Mshikamano wa Papa Francisko na Wakimbizi na Wahamiaji wa Afrika
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 23 Julai 2023, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alivuta hisia zake kwa masaibu yanayoendelea kuwakumba wahamiaji na wakimbizi, Kaskazini mwa Bara la Afrika. Hawa ni watu ambao wanakumbana na mateso yasiyoelezeka, wamenaswa na kutelekezwa katika maeneo ya Jangwa la Sahara kwa majuma kadhaa. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kutoa ombi kwa wakuu wa nchi za Ulaya na Afrika kutoa msaada wa haraka kwa wahamiaji na wakimbizi hawa. Bahari ya Mediterania isigeuke tena kuwa kaburi lisilo na alama, mateso, ukatili na unyama dhidi ya ubinadamu. Mwenyezi Mungu apende kuangazia akili na nyoyo za watu wote, ili wawe na hisia zenye msukumo wa udugu, mshikamano wa kibinadamu pamoja na ukarimu.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuiombea Ukraine inayoteseka kwa vifo, uharibifu na majanga mbalimbali kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Urusi. Kuanzia mwisho wa mwaka 2010, mfululizo wa uasi usiotarajiwa umeenea Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati. Kumekuwepo na matukio ambayo yamebadilisha mfumo wa uhamiaji, ikiwa ni pamoja na kuwang’oa watu, kubadilisha wahamiaji waliopo na kuwafanya wakimbizi na hivyo kuzuia harakati za watu wanaohama ili kuokoa maisha yao, kutafuta ulinzi na usalam na hatimaye, kupata maisha bora zaidi. Machafuko ya hali ya kisiasa kwa baadhi ya nchi Kaskazini mwa Afrika yamepelekea mtiririko wa uhamiaji mchanganyiko yaani!Wahamiaji wa kiuchumi wanaolazimika kuingia kwenye njia zisizo za kawaida ili kutafuta maisha.