Papa,Mt.Monica:Tuwaombee wamama wanaotazama watoto wakipoteza njia!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika 27 Agosti 2023 akiwageukia waamini na mahujaji waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro, pamoja na miito mbali mbali na salamu, amekumbusha siku ya Mtakatifu Monica.Baba Mtakatifu amesema: “Leo tunamkumbuka Mtakatifu Monica, mama wa Mtakatifu Agostino: kwa sala na machozi yake alimwomba Bwana kwa ajili ya uongofu wa mwanawe. Mwanamke mwenye nguvu, mwanamke mzuri: tuwaombee akina mama wengi wanaoteseka wakati watoto wao wamepotea kidogo au wako kwenye njia ngumu za maisha.”
Kila tarehe 27 Agosti ya kila mwaka Mama Kanisa anamkumbuka Mtakatifu Monica aliyezaliwa huko Tagaste nchini Algeria mnamo mwaka 332 na kifo chake kikatokea huko Ostia, eneo la Roma, Italia mnamo mwaka 387. Kwa njia hiyo alikuwa ni mwanamke mwafrika wa kabila la Waberberi na mke wa Patriki, afisa wa Dola ya Warumi. Mama Monica ni maarufu katika historia yake hasa kutokana na sifa zilizotajwa na mwanae Agostino wa Hippo katika kitabu chake maarufu cha Maungamo na anaheshimiwa na madhehebu mbalimbali ya kikristo kama mtakatifu, hasa katika tarehe 27 Agosti au tarehe 4 Mei kwa Makanisa mengine.
Tukirudi nyuma ya historia yake katika sehemu za magharibi za Afrika ya Kaskazini wenyeji walikuwa Waberberi kama Mtakatifu Monica, lakini watu wa mjini, kama mme wake, na wenye mashamba makubwa walikuwa wa asili ya Ulaya wakitumia hasa lugha ya Kilatini. Kwa ujumla sehemu hiyo ya Afrika ilikuwa karibu na utamaduni wa Ulaya ya Magharibi. Mama Monika, anayeheshimiwa mtakatifu alikuwa Mkristo na kumbe mme wake Patrik alifuata dini ya jadi ya kuabudu miungu mingi kabla hajabatizwa mwishoni mwa maisha yake. Historia ya Patriki inalezwa kuwa kwa hakuwa mkristo pia alikuwa na tabia ya wepesi wa kukasirika. Mama Monika alistahimili kwa upole alipogombezwa na mumewe na kuvumilia tu akimkabidhi Mungu katika maombi yake.
Mama Monica alizaa watoto watatu, Agostino anayeandika Historia yake baadaye, Naviji, na mwingine wa kike, ambaye hatujui jina lake, ila inasemekana kwamba baada ya kufiwa mume wake Monica akawa mmonaki. Watoto hawa Monica aliwafundisha kumpenda Bwana wetu Yesu na kulitaja jina lake kwa heshima. Hata mume wake Patriki kwa njia hiyo alipata kuongoka akawa mkristo kwa sababu ya mwenendo safi wa Mama Monika. Na kwa njia hiyo tabia hii ya Mama Monika ilimpekea na kumuambukiza sana mtoto wake Agostino na kumpeleka katika imani ya Kikristo. Agostino kwa hiyo aliweza kuandika kwamba alipokuwa ananyonya maziwa ya mama, alifyonza pia upendo kwa jina la Yesu. Akiwa mtoto alipokea chumvi kama ishara ya kuingia ukatekumeni akabaki daima anavutiwa na Yesu, hata alipozidi kusogea mbali na Kanisa lake.
