Papa:Milio ya silaha inazamisha majaribio ya mazungumzo,bali tusikate tamaa
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, katika siku kuu ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, tarehe 15 Agosti 2023, amewasalimia wote waliohudhuria, kuanzia Warumi na mahujaji kutoka nchi mbalimbali. Hasa, amewasalimu vijana wa Jimbo Kuu la Verona, Italia, na kuwatakia kila la kheri kwa uzoefu wao wa kiangazi jijini Roma.
Papa amesema: “Leo tunamkabidhi Maria Aliyepalizwa Mbinguni ombi la amani, katika Ukrainne na katika maeneo yote yaliyosambaratishwa na vita: kuna mengi, kwa bahati mbaya! Milio ya silaha huzamisha majaribio ya mazungumzo; sheria ya nguvu inashinda nguvu ya sheria. Lakini tusikate tamaa, tuendelee kutumaini na kuomba, maana Mungu, ndiye anayeongoza historia. Na yeye atusikilize”.
Baba Mtakatifu aidha katika siku kuu ya Mama amewasalimu vijana wa Parokia ya Mama Safi wa Moyo na amewatakia siku kuu njema, lakini wasisahau kusali kwa ajili yake. Na hatimaye kwa kuwaaga wote amewatakia mlo mwema na mchana mwema!