Papa atuma matashi mema kwa Sinodi ya Wavaldesi huko Torre-Pellice
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wake kupitia telegramu iliyotiwa saini na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, tarehe 21 Agosti 2023 ambayo imeelekezwa kwa Askofu Derio Olivero, wa Jimbo la Pinerolo (Torino) katika fursa ya wale wanaohusika katika Sinodi ya Makanisa ya Wamethodist - Waldensia inayoendelea huko Torre Pellice Torino, Italia ambayo ilianza tarehe 20 Agosti na itamalizika tarehe 25 Agosti 2023. Katika telegram hiyo, Kardinali Parolin anabainisha kuwa, Papa atuma salamu zake njema kwa washiriki wa Sinodi ya Makanisa ya Methodist - Waldensia "ili katika siku za mkutano ziwe fursa kwa kila mtu kwa uzoefu wa kina wa Kristo ambaye anakaribisha, anaongoza kwa utimilifu wa ushirika naye na pamoja na ndugu zake.”
Katika fursa hiyo ujumbe unaandikwa kuwa "Baba Mtakatifu anapoinua sala ya sifa kwa Mungu kwa karama zinazotolewa kwa njia ya mazungumzo ya kiekumeni, pamoja na ushirikiano wa maelewano kati ya Makanisa, anapenda kuungana kiroho katika tukio hilo muhimu ili tuweze kukua katika ujuzi wa kuvumiliana, kuwa shuhudia pamoja katika Injili ya Yesu.” Katika hisia hizo aidha, Baba Mtakatifu anawatakia matashi mema ya kazi za sinodi yao na kuwaombea Baraka za Bwana.
Hata hivyo hili ni tukio la kiutamaduni la kila mwaka ambalo hufanyika katika mabonde ya Waaldensia na huwaleta pamoja wajumbe 180 kutoka Italia yote, takriban wageni 30 wa kimataifa na wawakilishi wa kiekumeni ambao hubadilishana mawazo katika siku za mkutano. Kwa hiyo Sinodi inawakilisha baraza kuu la kufanya maamuzi na kusanyiko la kidemokrasia la Makanisa haya ya Kiprotestanti nchini Italia. Mada kuu la toleo la mwaka 2023 ni “Kujitolea kwa Kanisa katika jamii, imani, maadili.”
Mpango huo vile vile unajumuisha ibada ya ufunguzi, rasimi ambayo hufanyika kwa kawaida jioni kwa umma na katika muktadha huo (Jumatatu 21 Agosti 2023 katika hekalu la Waldensia la Torre Pellice), na ibada hiyo kwa mwaka 2023 iinaongozwa na mada: "Ukandamizaji, ujasiri, mabadiliko: wanawake katika nafasi ya umma”, lakini pia ni kabla ya Sinodi ya wanawake na Sinodi ya awali ya Shirikisho la Vijana wa Kiinjili nchini Italia (FGEI). Uteuzi mwingine muhimu unakaribia kukamilika wa 2024 ambao unaashiria hatua muhimu kwa Waaldensia, ambao watasherehekea kumbukumbu ya miaka 850 ya kuzaliwa kwa Harakati la Pietro Valdo huko Lyon nchini Ufaransa. Sinodi hiyo itaainisha hata kazi za mwaka 2024.