Papa amesalimiana na vijana 15 wa Ukraine huko Lisbon katika sala
Vatican News
Kabla ya kuondoka kwenye Ubalozi wa Vatican mjini Lisbon asubuhi ya Alhamisi tarehe 3 Agosti, 2023 Baba Mtakatifu Francisko alikutana na kundi la vijana kumi na watano mahujaji kutoka Ukraine wakiasindikizwa na Denys Kolada, mshauri wa mazungumzo na mashirika ya kidini katika serikali ya Ukraine. Hili lilitangazwa na Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Vatican, ikiripoti kwamba baada ya kusikiliza “historia zenye kugusa moyo” za vijana hao, Papa alizungumza maneno machache, “akidhihirisha ukaribu wake ‘wa uchungu na wa maombi.” Mkutano huo ulichukua takriban dakika 30; hatimaye, Papa Fransisko na vijana hao walisali sala ya Baba Yetu pamoja, na mawazo yaligeukia nchi ya Ukraine inayoteswa.
Katika asubuhi hiyo pia, katika Ibada ya Misa ambayo Papa aliadhimisha katika Ubalozi wa Vatican nchini Ureno, kulikuwa na mkutano mwingine muhimu wa wanafamilia wanne wa mwanamke wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 62, mchoraji wa michoro ya katekesi, ambaye alikuja Lisbon kwa ajili ya Siku ya Vijana duniani WYD na ambaye alifariki hivi karibuni kutokana na ajali katika nyumba aliyokuwa amekaribishwa.