Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amewatumia vijana wa Italia ujumbe mfupi kwa njia ya video akiwataka wasonge mbele kwa ujasiri na furaha. Baba Mtakatifu Francisko amewatumia vijana wa Italia ujumbe mfupi kwa njia ya video akiwataka wasonge mbele kwa ujasiri na furaha. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Vijana Wanaokwenda Lisbon, Ureno! Siku ya Vijana Ulimwenguni

Baba Mtakatifu Francisko amewatumia vijana wa Italia ujumbe mfupi kwa njia ya video akiwataka wasonge mbele kwa ujasiri na furaha, daima wakijitahidi kuambatana na kufungamana na vijana wengine, kamwe wasitembee pweke. Baba Mtakatifu anawatakia heri, baraka na mafanikio vijana wote wanaojiandaa kuanza safari kuelekea Jimbo kuu la Lisbon, Ureno ili kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa mwaka 2023. Ujasiri na Alama za Nyakati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023, yananogeshwa na kauli mbiu “Maria akaondoka kwa haraka” Lk 1:39. Kimsingi hii ni hija ya maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini lakini hasa vijana wa kizazi kipya, kuguswa na moyo wa unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa wengine kama alivyofanya Bikira Maria kwa kumtembelea binamu yake Elizabeti. Safari hii ya Bikira Maria inafungua macho ya waamini ili kuangalia historia ya wokovu, kwa wanawake hawa wawili, wanavyopokea na kukumbatia upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao na inavyopenyeza katika historia ya mwanadamu na hivyo kumkirimia furaha ya Injili. Takwimu zinaonesha kwamba, vijana 60, 000 kutoka nchini Italia wanashiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni huko Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia vijana wa Italia ujumbe mfupi kwa njia ya video akiwataka wasonge mbele kwa ujasiri na furaha, daima wakijitahidi kuambatana na kufungamana na vijana wengine, kamwe wasitembee pweke. Baba Mtakatifu anawatakia heri, baraka na mafanikio vijana wote wanaojiandaa kuanza safari kuelekea Jimbo kuu la Lisbon, Ureno ili kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa mwaka 2023. Anawataka wafike hatima ya safari yao, huku wakiwa wamesheheni furaha. Safari na kuanza kusafiri ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya mwanadamu! Safari ina raha, furaha, magumu na changamoto zake. Wakati mwingine kunahitajika ubora wa kuweza kuendelea kuwepo barabarani yaani ujasiri, daima kwa kusoma alama za nyakati ili kutambua hatima ya safari hiyo!

Papa Francisko anawatia shime vijana kujiandaa vyema kwa Siku ya Vijana
Papa Francisko anawatia shime vijana kujiandaa vyema kwa Siku ya Vijana

Safari hii itekelezwe kwa ujasiri bila woga, kwa kushirikiana na kushikamana na vijana wengine ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Safari ya kuelekea Lisbon nchini Ureno iwe ni sehemu ya maisha ya kila siku, kwa kushirikiana na kushikamana na vijana wengine, ili kuepuka kishawishi cha kutembea pweke hatari katika maisha ya ujana! Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuwasili nchini Ureno tarehe 2 Agosti 2023 tayari kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni. Katika maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka 2023, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu aliandamana na Bibi Cesira Cruciani mwenye umri wa miaka 75 na mjukuu wake anaitwa Michele Messina anayeshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni huko Lisbon, Ureno, kutoa salam na matashi mema kwa vijana wanaojiandaa kwenda Jimbo kuu la Lisbon, kuhudhuria Siku ya Vijana Ulimwenguni. Hili ni Agano kati ya vijana wa kizazi kipya na wale “vijana wa zamani” yaani wazee ili kwa pamoja waweze kushirikiana na kushikamana katika ujenzi wa jamii. Mara baada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 23 Julai 2023 wazee watano waliowawakilisha wazee wenzao kutoka katika mabara matano, wamewakabidhi vijana wa kizazi kipya Msalaba wa Siku ya Vijana Ulimwenguni, kama kielelezo cha kurithisha imani kutoka kizazi hata kizazi. Mwaka huu maadhimisho ya Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani yameadhimishwa karibu sana na Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023. Mwenyezi Mungu kwa njia ya mahusiano na mafungamano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, wanatambua kwamba, wameitwa kukuza na kudumisha kumbukumbu na kutambua uzuri wa kuwa ni sehemu ya historia kubwa zaidi.

Maandalizi ya Siku ya Vijana Ulimwenguni yamepamba moto
Maandalizi ya Siku ya Vijana Ulimwenguni yamepamba moto

Baba Mtakatifu anakaza kusema, urafiki na wazee unaweza kuwasaidia vijana kuona maisha yao si tu kwamba, ni jambo la mpito na kwamba, si kila kitu kinawategemea wao na uwezo wao. Kwa wazee, uwepo wa kijana katika maisha yao unaweza kuwapa matumaini kwamba, uzoefu wao hautapotea na kwamba, ndoto zao zinaweza kupata utimilifu. Mwaka huu maadhimisho ya Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani yanaadhimishwa karibu sana na Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yanayoanza kutimua vumbi huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Sherehe zote mbili zinagusia “haraka” ambayo Bikira Maria alipanga kumtembelea binamu yake Elizabeti, mwaliko kwa watu wa Mungu kutafakari dhamana na wajibu unaowaunganisha vijana na wazee. Mwenyezi Mungu kwa njia ya mahusiano na mafungamano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, wanatambua kwamba, wameitwa kukuza na kudumisha kumbukumbu na kutambua uzuri wa kuwa ni sehemu ya historia kubwa zaidi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, urafiki na wazee unaweza kuwasaidia vijana kuona maisha yao si tu kwamba, ni jambo la mpito na kwamba, si kila kitu kinawategemea wao na uwezo wao. Kwa wazee, uwepo wa kijana katika maisha yao unaweza kuwapa matumaini kwamba, uzoefu wao hautapotea na kwamba, ndoto zao zinaweza kupata utimilifu.

