuondoa vivuli vya ulimwengu uliofungwa na uliogawanyika na kujenga ustaarabu ambao ni bora zaidi kuliko ule tulioupokea. Kila mmoja wetu anaombwa kushiriki katika juhudi hii, lakini ni ile inayovutia hasa hisia ya uwajibikaji wa wale wanaofanya kazi katika nyanja ya mawasiliano ili waweze kutekeleza taaluma yao ya utume. Bwana Yesu, Neno safi lililomiminwa kutoka moyoni mwa Baba, atusaidie kufanya mawasiliano yetu kuwa yanayoeleweka, wazi na ya kutoka moyoni. Bwana Yesu, Neno aliyefanyika mwili, atusaidie kusikiliza mapigo ya mioyo, tujitambue tena kama kaka na dada, na kuondoa uhasama unaogawanya. Bwana Yesu, Neno la kweli na upendo, atusaidie kusema ukweli katika upendo, ili tujisikie kama walinzi wa kila mmoja wetu.

Jifunzeni kuzungumza katika ukimya!
Jifunzeni kuzungumza katika ukimya!

Imetolewa Roma, Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran, Januari 24, 2023, Kumbukizi ya Mtakatifu Francisko wa Sales. 

FRANCISCUS

[1] Waraka wa Kitume wa Deus Caritas Est (25 Desemba 2005), 31. [2] Waraka wa Kitume Kitume Totum Amoris Est (28 Disemba 2022). [3] Taz. Waraka wa Kitume Sabaudiae Gemma, wa Maadhimisho ya Miaka 100 ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Francisko wa Sales, Mwalimu wa Kanisa (29 Januari 1967). [4] Ujumbe kwa Siku ya LVI ya Upashanaji Habari Ulimwenguni (24 Januari 2022). [5] Waraka wa Kitume wa Fratelli Tutti (3 Oktoba 2020), 201. [6] Taz. Ujumbe wa Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani (1 Januari 2023).

05 August 2023, 14:35