Papa amkumbuka Padre Puglisi na kuwashauri Mapadre wawe wajasiri katika utumishi wao
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 20 Agosti 2023, amemtumia barua Askofu Mkuu Corrado Lorefice wa Jimbo Kuu la Palermo, Italia, katika fursa ya kumbukumbu ya miaka 30 ya kifo cha Padre Pino Puglisi, ambaye alitangazwakuwa mwenyeheri mnamo tarehe 25 Mei 2013 ambaye aliuawa na kikundi cha kihalifu cha mafia. Baba Mtakatifu katika barua hiyo anasema imepita miaka 30 tangu usiku ule wa tarehe 15 Septemba 1993 ambapo mpendwa Padre Pino Puglisi, kuhani mwema na shuhuda wa huruma ya Baba alipohitimisha maisha yake hapa duniani hasa katika eneo lile ambalo alikuwa ameamua kuwapo kama mhudumu wa amani, akipanda mbegu ya Neno ambalo linaokoa, na ambaye alitangaza upendo na msamaha katika eneo kwa wengi "lililokavu na lenye miamba”, lakini hapo Bwana alifanya kukua pamoja na ngano nzuri na magugu mabaya (Mt 13, 24-30). Baba Mtakatifu kwa hiyo anatamani kuungana nao kiroho katika tukio hilo lenye maana na kumshukuru Mungu kwa kila faraja, kwa ajili ya zawadi ya mwenyeheri shahidi Padre Pino Puglisi, na mchangaji mpendwa wa Kanisa la Parelmo na kwa Sicilia yote.
Kufuata mfano wa Yesu
Baba Mtakatifu anabainisha kuwa ilikuwa ni siku yake ya kuzaliwa ambapo Padre Pino aliuawa mtaani, na hasa mitaa ya wilaya ya Brancaccio, ambayo ilikuwa Kanisa la shamba ambalo alilitumikia kwa sadaka na safari wakati wa huduma yake ya kichungaji kukutana na watu katika nchi inayojulikana naye na ambayo hakuchoka kutunza na kumwagilia maji yenye kuzaliwa upya wa Injili. Kwa sababu yeye alitaka kila mtu aweze kukata kiu yake na kufurahia burudisho la nafsi ili kukabiliana na ukali wa maisha ambayo hayajawa na huruma sikuzote. Papa Francisko anabainisha kuwa, kwa kufuata mfano wa Yesu, Padre Pino alikwenda mbali sana katika upendo, na ambaye alikuwa na tabia sawa na mchungaji mwema, mpole na mnyenyekevu, na alijua mmoja baada ya mwingine wa vijana aliojaribu kuwanyakua mitaani na ulimwengu wa chini.
Padre Pino alikuwa shuhuda wa Mungu kuwapenda wadogo
Yeye ni ushuhuda wa mtu wa Mungu ambaye aliwapenda wadogo na wasio na ulinzi, aliwaelimisha kwa uhuru, kupenda maisha na kuyaheshimu. Kwa kujitolea bila kuchoka kwa ulinzi wa familia, wa watoto wengi waliopangwa mapema sana kuwa watu wazima na kuhukumiwa kuteseka, akiwasiliana nao kuwafundisha maadili ya kuishi kwa heshima zaidi. Na Padre huyo wa Palermo, hakukoma, alijitoa kwa upendo kwa kuukumbatia Msalaba hadi kumwaga damu. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu Fransisko amewaomba wachungaji wa Sicilia wasiishie mbele ya majeraha mengi ya kibinadamu na kijamii ya leo hii, ili waponywe kwa mafuta ya faraja na huruma. Chaguo la upendeleo kwa maskini ni la dharura anasema Papa; ni nyuso zinazotuuliza maswali na kutuongoza kuelekea unabii na kwamba vijana wanaomba kuwa utambuzi wa sinodi kuanza huduma mpya ya kichungaji ambayo inalingana kikamilifu na mahitaji ya leo.
Kuwa na ishara na kutafuta lugha sahihi ya huruma ya Mungu
Kwa hiyo Baba Mtakatifu amewasihi mapadre waweze kuleta uzuri na tofauti ya Injili huku wakifanya ishara na kutafuta lugha sahihi ili kuonesha huruma ya Mungu, haki yake na huruma yake. Ishara zote ni muhimu ili kujenga ubinadamu mpya. Na akikumbuka hekima ya vitendo na vya kina vya Padre Pino, ambaye alipenda kusema: 'Ikiwa kila mmoja wetu atafanya jambo fulani, basi tunaweza kufanya mengi, Papa amewaalika kila mtu kujua jinsi ya kushinda hofu nyingi na upinzani binafsi na kushirikiana pamoja ili kujenga jamii yenye haki na kidugu. Padre Puglisi pia alipambana ili mtu yeyote asijisikie peke yake katika kukabiliana na changamoto ya uharibifu na nguvu zilizofichwa za uhalifu. Kwa hiyo Papa Francisko amesisitiza tena kuwa ni kuondoa kutengwa, kufungwa na ubinafsi wa siri ni silaha zenye nguvu za wale wanaotaka kuwaelekeza wengine kwa masilahi yao binafsi. Kwa kuweza kukabiliana na haya yote, jibu ni ushirika, kutembea pamoja, kujisikia kama mwili na viungo vilivyounganishwa na kichwa. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu amewahimiza mapadre kuishi kwa umoja katika Kristo, kwanza kabisa ndani ya baraza la kikuhani pamoja na askofu wao na kati kati yao.
Uongofu wa ndani ili kuwa tayari kuhudumia ndugu
Hatimaye, Baba Mtakatifu Fransisko katika barua hiyo amewaomba mapadre wote, ambao kila siku wanapaswa kukabiliana na majukumu ya huduma ya kipadre katika kuwasiliana na hali halisi ya eneo, kuwa siku zote na kila mahali taswira ya kweli ya Mchungaji Mwema anayekaribisha, kuwa na ujasiri na kuthubutu bila woga na kuweka tumaini hasa kwa walio dhaifu, wagonjwa, wanaoteseka, wahamiaji na wale ambao wameanguka na wanataka kusaidiwa kuamka tena. Halafu vijana wao ndiyo wawe katikati ya wasiwasi wao ambao ndilo tumaini la siku zijazo. Kadhalika Papa amekumbusha tena juu Mapadre kuhusu tabasamu kubwa la Padre Pino Puglisi kwamba: “Watiwe moyo kuwa wanafunzi wenye furaha na wenye kuthubutu, wanaopatikana zaidi ya yote kwa ajili ya uongofu wa ndani wa kila mara unaowafanya kuwa tayari zaidi kuwahudumia kaka na dada zao na waaminifu kwa ahadi za kipadre na wanyenyekevu katika kutii Kanisa.