Papa Francisko kwa vijana wa WYD:Upendo wa Mungu ni kituo cha kuanza maisha
Na Angrella Rwezaula, - Vatican.
Karibu, karibu na asante kwa kuwa hapa, nimefurahi kuwaona! Ninafurahi kusikiliza kelele nzuri mnayopiga na kuruhusu furaha yenu iniambukize. Ni vizuri kuwa pamoja Lisbon: mmeitwa hapa na mimi, na Patriaki, ambaye ninamshukuru kwa maneno yake, na Maaskofu, mapadre, makatekista na wahuishaji wenu. Tunawashukuru wale wote waliowaita na wale wote waliofanya kazi ili kufanikisha mkutano huu, na tunafanya hivyo kwa kuwapigia makofi mengi! Lakini zaidi ya yote ni Yesu aliyewaita: hebu tumshukuru Yesu kwa mzunguko mwingi na mkubwa wa makofi! Ndivyo Baba Mtakatifu Francisko alivyoanza kuzungumza na moyo wa kila msichana na mvulana waliofika Lisbon katika Siku ya Vijana Duniani. Amekutana nao jioni tarehe 3 Agosti 2023 katika Bustani ya Eduardo VII, eneo kubwa la kijani kibichi lililo katikati mwa jiji la Lisbon ambapo vijana takriban 500,000 waliohudhuria.
Baada ya hotuba ya salamu ya Patriaki wa Lisbon, Kardinali Manuel José Macário do Nascimento Clemente, walikuwa ni vijana wenyewe wahusika wakuu wa sehemu ya kwanza ya wakati huo kwa maonesho ya muziki, nyimbo na tamasha wakiwasilisha barua kwa Papa Fransisko ya maswali yao mengi juu ya maisha, juu ya imani na kuwa wa Kanisa, huku wakipeperusha bendera za nchi zote za ulimwengu wanazotoka na wakiwa wamebeba alama za Siku ya vijana Duninia (WYD) jukwaani ambao ni Msalaba wa Hija na Picha ya Madonna Salus Populi Romani, yaani Mama Afya ya Watu wa Roma. Baba Mtakatifu akiendelea na hotuba yake amesema: “Hamko hapa kwa bahati mbaya. Bwana amewaita, si katika siku hizi tu, bali tangu mwanzo wa siku zenu.
Papa Francisko amekazia kusema kuwa Bwana alituita sisi sote tangu mwanzo wa maisha yetu. Ndiyo, amewaita ninyi kwa jina: tumesikia kutoka katika Neno la Mungu kwamba ametuita kwa jina. Jaribuni kufikiria maneno haya matatu yaliyoandikwa kwa herufi kubwa; kisha mfikirie ya kuwa yameandikwa ndani ya kila mmoja wenu, mioyoni mwenu, kana kwamba yanaunda cheo cha maisha yenu, maana ya kile mlicho yaani “Ninyi mnaitwa kwa jina, sisi sote tulio hapa, mimi, sisi na wote wameitwa kwa jina la kila mmoja. Hatukuitwa kiautomatiki; tuliitwa kwa majina. Hebu tufikirie hilo. Yesu aliniita kwa jina langu," Papa Francisko amekazia kusema.
Ni maneno yaliyoandikwa moyoni, Papa amengeza kusema kisha tufikiri kwamba yameandikwa ndani ya kila mmoja wetu, katika mioyo yetu, na kuunda aina ya jina la maisha yenu, maana ya sisi ni nani, maana ya wewe ni nani na umeitwa kwa jina. Hakuna hata mmoja wetu aliye Mkristo kwa bahati tu kwa sababu sote tumeitwa kwa jina. Mwanzoni mwa njama ya maisha, kabla ya talanta tuliyo nayo, vivuli na majeraha tunayobeba ndani, tuliitwa. Tumeitwa, kwa nini? Tumeitwa kwa sababu tunapendwa. Ni vizuri. Machoni pa Mungu sisi ni watoto wa thamani, ambao Yeye huwaita kila siku kuwakumbatia na kuwatia moyo; ili kumfanya kila mmoja wetu kuwa Kito cha kipekee na cha asili. Kwa hiyo kila mmoja wetu ni wa kipekee, asili na uzuri wa haya yote tunaweza kuyagundua tu kwa mbali. Baba Mtakatifu Francisko amekazia kusema, katika Siku hii ya Vijana Duniani, tusaidiane kutambua ukweli huu. Kwa hiyo siku hizi ziwe ni mwangwi mahiri wa wito wa upendo wa Mungu, kwa sababu sisi ni wa thamani machoni pa Mungu, licha ya yale ambayo macho yetu yanaona ukungu na wakati mwingine hasi na kushangazwa na vikengeushi vingi. Labda ziwe siku ambazo jina lako, kupitia kaka na dada wa lugha na mataifa mengi tunaona bendera nyingi zikilitamka kwa urafiki, kama habari za kipekee katika historia, kwa sababu mapigo ya moyo wa Mungu ni ya kipekee kwako.
