Nia za Baba Mtakatifu Francisko Kwa Mwezi Agosti 2023: Siku ya Vijana Ulimwenguni
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yanaanza kutimua vumbi huko Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Agosti 2023 anayaangalia Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023, akiwakumbusha vijana kwamba, Kanisa si klabu ya wazee bali ni mahali pa vijana, kwa sababu kama Kanisa litageuka kuwa ni klabu ya wazee, litakufa. Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema, ikiwa kama unaishi na kijana, hata wewe mwenyewe unageuka kuwa kijana. Kanisa linawahitaji vijana wa kizazi kipya, kumbe kwa mantiki hii, haliwezi kuzeeka. Kauli mbiu inayonogesha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni ni “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Bikira Maria alipoambiwa kwamba, angekuwa ni Mama wa Mungu hakukaa kitako na kuanza kujipiga picha, bali aliondoka kwa haraka, akaenda hata nchi za milimani, ili kuhudumia na kumsaidia binamu yake Elizabeti aliyekuwa mjamzito! Huu ni mwaliko kwa vijana kujifunza kutoka kwa Bikira Maria, ili kuondoka kwa haraka kwa ajili ya kuwasaidia wengine. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jimbo kuu la Lisbon, Ureno limechaguliwa kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, ili kupandikiza mbegu ya matumaini kwa siku za usoni; mahali ambapo upendo unapewa kipaumbele cha kwanza. Jumuiya ya Kimataifa inashuhudia vita na mipasuko ya kijamii sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, watu wanahitaji ulimwengu mpya ambao hauogopi kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili, kuwatangazi watu wa Mataifa ile furaha ya Injili.
Ikiwa kama Wakristo wenyewe hawana furaha, wala hawaaminiki, hakutakuwepo na mtu yeyote atakaye waamini. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana wa kizazi kipya kusali ili kwamba, Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni yawasaidie vijana wa kizazi kipya kujielekeza zaidi katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha yao. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Agosti 2023 anakazia kuhusu dhamana na utume wa vijana wa kizazi kipya katika Kanisa na ulimwengu, yaani kuondoka kwa haraka kwa ajili ya huduma kwa watu wengine. Nia za Baba Mtakatifu Francisko zinasambazwa sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya Mtandao wa Sala Kimataifa ambao umeundwa kwa kushirikiana na Mfuko wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Lisbon 2023, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kujizatiti kwa haraka kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, anajitahidi kujibu maswali ya msingi yaliyoulizwa na vijana wa kizazi kipya kutoka nchini Ufilippini, Brazil na Pwani ya Pembe, ambao ni umoja wa wanachama wa Harakati za Vijana wa Kiekaristi “Eucharistic Youth Movement, EYM” unaoundwa na vijana 1, 700, 000 kutoka katika nchi 60 duniani. Hawa wanamuuliza Baba Mtakatifu ikiwa kama Kanisa ni kwa ajili ya wazee peke yao na kwa nini aliamua kuchagua tema ya Bikira Maria ili kunogesha maadhimisho haya.
Kardinali mteule Américo Manuel Alves Aguiar, Rais wa Mfuko wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Lisbon kwa Mwaka 2023 ambaye pia ni Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno anasema, hili ni tukio la vijana wanaokutana na Baba Mtakatifu Francisko; ni tukio linalowakutanisha vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ni tukio linalowakutanisha vijana na Kristo Yesu aliye hai. Kwa hakika, vijana wengi wataguswa na maneno ya Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya, kwa kutambua kwamba, vijana kimsingi wanakutana na Kristo Yesu kila siku ya maisha yao, changamoto na mwaliko wa kujisadaka bila ya kujibakiza sanjari na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kwa Kristo Mfufuka. Naye Padre Joào Chagas, Mkurugenzi wa Idara ya Vijana, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, inapendeza kwa vijana kusali, kutafakari sanjari na kujadiliana, kwani vijana wanazo ndoto, lakini wanahitaji hekima, busara na maono ya wazee. Vijana wanaweza kuruka na kupaa, lakini wanahitaji kugundua mizizi na asili yao, yaani kutambua historia ya maisha yao. Ndiyo maana kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na hasa baada ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, uliopelekea watu kujitenga. Kumbe, Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni ni fursa adhimu kwa vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia kukutana tena Jimbo kuu la Lisbon. Kwa upande wake, Padre Frédéric Fornos S.J, Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Agosti 2023 anajikita zaidi katika ulimwengu wa vijana wa kizazi kipya; maandalizi ambayo yalianza kunako mwaka 2020 kwa kusindikizwa na sala. Kuanzia tarehe 30 Julai hadi tarehe 6 Agosti 2023 Mtandao wa Sala Kimataifa utatumika kuwaunganisha vijana ambao kutokana na sababu mbalimbali hawataweza kuhudhuria katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023. Huu ni msaada wa sala, tafakari na matukio mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023.