Agostino alikwenda kukaa Kartago(Tunisia) ili asome shule, akaendelea katika maarifa yote, lakini alizidi kufanya uashereti na mambo yote yasiyofaa. Alimsikitisha sana mama yake. Kwa hiyo mama Monika alimwendea Askofu mmoja huko akamuulizia: Je Itakuwaje na mwanangu? Naye askofu akamjibu “Usiogope mama, mtoto huyu wa machozi mengi hivi hawezi kupotea”. Kweli Mama Monika hakumwomba Mungu bure, maana Augustino aliongoka, akabatizwa na Mtakatifu Ambrosi na hatimaye akawa mwalimu shujaa wa mafundisho ya Kanisa katoliki. Monika alipojiona yuko karibu kufa, aliwaambia wanawe kwamba: “Mnizike mpendavyo ila nawambeni kitu kimoja: Mnikumbuke kwenye altare ya Bwana”. Akafa huko Ostia nchini Italia mnamo mwaka 387.
Sala ya Mama Mkristo kwa Maombezi ya Mtakatifu Monica
Sala: Mtakatifu Monica, mwanamke na mama mwenye kuteseka, unajua machozi yangu, mahangaiko na uchungu wangu. Wakati fulani uliteseka kama mimi; ninaomba unionee huruma kwa mateso niliyonayo, Uniombee. Kutoka katika Roho Mtakatifu ulipokea zawadi ya ufahamu na busara, nguvu na sala. Uniombee ili nami nijaliwe zawadi zile zile. Kwa kuwa ulikuwa mpatanishi, daima uwaombee mume na watoto wangu na usali kwa ajili ya amani ya nyumba yetu. Kwa maombezi yako uliwaokoa mumeo na mwanao. Utuombee neema ya Mungu ili tuwe na imani katika nyumba yetu. Kutokana na kuhudhuria Misa kila siku uliweza kupata nguvu na faraja; basi utuombee nasi nguvu na faraja katika maisha yetu daima. Utuombee kwa ajili ya mahitaji yetu muhimu ya kidunia; kusudi tuweze kufanya kazi na kuwa na amani katika familia yetu. Uwakumbuke watoto wangu, ili daima wajue pendo la kweli na hivyo wamtumikie Mungu kwa mapendo safi. Uniombee, ili niwe mama mwema kwao, na mwisho wa maisha haya, mimi pamoja na mume wangu, watoto wangu na wapendwa wangu wote tuweze kufika kwa Mungu, huko ambako wewe upo pamoja na mume wako na watoto wako wote. Kwa njia ya Kristo, Bwana wetu. Amina. Mtakatifu Monika, Mlinzi wa wa akina mama Wakristo, Utuombee.
Mtakatifu Agostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Na tarehe 28 Agosti ya kila mwaka, Mama Kanisa anamkumbuka Mtakatifu Agostino mama yake Mtakatifu Monica. Katika siku hii, tukumbuke maneno yake muhimu katika kitabu chake cha maungamo kwani anakumbukwa sana katika suala la Dhambi na neema kwani katika suala la neema na dhambi ni Agostino aliyefundisha kwamba ubinadamu umerithi dhambi ya asili kutoka kwa Adamu. Uhuru wa asili umepotezwa na dhambi hiyo, na hali hii imerithiwa na watu wote baadaye. Lakini kwa neema yake Mungu hufunua upendo wake kwao. Alisisitiza kwamba si binadamu anayemtafuta Mungu, bali Mungu ndiye anayemhurumia mwanadamu mwenye dhambi. Utakaso unaopatikana kwa imani unasababisha ondoleo kamili la dhambi zote kabisa. Halafu mwamini anazidi kufanywa mpya kwa mchakato utakaokamilishwa na ufufuko wa siku ya mwisho. Mchakato huo wote ni kazi ya neema ya Mungu: bila hiyo, binadamu hawezi kuongoka, kukwepa dhambi na kufikia utimilifu wa wokovu. Hayo yote ni zawadi tu ya Mungu, kama vilivyo pia udumifu na stahili za mtu.