Wazee wanapaswa kurithisha imani kwa watoto na vijana
Wazee wanapaswa kurithisha imani kwa watoto na vijana

Hija ya Bikira Maria kwa binamu yake Elizabeti na ufahamu wao wa pamoja kwamba, huruma ya Mungu ni kutoka kizazi hata kizazi, inawakumbusha waamini kwamba, peke yao, hawawezi kusonga mbele, sembuse, kujiokoa na kwamba, uwepo wa Mwenyezi Mungu ni sehemu ya historia ya watu. Bikira Maria aliyatamka haya katika utenzi wake wa “Magnificat”, akielezea furaha yake inavyopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyefanya nguvu kwa mkono wake, akawatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao, amewaangusha wakuu kutoka katika viti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza; wenye njaa amewashibisha mema, na wenye mali amewaondoa mikono mitupu, amekumbuka rehema zake kama alivyowaambia Baba zetu, Ibrahimu na uzao wake. Rej. Lk. 1: 51-55. Waamini wajitahidi kufahamu utendaji wa Mungu, kwa kukumbuka kwamba, Mwenyezi Mungu anakusudia maisha ya waja wake, yafikie utimilifu na kwamba, matumaini na ndoto za maisha zinapitia mchakato wa ukuaji na ukomavu katika majadiliano pamoja na mahusiano na watu wengine, changamoto na mwaliko wa kuondokana na upofu unaojikita katika fedha, mali na usasa, kwani Mwenyezi Mungu hatendi kwa jinsi hii. Mpango wa upendo wa Mungu unakumbatia na kuviunganisha vizazi; unajumuisha na kuwasaidia watu kusonga mbele. Huu ni mwaliko kwa vijana kuwa tayari kujiondoa katika tafakuri ya muda mfupi ambayo inaweza kuwazuia kufanya kitu chenye tija. Wazee wanahamasishwa kutopoteza nguvu zao za kimwili na kuanza kufikiri kwa majuto juu ya fursa na nafasi walizokosa au kupoteza na badala yake, Baba Mtakatifu anawahimiza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, huku wakiruhusu neema ya Mwenyezi Mungu kuwaunda upya. Hii ni neema ambayo kutoka kizazi hadi kizazi inamkomboa mwanadamu kutoka katika hofu na kuwaza ya zamani!

Wazee wanalo jukumu la kusali na kuwaombea vijana
Wazee wanalo jukumu la kusali na kuwaombea vijana

Katika mkutano kati ya Bikira Maria na binamu yake Elizabeti; kati ya vijana na wazee, ni mikutano inayofungua mbele ya macho ya waamini mwanzo wa wokovu katika kukumbatiana kwao katika hali ya ukimya, huruma ya Mungu inaleta wingi wa furaha katika historia ya maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafakari juu ya mkutano huu, kwa kuweka mbele ya macho yao, picha inayoonesha ishara ya kukumbatiana kati ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na binamu yake Elizabeti, Mama wa Yohane Mbatizaji na hivyo kuitengeneza katika akili na nyoyo zao kama umbo lenye kuleta mvuto! Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kutowaacha wazee katika upweke wao, kwani uwepo wao katika familia na jamii ni wa thamani kubwa, kwa sababu binadamu wote wanashiriki urithi huo huo na ni sehemu ya watu waliojitolea kuhifadhi mizizi yake. Kutokana na uwepo wa wazee, waamini wamepokea zawadi ya kuwa ni watu watakatifu wa Mungu. Kanisa na jamii katika ujumla wake, linawahitaji wazee kwa sababu wanarithisha ya kale ambayo yanahitajika ili kujenga ya mbeleni kwa siku zijazo. Huu ni mwaliko kwa kushirikiana na kushikamana na wazee; kwa kuwaheshimu na kuwathamini na kamwe wazee wasitelekezwe pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Maadhimisho ya Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani ni ishara ndogo lakini yenye thamani ya matumaini kwao na kwa Kanisa zima. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuifanya siku hii kuwa ni fursa ya kukutana kwa furaha na upya kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee.

Mshikamano wa imani. mapendo na imani kati ya vizazi
Mshikamano wa imani. mapendo na imani kati ya vizazi

Baba Mtakatifu anawaalika vijana wanaojiandaa kuadhimisha Siku ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi mbalimbali, kuanza maadhimisho hayo kwa kuwatembelea babu, bibi na wazee wanaoishi peke yao. Sala na maombi yao, ni zawadi na amana kubwa na kwamba, ndani mwa vijana watabeba baraka na neema ya kukutana na wazee hawa. Baba Mtakatifu anawaalika wazee kuwasindikiza vijana wa kizazi kipya wanaojiandaa kuadhimisha Siku ya Vijana Ulimwenguni kuanzia tarehe 1-6 Agosti 2023 huko Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. Vijana ni jibu la maombi ya wazee kwa Mwenyezi Mungu, matunda ya kazi waliyoipanda, ishara na kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu hawaachi waja wake, lakini daima huwahuisha upya kwa ubunifu wa Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka huu wa 2023 anawatakia heri na baraka zinazobubujika kutoka kwenye kumbatio kati ya Bikira Maria na Elizabeti, ili liwajaze amani na hatimaye, anatoa baraka zake za kitume.

Papa Vijana Lisbon

 

25 July 2023, 16:00