Papa kwa vijana wa Córdoba:katika WYD inueni pamoja kikombe cha udugu!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Dominika tarehe 16 Julai 2023, kabla ya sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kikundi cha Vijana wa Jimbo kuu katoliki la Córdoba nchini Argentina watakaoshiriki katika Siku ya Vijana Duniani (WYD) ijayo huko Lisbon nchini Ureno kuanzia tarehe 1 hadi 6 Agosti 2023. Papa Francisko akizungumza nao kwa lugha yake ya kihispania amesema wao kama ilivyo kwa maelfu ya vijana wengine ambao wanajiandaa kuelekea Ureno katika siku hizi, wako wanaweka uhai wa kauli mbiu itakayowajumuisha pamoja isemayo " Kama Maria", waliamka wakaacha kile wanachojua, familia zako, starehe zao na walianza safari kwa haraka ili kukutana na wengine (taz. Lk 1:39). Papa ameongeza kusema kuwa: huenda wengine waliondoka na mwanzi pamoja, na wengine gitaa; lakini kinachowatambulisha wao wote ni "T shet ya imani na upendo kwa Mungu na ndugu”.
Tunaweza kuinua kikombe pamoja cha udugu
Kwa kukazia zaidi, Papa Francisko amependelea kuuliza swali: “Je mmeweza kugundua kuwa mko mnajiandaa kwa ajili ya kucheza kombe la dunia? Kombe hili la Dunia ni maalum sana; ni mechi ya kirafiki ambayo hakuna washindi au walioshindwa, lakini sisi sote tunashinda. Ndiyo, kwa sababu tunapotoka nje ya nafsi zetu na kukutana na wengine, tunaposhiriki, yaani, tunapotoa kile tulicho nacho na tuko tayari kupokea kile ambacho wengine wanatupatia na wakati hatukatai mtu yeyote; basi sisi sote ni washindi na kwa pamoja tunaweza kuinua kikombe cha udugu. Ni jinsi gani kilivyo cha lazima katika wakati wetu!, Papa Francisko amesema.
Kabla ya WYD vijana wa Cordoba wataona mjini Roma nyuso za wakristo walitoa maisha yao
Kufuatia na hija yao mjini Roma, Baba Mtakatifu Francisiko amesema kwamba kabla ya kuanza Siku ya Vijana duniani, wanaweza kuona nyayo za Wakristo wengi waliomfuata Kristo hadi mwisho, za watakatifu wengi waliotoa maisha yao kwa ajili yake kwa nyakati tofauti katika historia. Hii inatufundisha kwamba, tukiwa na timu ya Kristo, mchezo unachezwa hadi dakika ya mwisho, hatuwezi kukengeushwa au kufunga mabao dhidi yake. Ni lazima tuwe waangalifu na kufanya kazi kama timu, tukifuata maagizo ya mkurugenzi wa kiufundi, yaani, ya watu wanaotusindikiza na kutuongoza,ili kuwa marafiki bora na Yesu kila siku.”
Papa Francisko kwa hiyo amewatia moyo ili waishi kwa bidii ya Siku hii ya Vijana Ulimwenguni, ambayo "itawatajirisha kwa utofauti mkubwa wa nyuso, tamaduni, uzoefu, maonesho tofauti na maonesho ya imani yetu. Lakini, zaidi ya yote, wataweza kuona shauku ya Yesu kikamilifu: kwamba sisi ni “wamoja” ili ulimwengu upate kuamini (rej. Yh 17:21) na hii itawasaidia kushuhudia furaha ya Injili kwa vijana wengine wengi wasiojua maana ya maisha au waliopotea njia ya kwenda mbele." Papa amehitimisha kwa kuwatakia "heri ya kucheza vizuri mchezo". Na kwamba Yesu awabariki na Bikira Maria awalinde. Lakini hakusahau kama kawaida yake kuomba wasali kwa ajili yake na kuwamba wataonana huko Lisbon.