Maombi ya Papa kwa ajili ya Niger,kanda ya Sahel ili kupata suluhisho
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 20 Agosti 2023, amesema kwamba: “Ninafuatilia kwa wasiwasi kile kinachotokea nchini Niger. Naungana na ombi la Maaskofu katika kuunga mkono amani ya nchi na utulivu wa Kanda ya Sahel. Ninasindikiza na maombi yangu juhudi za Jumuiya ya Kimataifa ya kutafuta suluhisho la amani haraka iwezekanavyo kwa manufaa ya wote. Tuwaombee watu wapendwa wa Niger. Na tuombe amani kwa ajili ya watu wote waliojeruhiwa na vita na vurugu, hasa kwa Ukraine, ambayo imekuwa ikiteseka kwa muda mrefu”.
Baba Mtakatifu aidha akiendelea amesema: “Ninawasalimu ninyi nyote, waamini wa Roma na mahujaji kutoka nchi mbalimbali. Hasa, ninawasalimu waseminari wapya wa Chuo cha Amerika Kaskazini na kuwatakia safari njema ya kimaendeleo; pamoja na salamu za jumuiya ya Borriquita ya Cadiz, nchini Hispania; Ninawasalimu Wapoland, huku nikifikiria pia kuhusu wanawake na wasichana wanaohiji kwenye Madhabahu ya Mama Yetu huko Piekary Śląskie."
Papa vile vile amesema "Ninawasalimu vijana wa Mpango wa “Tucum”, ambao wanaanza leo wa Njia ya Msalaba kupitia vituo vya treni vya Italia, ili kukutana na watu wanaoishi pembezoni na kuwaletea matumaini ya Injili. Ninawasalimu wote na ninawatakia Dominika njema. Tafadhali msisahau kuniombea. Mlo na Mchana mwena na kwaheri ya kuonana”. Ndivyo Baba Mtakatifu amehitimisha Salamu zake kwa mahujaji na waamini walifika katika uwanja wa Mtakatifu Petro Vatican.