Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 23 Julai 2023 amegusia kuhusu athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbalimbali za dunia; kuna sehemu ambazo zimekumbwa na joto kali kiasi cha kusababisha mafuriko, majanga ya moto na baridi kali Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 23 Julai 2023 amegusia kuhusu athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbalimbali za dunia; kuna sehemu ambazo zimekumbwa na joto kali kiasi cha kusababisha mafuriko, majanga ya moto na baridi kali   (AFP or licensors)

Papa Francisko: Athari za Mabadiliko ya Tabianchi! Ukame, Mafuriko na Joto la Kutisha

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 23 Julai 2023 amegusia kuhusu athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbalimbali za dunia; kuna sehemu ambazo zimekumbwa na joto kali kiasi cha kusababisha mafuriko, majanga ya moto na baridi kali kama ilivyojitokeza hivi karubuni, huko Korea ya Kusini. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaongezeka kwa kasi kubwa, hasa kutokana na vimbunga, mvua kubwa, ukame, mawimbi ya baridi na halijoto tete sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika dimbwi la umaskini na magonjwa ya mlipuko. Ikolojia ya maisha ya kiroho iwahamasishe waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na shauku ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwa kufungamanisha maisha ya kiroho na utunzaji bora wa mazingira, kwa kutambua uwepo angavu wa Mungu katika kazi ya uumbaji, kwa kuonesha moyo wa ukarimu na kujali, kwa kutambua kwamba, ulimwengu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, huu ni mwaliko wa kujitoa sadaka kwa ajili ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Changamoto ya utunzaji bora wa mazingira haina budi kupewa kipaumbele cha pekee kama ilivyo pia kwa sekta ya afya na vita sehemu mbalimbali za dunia, wito kwa wote ni wongofu wa kiikolojia unaosimikwa katika wongofu wa kijumuiya ili kuleta mabadiliko endelevu na ya kudumu; mambo yanayopaswa pia kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa.

Athari za mabadiliko ya tabianchi wimbi la joto kali
Athari za mabadiliko ya tabianchi wimbi la joto kali

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kuendelea kujikita katika mchakato wa kuragibisha elimu ya ikolojia na maendeleo fungamani ya binadamu. Amesema, changamoto na matatizo yanayosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi zinahitaji toba na wongofu wa ndani pamoja na maamuzi thabiti yanayopaswa kufanywa na kutekelezwa kwa ujasiri. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Vita ya Tatu ya Dunia inayoendelea kupiganwa sehemu mbalimbali za dunia ni matukio yenye athari kubwa kisiasa, kiuchumi na kijamii kiasi cha kutishia ulinzi na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa; Usalama na uhakika wa chakula duniani. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika mambo makuu manne: Kudhibiti, kukabiliana, fedha, hasara na uharibifu (Mitigation, adaptation, finance, loss and damage).

Korea ya Kusini imeathirika kutoka mabadiliko ya tabianchi
Korea ya Kusini imeathirika kutoka mabadiliko ya tabianchi

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 23 Julai 2023 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amegusia kuhusu athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbalimbali za dunia; kuna sehemu ambazo zimekumbwa na joto kali kiasi cha kusababisha mafuriko, majanga ya moto na baridi kali kama ilivyojitokeza hivi karubuni, huko Korea ya Kusini. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaongezeka kwa kasi kubwa, hasa kutokana na vimbunga, mvua kubwa, ukame, mawimbi ya baridi na halijoto isiyo ya kawaida, kulingana na utafiti uliochapishwa katika Jarida na “Nature” kwani, wastani wa halijoto Korea ya Kusini imeongezeka kwa takriban nyuzi joto 1.5 katika karne iliyopita.

Algeria imeathirika kwa janga la moto
Algeria imeathirika kwa janga la moto

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wanaoteseka kutokana na majanga asilia na wale ambao hawana makazi ya kudumu. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kuwaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, kutekeleza kwa vitendo maamuzi yaliyokwisha kufikiwa ili kudhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa na kwamba, hii ni changamoto pevu inayopaswa kufanyiwa kazi bila mzaha na kwamba, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni wajibu wa kila binadamu. Habari kutoka nchini Ugiriki zinaonesha kwamba, watu zaidi ya 30, 000 wengi wao wakiwa ni watalii wamelazimika kuondoka nchini Ugiriki. Nchini Italia miji ya: Catania, Siracusa na mkoa wa Sicilia umekumbwa na wimbi kubwa la joto kali kiasi cha kufikia nyuzijoto 50 na hivyo kujikuta miji hii haina nishati ya umeme.

Mazingira
25 July 2023, 14:45