Papa apongeza Jumuiya ya Cenacolo kwa miaka 40 ya kutoa huduma!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Mara baada ya tafakari na sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 16 Julai 2023, Baba Mtakatifu Francisko akiwageukia waamini na mahujaji waliofika kwa wingi katika uwanja wa Mtakatifu Petro, amesema kuwa “Kwa moyo mkunjufu, ninatuma salamu zangu kwa Jumuiya ya Cenacolo, ambayo imekuwa mahali pa kukaribisha na kuhamasisha watu kwa miaka 40; Ninambariki Mama Elvira, Askofu wa Saluzzo na ndugu na marafiki wote. Ni kitu kizuri mnachofanya na ni vizuri kuwepo! Asante!
Akiendelea Papa Francisko aidha amesalimu Wamisionari wa Mama Yetu wa Mitume waliokusanyika jijini Roma kwa ajili ya Mkutano wao mkuu. Kadhalika amesalimu wote, waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Warumi na mahujaji kutoka nchi mbalimbali.
Papa amependa “kuwasalimu na kuwashukuru Parokia zote zinazofanya shughuli za majira ya joto na watoto na vijana katika kipindi hiki hata mjini Vatican kuna kikundi kimoja ambacho kinathaminiwa sana," Shukrani kwa makuhani, watawa, wahuishaji na familia! alisisitiza.
Katika muktadha huo, Papa aliwatakia kila la kheri na baraka kwa toleo lijalo la Tamasha ya Filamu la Giffoni, ambapo wahusika wakuu ni watoto na vijana. Na kwa kuhitimisha amewatakia wote Dominika njema, lakini kama kawaida yake akiwasihi wasisahau kumuombea na yeye anafanya hiyo hivyo!