Papa:kwa mfano wa Kateri Tekakwitha,tumeutwa wote katika utakatifu!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu amebainisha kwamba ni mwendelezo wa dhamira ya ari ya kitume na shauku ya kutangaza Injili, ambapo alipenda kumtazama Mtakatifu Kateri Tekakwitha, mwanamke wa kwanza mzaliwa wa Amerika Kaskazini kutangazwa kuwa mtakatifu. Alizaliwa yapata mwaka wa 1656 katika kijiji kimoja kaskazini mwa New York, na alikuwa binti wa chifu wa Mohawk ambaye hakuwa amebatizwa na mama Mkristo wa Algonquian, ambaye alimfundisha Kateri kusali na kumwimbia Mungu nyimbo. Wengi wetu pia tulitambulishwa kwa Bwana kwa mara ya kwanza katika mazingira ya familia, hasa na mama na nyanya zetu. “Hivi ndivyo uinjilishaji unavyoanza na kwa hakika, tusisahau hili, kwamba imani siku zote hupitishwa kwa na akina mama na bibi. Imani lazima isambazwe kwa kilugha na tuliipokea kwa kilugha hii kutoka kwa akina mama na bibi. Uinjilishaji mara nyingi huanza hivi: kwa ishara rahisi, ndogo, kama vile wazazi wanaosaidia watoto wao kujifunza kuzungumza na Mungu katika sala na wanaowaambia juu ya upendo wake mkuu na wa huruma. Na misingi ya imani kwa Kateri, na mara nyingi kwetu pia, iliwekwa kwa njia hii. Alikuwa ameipokea kutoka kwa mama yake kwa kilugha, ma kilugha cha imani.
Kateri alipokuwa na umri wa miaka minne, janga kubwa la ndui lilikumba watu wake. Wazazi wake na kaka mdogo walikufa, na Kateri mwenyewe aliachwa na makovu usoni na shida ya kuona. Kuanzia wakati huo Kateri alilazimika kukumbana na matatizo mengi: hakika yale ya kimwili kutokana na athari za ndui, lakini pia kutokuelewana, mateso na hata vitisho vya kifo alichopata kufuatia Ubatizo wake Dominika ya Pasaka mnamo 1676. Haya yote yalimpatia Kateri upendo mkuu kwa msalaba, ishara dhahiri ya upendo wa Kristo, ambaye alijitoa hadi mwisho kwa ajili yetu. Kwa hakika, ushuhuda wa Injili sio tu kuhusu yale yanayopendeza; lazima pia tujue jinsi ya kubeba misalaba yetu ya kila siku kwa uvumilivu, uaminifu na matumaini. “Uvumilivu, katika uso wa magumu, wa misalaba: subira ni sifa kuu ya Kikristo.
Yeyote asiye na subira si Mkristo mzuri. Uvumilivu wa kuvumilia yaani kuvumilia magumu na pia kuvumilia wengine, ambao wakati mwingine wanakuchosha au kukupatia magumu… Maisha ya Kateri Tekakwitha yanatuonesha kwamba kila changamoto inaweza kushinda ikiwa tutafungua mioyo yetu kwa Yesu, ambaye hutupatia neema tunayohitaji: subira na moyo ulio wazi kwa Yesu, hiki ni kichocheo cha kuishi vizuri. Baada ya kubatizwa, Kateri alilazimika kukimbilia kati ya Mohawk kwenye Utume wa Kijesuit karibu na jiji la Montreal. Huko alihudhuria Misa kila asubuhi, akitoa wakati wake kwa kuabudu mbele ya Sakramenti Takatifu, akisali Rozari, na kuishi maisha ya kitubio. Mazoea haya ya kiroho yalimvutia kila mtu kwenye Utume huo, walitambua kwake Kateri utakatifu uliovutia kwa sababu ulizaliwa na upendo wake wa kina kwa Mungu. Inafaa kwa utakatifu kuvutia.
Baba Mtakatifu amekazia kusema kuwa Mungu anatuita kwa mvuto, anatuita kwa hamu hii ya kuwa karibu nasi na alihisi neema hiyo ya mvuto wa kimungu. Sambamba na hayo, aliwafundisha watoto wa Utume kusali na kwa njia ya utekelezaji wa mara kwa mara wa majukumu yake, ikiwa ni pamoja na kuwatunza wagonjwa na wazee, akawa kielelezo cha utumishi wa unyenyekevu na upendo kwa Mungu na jirani. Imani daima huoneshwa katika huduma. Imani si kujitengenezea nafsi, hapana; ni kutumikia. Ingawa alihimizwa kuolewa, badala yake Kateri alitaka kuweka maisha yake wakfu kabisa kwa Kristo. Kwa kuwa hakuweza kuingia katika maisha ya kuwekwa wakfu, aliweka nadhiri ya ubikira wa milele mnamo tarehe 25 Machi 1679. Uchaguzi wake huu unafunua kipengele kingine cha bidii yake ya kitume: kujitolea kamili kwa Bwana. Bila shaka, si kila mtu ameitwa kufanya nadhiri sawa na Kateri; hata hivyo, kila Mkristo anaitwa kila siku kujitoa kwa moyo usiogawanyika katika wito na utume aliokabidhiwa na Mungu, akimtumikia yeye na jirani yake katika roho ya mapendo.
Baba Mtakatifu aidha amesema kwamba, maisha ya Kateri ni ushuhuda zaidi wa ukweli kwamba bidii ya kitume ina maana ya umoja na Yesu, unaolishwa kwa sala na sakramenti, na hamu ya kueneza uzuri wa ujumbe wa Kikristo kwa uaminifu kwa wito fulani. Maneno ya mwisho ya Kateri ni mazuri. Kabla ya kufa alisema: “Yesu, nakupenda.” Kwa hiyo, sisi pia, tukipata nguvu kutoka kwa Bwana, kama vile Mtakatifu Kateri Tekakwitha alivyofanya, tunajifunza kutenda matendo ya kawaida kwa namna isiyo ya kawaida na hivyo kukua kila siku katika imani, mapendo na ushuhuda wa bidii kwa Kristo. “Tusisahau: kila mmoja wetu ameitwa katika utakatifu, kwa utakatifu wa kila siku, kwa utakatifu wa maisha ya kawaida ya Kikristo. Kila mmoja wetu ana wito huu: tuendelee kwenye njia hii. Bwana hatakosekana”, Papa amehitimisha tafakari yake.