Papa akiendelea na ushauri kwa vijana hawa amewaomba kuwa: “Na hizi ziwe siku za kuweka ndani ya mioyo yetu kwamba tunapendwa kama tunavyopenda kuwa, na sio kama tungependa kuwa, yaani kama tulivyo sasa. Huu ndio mwanzo wa Siku ya Vijana (WYD) lakini zaidi maisha yote. Papa amewauliza vijana: Je tunapendwa kama tulivyo, bila mapambo. Je, mmeelewa hili?” Kwa hiyo kuitwa kwa jina la kila mmoja wetu, sio njia ya kuzungumza bali ni Neno la Mungu (Rej. Isa 43, 1; 2 Tim 1,9). Papa ameongeza kusema: “ikiwa Mungu anakuita kwa jina ina maana kwamba kwa Mungu hakuna hata mmoja wetu aliye idadi ya namba, bali ni uso na moyo.
Papa Francisko aidha amesema "Ningependa kila mmoja wenu atambue jambo moja kwani wengi, leo, hii wanajua jina lako, lakini hawakuiti kwa jina". Na hii kiukweli, jina lako linajulikana, linaonekana kwenye mitandao ya kijamii, linashughulikiwa na (mifumo ya mitandao) ambayo inahusisha ladha na upendeleo. Walakini, haya yote hayahoji upekee wako, japokuwa manufaa yako kwa ajili ya utafiti wa soko. Ni mbwa mwitu wangapi hujificha nyuma ya tabasamu la wema wa uwongo, huku wakisema wanakujua wewe ni nani lakini hawakupendi, wakisingizia kwamba wanakuamini na kukuahidi kuwa utakuwa mtu fulani na kukuacha peke yako wakati hufai tena?
Huo ndio udanganyifu wa mtandaoni, Papa ametoa angalisho kwamba lazima tuwe makini ili tusidanganywe kwa sababu ukweli mwingi ambao hutuvutia na kuahidi furaha, basi hujidhihirisha kwa jinsi ulivyo, katika vitu visivyo na maana, kama povu la sabuni, vitu vya kupita kiasi, vitu visivyo na maana ambavyo hutuacha sisi watupu wa ndani. Kwa hiyo Papa amewambia vijana jambo moja kuwa: “Yesu hayuko hivi: Anawaamini ninyi, anawaamini kila mmoja wenu, kila mmoja wetu kwa sababu kwa Yesu kila mmoja wetu ni muhimu, kila mmoja wenu ni wa muhimu. Huyo ni Yesu...” Na kwa hiyo sisi, Kanisa lake ni jumuiya ya walioitwa na hivyo sisi, sio jumuiya ya walio bora zaidi, la! sisi sote ni wenye dhambi lakini tumeitwa, jinsi tulivyo. Hebu tufikirie kidogo kuhusu hili, mioyoni mwetu kwamba tunaitwa jinsi tulivyo, na matatizo tuliyo nayo, mapungufu tuliyo nayo, kwa furaha yetu kubwa na shauku yetu ya kuwa bora na hamu yetu ya kushinda. Tunaitwa kama tulivyo, Papa amerudia tena. Tufikirie hivyo kidogo. Yesu ananiita jinsi nilivyo, si kama ningependa kuwa. Sisi ni jumuiya ya kaka na dada zake Yesu, wana na binti wa Baba mmoja.
