Kumbukizi la uchaguzi wa Papa Yohane Paulo wa Kwanza,26 Agosti 1978
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Papa Yohane Paul I (kwa Kilatini: Ioannes Paulus PP. I) aliyezaliwa huko Canale Agordo, mnamo tarehe 17 Oktoba 1912 na kubatizwa kwa jina la Albino Luciani, alikuwa Askofu wa 263 wa Roma na Papa wa Kanisa Katoliki ulimwenguni kote. Alichaguliwa mnamo tarehe 26 Agosti 1978 na upapa wake ulikuwa ni wa kumi kwa kukaa kwa muda mfupi zaidi katika historia ya Kanisa Katoliki. Hii ni kwa sababu kifo chake kilitokea siku 33 tu baada ya kuchaguliwa kwake katika kiti cha Kharifa wa Mtume Petro.
Mnamo mwaka 2017, alitangazwa kuwa Mtumishi wa Mungu na Baba Mtakatifu Francisko. Na mnamo tarehe 13 Oktoba 2021, Papa Francisko aliidhinisha kutangazwa kuwa Mwenye eri kufuatia na muujiza uliohusishwa kwa maombezi ya Yohane Paulo wa I. Kwa hatua hiyo ilimfanya astahili kutangazwa kuwa mwenyeheri, kwa Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko mnamo tarehe 4 Septemba 2022 katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Mwenyeheri Papa Yohane Paulo I anakumbukwa sana kwa majina ya : “upendo wa Papa wa Tabasamu” na “Tabasamu la Mungu.” Kwake Yeye wameweka jumba la Makumbusho katika Jengo la kizamani la miaka ya karne ya XVI, huko Canale Agordo alikozaliwa, na kuweka humo mambo ambayo yanakumbusha maisha yake ya awali.