Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka huu wa 2023 ni hapo Dominika tarehe 23 Julai 2023 Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka huu wa 2023 ni hapo Dominika tarehe 23 Julai 2023   (Vatican Media)

Sala Kwa Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani Kwa Mwaka 2023

Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani ni hapo Dominika tarehe 23 Julai 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi” Lk. 1:50. Papa katika ujumbe wake anagusia kuhusu: Bikira Maria akiwa amejazwa na nguvu ya Roho Mtakatifu akaondoka kwa haraka, Mkutano kati ya Bikira Maria na Elizabeti, Kati ya vijana na wazee; Iwe ni siku ya kukutana kwa furaha na kwa upya kati ya vijana wa kizazi kipya na vijana wa zamani! Kukutana

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka huu wa 2023 ni hapo Dominika tarehe 23 Julai 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi” Lk. 1:50. Maadhimisho haya yanafanyika siku chache tu kabla ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria akaondoka kwa haraka” Lk 1:39. Ifuatayo ni sala iliyotungwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa Mwaka 2023.

Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka 2023
Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka 2023

“Bikira Maria, Mama wa imani na matumaini, kielelezo kwa ubinadamu huu uliopinda kwa kutojali, nifanye niwe tayari kukubali mapenzi ya Mungu, kutukuza na kusifu rehema zake. Bikira Maria, Mama wa ujasiri, wewe unayejua moyo wangu, usiruhusu nikatishwe tamaa. Ninayakabidhi maisha yangu mikononi mwako kwa ujasiri. Ponya majeraha yangu. Huruma yako ifuatane nami njiani. Uwepo wako, Mama wa upendo, unatuletea uzoefu wa furaha ya kuona familia zetu zikiwa zimeungana. Nisaidie kusambaza huruma na Upendo wa Mungu kwa wajukuu na vijana ili, pamoja na kuwaombea, tuweze kusali pamoja nao. Bikira Maria, karama ya Roho Mtakatifu iombee kwa ajili yangu; nijalie moyoni mwangu faraja ili niache mabaki ya imani miongoni mwa vijana, nikishuhudia uzuri wa maisha, nikijua kwamba maisha yana kikomo na zaidi ya hayo yapo mbele yetu lipo kumbatio la Baba yetu. Amina.”

Kauli mbiu "Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi
Kauli mbiu "Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kimsingi hii ni hija ya maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini lakini hasa vijana wa kizazi kipya, kuguswa na moyo wa unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa wengine kama alivyofanya Bikira Maria kwa kumtembelea binamu yake Elizabeth. Safari hii ya Bikira Maria inafungua macho ya waamini ili kuangalia historia ya wokovu, kwa wanawake hawa wawili, wanavyopokea na kukumbatia upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao na inavyopenyeza katika historia ya mwanadamu na hivyo kumkirimia furaha ya Injili. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuadhimisha Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa Ibada ya Misa Takatifu na vijana wa kizazi kipya watumie fursa hii, kuwatembelea na kuwasaidia wazee katika maisha yao. Na wazee nao, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno, wajisadake kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea vijana wa kizazi kipya katika hija ya maisha ya kiroho kama sehemu ya ujenzi wa mshikamano na mafungamano ya kijamii. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa awe ni mfano bora wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu katika ulimwengu mamboleo.

Sala siku ya wazee 2023
18 July 2023, 14:13