Kwa kutaka kufafanua wazi zaidi, Baba Mtakatifu amesema: “Marafiki, ningependa kuwa wazi na ninyi, ambao mna alegi ya uongo na maneno tupu. Katika Kanisa kuna nafasi kwa kila mtu, Papa amerudia - hakuna mtu asiye na maana, kuna nafasi kwa kila mtu. Kama tulivyo sisi sote. Na hili Yesu anasema waziwazi anapowatuma mitume kuwaalika kwenye karamu ya mtu aliyemwandalia, alisema: “Nendeni mkawalete watu wote, vijana kwa wazee, wenye afya na wagonjwa, wenye haki na wenye dhambi; wote,” Papa amerudia mara kadhaa neno 'wote'. Na Kanisa ni mahali pa kila mtu. Kwa mfano amesema mwingine anaweza kusema: “Padre, lakini mimi nina bahati mbaya: kuna nafasi kwa ajili yangu”. Amejibu “kuna nafasi kwa kila mtu pamoja, kila mtu na lugha yake mwenyewe na kila mmoja kwa lugha yake. Kwa hiyo Papa ameomba warudie neno: “Wote, wote, wote” [wamerudia…] Sijasikia: bado! Kila mtu, kila mtu, kila mtu! Na hili ndilo Kanisa, Mama wa wote: kuna nafasi kwa kila mtu”.
“Bwana haoneshi kwa kidole chake, bali hufungua mikono yake. Inashangaza: Bwana hajui jinsi ya kunyosha kidole chake, lakini anajua jinsi ya kukumbatia, anatukumbatia sisi sote. Yesu anatuonesha pale msalabani, ambaye alifungua mikono yake kiasi cha kusulubiwa na kufa kwa ajili yetu. Yesu kamwe hafungi mlango, lakini anakualika uingie yaani uingie na utazame. Yesu anapokea, Yesu anakaribisha. Katika siku hizi kila mmoja wetu aeneze lugha ya upendo wa Yesu kwamba Mungu anakupenda, Mungu anakuita. Ni kwa jinsi gani ilivyo vizuri. Mungu ananipenda, Mungu ananiita, na anataka niwe karibu naye”.
Baba Mtakatifu aidha amewambia vijana kuwa: “Usiku wa leo mmeniuliza maswali mengi. Msichoke kuuliza maswali; Kuuliza maswali ni sawa na kiukweli mara nyingi ni bora kuliko kutoa majibu, kwa sababu yeyote anayeuliza anabaki asiyetulia na kutotulia ni dawa bora ya mazoea, kwa hali hiyo ya kawaida ambayo inatia moyo. Kila mmoja wetu ana mahangaiko yake ndani yetu. Tunabeba mahangaiko haya pamoja nasi na tunayabeba katika mazungumzo yetu, tunayabeba pamoja nasi tunapoomba mbele za Mungu, maswali haya ambayo kwa uzima huwa majibu, ambayo inatubidi kuyangojea tu.
Kuna jambo la kuvutia sana. "Mungu anapenda kwa mshangao, hajapanga na upendo wa Mungu ni mshangao. Anashangaza kila wakati, wakati hatujawa makini na kutushangaza. Kwa hiyo Papa amewaalika wafikirie jambo hilo zuri sana, kwamba Mungu anatupenda, Mungu anatupenda jinsi tulivyo, si vile ambavyo tungependa kuwa au jinsi jamii inavyotaka tuwe yaani jinsi tulivyo. Anatupenda kwa kasoro tulizo nazo, kwa mapungufu tuliyo nayo na kwa nia tuliyo nayo ya kusonga mbele kimaisha. Hivi ndivyo Mungu anatuita." Muwe na matumaini kwa sababu Mungu ni baba na yeye ni baba anayetupenda. Hii si rahisi sana na kwa hili tuna msaada mkubwa wa Mama wa Bwana. Yeye pia ni Mama yetu. Na ndiyo tu Papa alitaka kuwambia kwamba wasiogope kuwa na ujasiri, wa kwenda mbele kwa kujua kwamba tunalindwa na upendo wa Mungu. Kwa kuhitimisha Papa Francisko amesema “Mungu anatupenda" na kuwaomba warudie sentensi hiyo, kwa nguvu ili isikike. Na wote walirudia na akawashukuru na kusema Ciao!