Tafuta

Katekesi zinazoendeshwa na Makardinali pamoja na Maaskofu kwa ajili ya vijana hususan: Ekolojia, Udugu na Urafiki wa Kijamii pamoja na Huruma ya Mungu. Katekesi zinazoendeshwa na Makardinali pamoja na Maaskofu kwa ajili ya vijana hususan: Ekolojia, Udugu na Urafiki wa Kijamii pamoja na Huruma ya Mungu.   (Vatican Media)

Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni:Katekesi, Ikolojia, Udugu, Urafiki na Huruma

Kuanzia tarehe 2 Agosti hadi tarehe 4 Agosti, 2023 kuna katekesi zinazoendeshwa na Makardinali pamoja na Maaskofu kwa ajili ya vijana hususan: Ekolojia, Udugu na Urafiki wa Kijamii pamoja na Huruma ya Mungu. Katekesi hizi zinafanyika kadiri ya makundi ya lugha za vijana. Huu ni muda muafaka pia wa kujifunza Ketekesi kuhusu Bikira Maria, mwaliko kwa vijana kumuiga Mama wa Mungu, kwa kusikiliza na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 6 Agosti 2023 anashiriki katika Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni Jimbo kuu la Lisbon, Ureno inayonogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Hii ni hija yake ya 42 ya Kitume Kimataifa na mwendelezo wa tema kuhusu dhamana na utume wa Bikira Maria katika maisha ya Kanisa. Jumatano tarehe 2 Agosti 2023 baada ya kuwasili, amemtembelea Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno na hatimaye akawahutubia viongozi wa Serikali, vyama vya kiraia pamoja na wanadiplomasia amegusia kuhusu: Mkataba wa Lisbon, unaojulikana pia kama Mkataba wa Mageuzi uliorekebisha Mkataba wa Umoja wa Ulaya na hivyo kuanzishwa kwa Jumuiya Umoja wa Ulaya, uliotiwa saini tarehe 13 Desemba 2007 na kuanza kutumika rasmi tarehe 1 Desemba 2009. Lengo likiwa ni kujenga na kudumisha amani, usalama, ustawi, maendeleo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Jumuiya ya Umoja wa Ulaya inapania pamoja na mambo mengine kudumisha usawa, kupambana na umaskini, kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Mashuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu
Mashuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu

Kwa uwepo na ushiriki wa vijana wa kizazi kipya nchini Ureno, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya inayo dhamana ya ujenzi wa madaraja yanayounganisha Bara la Afrika na Mashariki ya Kati na hivyo kushiriki katika kutafuta, kukuza na kudumisha amani, upatanisho, majadiliano katika haki, ukweli na uwazi pamoja na kudumisha diplomasia ya Kimataifa itakayoweza kuzimisha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, ili rasilimali fedha hii itumike katika maboresho ya sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Ni mwaliko wa kuachana na falsafa ya kuwekeza katika utengenezaji wa silaha tayari kujikita katika ujenzi wa utamaduni wa uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatia sera za utoaji mimba na kifo laini. Baba Mtakatifu ameishukuru nchi ya Ureno kwa kuwa ni mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, tayari kuwachangamotisha vijana, kusafiri kwa pamoja katika matumaini ya kulinda, kutunza na kudumisha umoja, mazingira bora nyumba ya wote na udugu wa kibinadamu. Hii ni changamoto ya vijana wa kizazi kipya kujenga umoja na udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, huku wakishirikiana na kushikamana na wazee.

Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno amemshukuru na kumpongeza Papa.
Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno amemshukuru na kumpongeza Papa.

Kwa upande wake Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kujipambanua katika ushuhuda wa utu wa kibinadamu, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; katika mchakato wa ujenzi wa Injili ya matumaini, udugu wa kibinadamu pamoja na mapambano dhidi ya baa la njaa, umaskini, unyonyaji, dhuluma, ubaguzi pamoja na chuki dhidi ya wageni “Xenofobia.” Anasema Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno, Baba Mtakatifu amekuwa ni shuhuda na chombo cha majadiliano ya kidini na kiekumene na kwamba, sauti yake, inavuka mipaka ya Kanisa Katoliki. Anampongeza Baba Mtakatifu kwa kuendelea kuwahamasisha vijana wa kizazi kipya kusimama kidete kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu, wala wajanja wachache kuwapoka furaha ya ujana wao. Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni yananogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Huu ni mwaliko wa kuamka kwani bado vijana hawajachelewa, tayari kwenda mbali zaidi, kuliko walivyofanya jana, kesho inawadai zaidi, Vijana wanatakiwa kuondoka kwa haraka ili wakatekeleze majukumu yaliyoko mbele yao!

Katekesi: Ikolojia, Udugu, Urafiki na Huruma ya Mungu
Katekesi: Ikolojia, Udugu, Urafiki na Huruma ya Mungu

Kuanzia tarehe 2 Agosti hadi tarehe 4 Agosti, 2023 kuna katekesi zinazoendeshwa na Makardinali pamoja na Maaskofu kwa ajili ya vijana hususan: Ikolojia, Udugu na Urafiki wa Kijamii pamoja na Huruma ya Mungu. Katekesi hizi zinafanyika kadiri ya makundi ya lugha za vijana. Huu ni muda muafaka pia wa kujifunza Ketekesi kuhusu Bikira Maria, mwaliko kwa vijana kumuiga Mama wa Mungu, kwa kusikiliza na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao; Kukuza na kudumisha moyo wa Sala; Ukimya na tafakuri ya kina tayari kujenga mshikamano na mafungamano na Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ni wakati wa kujenga na kukuza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ili kukuza moyo wa sala na majadiliano, tayari kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani.

Vijana Duniani 2023
03 August 2023, 15:05