Papa kwa Mtandao wa wanasheria Katoliki:Lengo ni kuungnanisha watu wajitambue
Na Angella Rwezaula, -Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 26 Agosti 2023 amekutana na washiriki wa Mkutano wa 14 wa Kimataifa wa Mtandao wa Wanasheria Katoliki. Katika hotuba yake Baba Mtakatifu ameonesha furaha ya kuwasalimu katika hafla ya mkutano wao wa kumi na nne wa kila mwaka huko Frascati. Amewashukuru kwa ziara yao. Papa amesema kwa Mada waliyochagua kwa ajili ya mkutano wao mwaka huu, ni “Mapambano makubwa ya Nguvu, Ukamataji wa Biashara na Teknokrasia: Jibu la Kikristo kwa Mienendo ya kudhalilisha Utu", inagusa vipengele muhimu vya maisha yetu. Kwa hakika, “mtazamo mkuu wa kiteknolojia” wa leo unazua maswali mazito kuhusu “mahali pa wanadamu na matendo ya kibinadamu ulimwenguni” (Rej. Laudato si', 101). Hakika moja ya vipengele vinavyohusika zaidi vya dhana hii, pamoja na athari zake mbaya kwa ikolojia ya binadamu na asilia sawa, ni ulaghai wake wa hila wa roho ya mwanadamu, kuwashawishi watu na hasa vijana katika kutumia uhuru wao vibaya.
Tunaona hili wakati wanaume na wanawake wanahimizwa kudhibiti, badala ya malezi yanayowajibika ya nyenzo au vitu vya kiuchumi, maliasili ya nyumba yetu ya kawaida, au hata mtu mwingine. “Upinzani kama huo, ambao hatimaye huathiri vibaya zaidi walio maskini zaidi na walio hatarini zaidi katika jamii, unaweza kufanyika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kupitia chaguzi za kila siku ambazo zinaweza kuonekana kuwa zisizoegemea upande wowote lakini kiukweli ni maamuzi kuhusu aina ya jamii tunayotaka kujenga”(Laudto si 107)
Unapotafuta kujibu la swali hili na changamoto zake nyingi zinazohusiana, kwa kukuza mafundisho ya kijamii ya Kikatoliki,hasa kiini cha thamani na utu wa kila mwanadamu, Baba Mtakatifu amependa kupendekeza kwamba muundo wenyewe wa shirika lao wanaweza kutoa marejeo muhimu, kwa kuwa wao ni mtandao wa kimataifa, na unaelezea lengo lao: “kama kutafuta kuunganisha katika ushirika kizazi kipya cha viongozi wa Kikristo wenye ujasiri”. Lengo la mtandao wowote ni kuunganisha watu, kuwasaidia kutambua kwamba wao ni sehemu ya kitu kikubwa kuliko wao wenyewe. Hakika, hilo ndilo lengo lililotajwa katika majukwaa mengi ya mitandao ya kijamii, na hakika mengi mazuri hufanyika kupitia njia hizi za mawasiliano. Hata hivyo, amesema Papa kuwa: “tunapaswa pia kuwa waangalifu, kwa maana cha kusikitisha ni kwamba mielekeo mingi ya ubinadamu inayotokana na tekinolojia inapatikana kwenye vyombo hivi vya habari, kama vile uenezaji wa habari za uwongo kimakusudi, kukuza chuki na migawanyiko, na kupunguzwa kwa uhusiano wa kibinadamu kuwa kanuni tu, na sio kutaja hisia ya uwongo ya ushiriki, hasa kati ya vijana, ambayo inaweza kusababisha kutengwa na upweke.”
Baba Mtakatifu Francisko akiendelea na hotuba yake kwa Mtandao huo wa wanasheria Katoliki amesema “Matumizi mabaya haya ya kukutana mtandaoni yanaweza kushindwa tu na utamaduni wa kukutana kihalisi, ambao unahusisha mwito mkali wa kuheshimiana na kusikilizana, ikiwa ni pamoja na wale ambao tunaweza kutokubaliana nao vikali. Hapa pia mtandao wao unaweza kutoa mfano, kwa kuwa unatafuta kuwavuta watu kutoka ulimwenguni kote ili wakutane kwa njia hii ya kweli. Hata hivyo mitandao si tu kuhusu kukusanya watu pamoja; pia ni kwa ajili ya kuwawezesha kushirikiana katika kufikia lengo moja.” Papa ameongeza: Tunaweza kufikiria wanafunzi wa kwanza, walioitwa na Yesu kufanya kazi pamoja katika kutupa nyavu zao ili kupata samaki wengi (rej. Lk 5:1-11); nyavu ambazo tunaweza kuzielezea kama zana za kutumika kwa njia ya pamoja kwa ajili ya malengo ya pamoja.
Mambo haya mawili muhimu ya kuunganisha watu na mwisho wa pamoja ni sifa ya kazi yao na kuakisi kwa usahihi asili ya Kanisa lenyewe, Watu wa Mungu walioitwa kuishi katika ushirika na utume. Nguvu hizo za kitovu (centripetal na centrifugal) za maisha ya Kikristo, zikidumishwa na nguvu za Roho Mtakatifu, huwafunga watu ndani katika umoja wa kidugu na kuwaelekeza nje kwenye utume wa pamoja wa kutangaza Injili kwa furaha. Mtandao halisi wa Kikristo, basi, tayari ni jibu la mienendo ya kudhalilisha utu" kwa kuwa hauelekezi tu ukweli wa ukombozi kuhusu kuwepo kwa mwanadamu, lakini unatafuta kuwaiga katika utekelezaji wa shughuli yake yenyewe. Kwa hivyo, kwa kubaki kuwa mtandao wa Kikatoliki wa kimataifa wa kweli, utaonesha kwa hakika njia mbadala ya dhuluma hiyo ya kiteknolojia ambayo inawavuta kaka na dada zetu katika kukamata vitu vibichi vya asili na asili ya mwanadamu, na kupunguza uwezo wao wa kufanya maamuzi au kuishi maisha ya uhuru wa kweli. (rej Laudato Si', 108).
Papa Francisko anaomba kwamba Roho Mtakatifu awatie msukumo na kuongoza juhudi zao za kuunda kizazi kipya cha viongozi waaminifu wa Kikatoliki walioelimika na waliojitolea kuendeleza mafundisho ya kijamii na kimaadili ya Kanisa katika nyanja ya umma. Kwa njia hiyo, hakika watachangia katika ujenzi wa ufalme wa Mungu. Bikira Maria awalinde, na Mwenyezi Mungu abariki juhudi zao na kuzifanikisha. Hatimaye Baba Mtakatifu amewaomba wasisahau kusali kwa ajili yake.