Makardinali wapya watasimikwa rasmi tarehe 30 Septemba 2023. Makardinali wapya watasimikwa rasmi tarehe 30 Septemba 2023.   (Vatican Media)

Orodha ya Makardinali Wapya: Protase Rugambwa, Stephen Mulla na Stephen Brislin

Makardinali wapya 21 kati yao Makardinali watatu ni wale ambao wamejipambanua katika huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao. Makardinali wapya watasimikwa rasmi tarehe 30 Septemba 2023. Kati yao yumo Askofu mkuu mwandamizi Protase Rugambwa wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania pamoja na Askofu mkuu Stephen Ameyu Martin MULLA, Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini pamoja na Askofu mkuu Stephen Brislin wa Jimbo kuu la Cape Town.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 9 Julai 2023 amewateuwa Makardinali wapya 21 kati yao Makardinali watatu ni wale ambao wamejipambanua katika huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao. Makardinali kimsingi ndio washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kukoleza juhudi za toba, haki, amani na maridhiano; kwa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili watu waweze kuishi katika mazingira bora zaidi. Makardinali wapya watasimikwa rasmi katika mkutano wa kawaida wa Makardinali utakaoadhimishwa tarehe 30 Septemba 2023 mjini Vatican. Hawa ni Makardinali wanaoonesha ukatoliki wa Kanisa, wanaotumwa kutangaza na kushuhudia upendo wa huruma ya Mungu kwa watu wote wa Mataifa. Makardinali hawa wataingizwa kwenye Jimbo kuu la Roma ili kuonesha mahusiano na mafungamano kati ya Khalifa w Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia yaliyoenea sehemu mbalimbali za dunia. Uteuzi wa Makardinali wapya ni changamoto kubwa inayowataka kujizatiti zaidi katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu, kwa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo; daima wakijielekeza zaidi katika huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Makardinali wanaojitambulisha kwa mavazi mekundu, wanaitwa kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, tayari kuwashirikisha watu wa Mataifa, ile furaha ya Injili. Ni mwaliko wa huduma makini kwa watu wa Mungu. Jicho la kibaba linalooneshwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa maskini na wale wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii, ni chachu ya matumaini na mapendo ambayo yanapaswa kutawala katika maisha ya watu! Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Aprili 2023 alimteuwa Askofu mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania.

Makardinali ni washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro
Makardinali ni washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro

Itakumbukwa kwamba, Kardinali mteule Rugambwa alizaliwa tarehe 31 Mei 1960 huko Bunena-Bukoba nchini Tanzania, akapata Daraja Takatifu ya Upadri kutoka mikononi mwa Mtakatifu Yohane wa Pili alipotembelea Tanzania tarehe 2 Septemba 1990 na kuwa Padri wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara. Kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2008 alifanya utume wake kwenye Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu mjini Vatican. Baba Mtakatifu Benedikto XVI, tarehe 18 Januari 2008 akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, na tarehe 26 Juni 2012 akateuliwa kuwa Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari na wakati huo huo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu. Tarehe 9 Novemba 2017 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Baada ya kulitumikia Baraza kwa vipindi viwili na muda wake ulipogota ukomo, kadiri ya Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” tarehe 13 Aprili 2023, Baba Mtakatifu amemteuwa Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu wenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania.

Kardinali mteule Protase Rugambwa akiagana na Papa Francisko mjini Vatican
Kardinali mteule Protase Rugambwa akiagana na Papa Francisko mjini Vatican

Askofu mkuu Robert Francis PREVOST, O.S.A., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa; Askofu mkuu Claudio GUGEROTTI, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki; Askofu mkuu Víctor Manuel FERNÁNDEZ, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Askofu mkuu Emil Paul TSCHERRIG, Balozi, Askofu mkuu Christophe Louis Yves Georges PIERRE, Balozi, Askofu mkuu Pierbattista PIZZABALLA, Patriaki wa Madhehebu ya Kilatini mjini Yerusalemu:  Askofu mkuu Stephen BRISLIN, wa Jimbo kuu la Cape Town, Afrika ya Kusini,  Askofu mkuu Ángel Sixto ROSSI, S.J., wa Jimbo kuu la Córdoba; Askofu mkuu Luis José RUEDA APARICIO, wa Jimbo kuu la Bogotá; Askofu mkuu Grzegorz RYŚ, wa Jimbo kuu la Łódź, Askofu mkuu Stephen Ameyu Martin MULLA, Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini; Askofu mkuu José COBO CANO, wa Jimbo kuu la Madrid, Askofu mkuu mwandamizi Protase RUGAMBWA, wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania;  Askofu mkuu Sebastian FRANCIS, wa Jimbo kuu la Penang; Askofu Stephen CHOW SAU-YAN, S.J., Askofu wa Hong Kong: Askofu François-Xavier BUSTILLO, O.F.M. Conv., wa Jimbo la Ajaccio, Askofu msaidizi Américo Manuel ALVES AGUIAR, wa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno pamoja na Padre Ángel FERNÁNDEZ ARTIME, s.d.b., Mkuu wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco.

Makardinali wapya wanasimikwa tarehe 30 Septemba 2023
Makardinali wapya wanasimikwa tarehe 30 Septemba 2023

Makardinali wengine katika orodha hii ni wale ambao wamejipambanua katika huduma kwa watu wa Mungu ni pamoja na Askofu mkuu Agostino MARCHETTO, Balozi; Askofu mkuu mstaafu Diego Rafael PADRÓN SÁNCHEZ, wa Jimbo Cumaná; Padre Luis Pascual DRI, OFM Cap., Muungamishi wa Madhabahu ya Mama Yetu wa Pompei, Buenos Aires nchini Argentina. Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu kuwakumbuka na kuwaombea Makardinali hawa wapya, ili waendelee kushikamana na Kristo Yesu Kuhani Mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, huku wakiendelea kumsaidia Baba Mtakatifu, Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kutekeleza dhamana na wajibu wake kama Askofu wa Roma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu waaminifu wa Mungu.

Makardinali wapya 2023

 

09 July 2023, 14:58