Uekumene wa Damu Unasimikwa Katika Damu ya Mashuhuda wa Imani Kwa Kristo Yesu na Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake anakazia uekumene wa: Damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha adili na matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 23 Februari 2023 alikutana na kuzungumza na Mapadre vijana pamoja na watawa kutoka Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki anasema, Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbalimbali za dunia ni mambo yanayowaunganisha wote bila ubaguzi hata kidogo. Damu ya Wakristo, itaendelea kuwa ni mbegu ya Ukristo na mchakato wa umoja wa Wakristo. Wakristo wote wanateseka na kudhulumiwa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kumbe, uekumene wa damu una nguvu sana kama kielelezo cha ushuhuda wa imani yenye mvuto na mashiko. Umoja wa Kanisa upewe kipaumbele cha kwanza kuliko mafao mengine yote! Kwa njia hii, Wakristo wataweza kujenga na kudumisha ushirika na Kristo Yesu pamoja na Wakristo wenzao kwa kuumega na kushiriki Fumbo la Ekaristi, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kama ilivyokuwa kwa mahujaji wa Emau walivyoamua kurejea tena Yerusalemu ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, “ili ulimwengu upate kusadiki.” Yn 17:21.
Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa hotuba yake amewataka Mapadre vijana pamoja na watawa kutoka Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili na Kristo Yesu Mfufuka. Wakuze na kukoleza majadiliano ya kidugu, ili kupyaisha na kunogesha moto wa ushirika wa waamini. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Julai 2023 ameanzisha Tume ya Mashahidi Wapya, Mashuhuda wa Imani kwenye Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu. Lengo ni kuandaa orodha ya majina ya waamini walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ikumbukwe kwamba, Wafiadini ndani ya Kanisa ni Mashuhuda wa matumaini yanayobubujika kutoka katika Injili ya Kristo Yesu na kukita mizizi yake katika upendo wa kweli. Tumaini huweka hai imani ya kina kwamba, wema una nguvu kuliko uovu, kwa sababu Mwenyezi Mungu katika Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti. Tume hii itaendeleza tafiti ambazo zimeanza tangu wakati wa Maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, kuwatambua Mashuhuda wa imani katika robo hii ya kwanza ya Karne ya Ishirini na moja na kisha kuendelea katika siku zijazo.
Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema katika miaka ya hivi karibuni, kuna Wakristo wengi ambao wameyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake na kwamba, hiki ni kielelezo makini cha uekumene wa damu unaosimikwa katika damu ya mashuhuda wa imani. Mashuhuda waliosadaka maisha yao kwa ajili ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake ni alama ya umoja wa Kanisa, kiasi kwamba, mashuhuda hawa huko mbinguni sasa wanaishi ushirika kamili wa watakatifu wa Mungu na kwamba, hawa wanaweza kuwasaidia Wakristo walioko huku Bondeni kwenye machozi kutafuta na kuambata umoja wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema kwamba, kwa hakika wafia imani wameandamana na maisha ya Kanisa katika kila zama na wanastawi wakiwa ni “matunda yaliyoiva na bora ya shamba la Mzabibu la Bwana.”
Wafia imani ni wengi zaidi katika zama hizi kuliko katika karne ya kwanza. Hawa ni maaskofu, mapadre watawa na waamini walei na familia zao ambao katika nchi mbalimbali za ulimwengu wana tuzo ya maisha yao na kwamba, wamethibitisha upendo mkuu. Kardinali Kurt Koch anasema, katika orodha hii kuna wafiadini wa Kanisa la Kikoptik, waliouwawa kikatiliki nchini Libya tarehe 15 Februari 2015 na ambao tayari wameandikwa kwenye Orodha ya Wafiadini “Martilogio Romano”, Mwezi Mei 2023 kwa uwepo wa Papa Tawadros wa Pili, kielelezo cha ushirika kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox na kwamba, wafiadini wote hawa ni waamini walei. Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema, kuna matumaini makubwa kwamba, wafiadini na mashuhuda wa imani wataliwezesha Kanisa sehemu mbalimbali za dunia kujizatiti katika kukuza na kudumisha ushirika wa Kanisa. Lakini inasikitisha kuona kwamba, hata Wakristo wenyewe kwa wenyewe wanauwana. Ni matumaini yake kwamba, barua hii ya Baba Mtakatifu itasaidia kuwaunganisha Wakristo ili kukuza na kudumisha uekumene wa damu unaosimikwa katika ushuhuda wa damu ya Wakristo! Tume ya Mashahidi Wapya, Mashuhuda wa Imani kwenye Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu inaongozwa na Kardinali Marcello Semeralo, Rais wa Tume, Askofu Fabio Fabene, Katibu; Professa Andrea Riccardi, Muasisi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Makamu wa Rais, Monsinyo Marco Gnavi, Katibu, Paroko wa Kanisa kuu la “Santa Maria in Trastevere. Wajumbe ni pamoja na: Padre Dominique Arnauld, M.Afr; Pd. Kokou Mawuena Ambroise Atakpa; Sr. Nadia Coppa, ASC; Professa Gianni La Bella, Professa Maria Lupi; Padre Dinh Anh Nhue Nguyen, O.F.M. CONV; Shemasi Didier Rance; Mh. Roberto Regoli, Mh. Angelo Romano pamoja na Padre Arturo Marcelino Sosa Abascal, SJ.