"Wewe ni Bwana Mkuu"
Sisitizo hilo la kwamba neema ni dezo, lilimuongoza Augustino kufundisha juu ya uteule, neema ambayo hakuna anayeweza kuikataa na ambayo inafikisha kwa hakika mbinguni. Kwa nini Mungu hawapi wote neema hiyo ni fumbo ambalo tuliinamie tu, kwa sababu hatuwezi kabisa kulielewa. Kwa vyovyote haiwezekani kumlaumu Mungu kwa ajili hiyo, eti si haki. Mawazo hayo yalikuja kukaziwa zaidi tena na watu kama Martin Luther, Yohane Kalvini na Janseni, namna iliyokataliwa na Kanisa Katoliki. Sala zake zimekuwa ni mwanga mkuu kwa kila mmoja mwenye kujikita katika hija ya Bwana kwa: Wewe Bwana ni mkuu na unastahili kabisa sifa. Uweza wake ni mkuu na hekima yako haina mipaka. Mtu anataka kukusifu, yeye aliye sehemu ndogo ya viumbe vyako vyote, yeye anayetembea akielekea kifo, ushahidi wa dhambi yake, wa kwamba wewe unapinga wenye kiburi. Hata hivyo mtu, sehemu ndogo ya viumbe vyako vyote, anataka kukusifu. Wewe unamchochea aonje furaha ya kukusifu, kwa kuwa umetuumba kwa ajili yako, na moyo wetu hautulii mpaka ustarehe ndani mwako.
Nijalie kusonga mbele ili kuwa mkamilifu
Ee upendo wenye kuwaka daima usiweze kuzimika kamwe, Mungu wangu uniwashe moto! Unijalie mimi, mimi pia, Bwana wangu mpenzi, nikujue, nikupende na kukufurahia. Nisipoweza kufanya hayo kikamilifu katika maisha haya, unijalie walau kusonga mbele kila siku hata niweze kufikia kuyafanya kwa ukamilifu. Acha nikufahamu zaidi na zaidi hata ukamilifu. Acha nikupende kila siku zaidi na zaidi hata ukamilifu; furaha yangu iwe kubwa kwa yenyewe, na kamili ndani yako. Wewe ni nini kwangu? Uniwie huruma, niweze kusema. Mimi ni nini kwako, hata uniagize nikupende, halafu nisipokutii unanikasirikia na kunitishia maafa makubwa? Je, kutokupenda si balaa kubwa tayari? Lo, kwa huruma yako, Bwana Mungu wangu, uniambie wewe ni nini kwangu. “Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako”. Sema hivyo, nami nitasikiliza. Tazama, moyo wangu unakusikiliza, Bwana; uuweke tayari ukaniambie, “Mimi ni wokovu wako”. Nitafuata sauti ya neno lako hilo hata nikufikie. Usinifiche uso wako: nife nisije kufa, bali niuone uso wako.
Nijalie nifanye unachoniagiza
Unijalie nifanye unachoagiza, halafu uniagize unachotaka: Nimechelewa kukupenda, Uzuri wa kale na mpya daima; nimechelewa kukupenda. Tazama, wewe ulikuwa ndani mwangu, nami nilikuwa nje na kukutafuta huko. Mimi, mbaya, nilikuwa ninaparamia vitu vizuri ulivyoviumba. Wewe ulikuwa nami, lakini mimi sikuwa nawe. Vilikuwa vikinishika mbali nawe viumbe vile ambavyo kama visingekuwa ndani yako hata kuwepo visingekuwepo. Uliniita, ukanipigia kelele, ukashinda uziwi wangu. Uliniangaza, ukanimulikia kama umeme angani, hatimaye ukaponya upofu wangu. Ulinipulizia harufu yako nami nikainusa, na sasa nakuonea shauku. Nimekuonja na sasa nakuonea njaa na kiu. Umenigusa nami sasa nawaka tamaa ya kupata amani yako. Sasa nakupenda wewe tu, nakufuata wewe tu, nakutafuta wewe tu, niko tayari kukutumikia wewe tu, kwa kuwa wewe tu unatawala kwa haki, natamani kuwa chini ya uwezo wako. Naomba kitu hiki tu kutokana na hisani yako kuu: kwamba unigeuzie kabisa kwako, usiruhusu chochote kunizuia nisielekee kwako.