Tafuta

Mwenyezi Mungu anawapenda jinsi walivyo hata katika udhaifu wa mwili na hali yao ya dhambi, Mwenyezi Mungu ni Baba wa wote pasi na ubaguzi Mwenyezi Mungu anawapenda jinsi walivyo hata katika udhaifu wa mwili na hali yao ya dhambi, Mwenyezi Mungu ni Baba wa wote pasi na ubaguzi   (ANSA)

Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, Lisbon, Ureno! Tarehe 1-6 Agosti 2023

Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na vijana mbalimbali anapenda kuwaambia kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda jinsi walivyo hata katika udhaifu wa mwili na hali yao ya dhambi, Mwenyezi Mungu ni Baba wa wote pasi na ubaguzi na kwamba, anaangalia uwezekano wa kuandaa Siku ya Watoto Duniani, inayopaswa kuandaliwa na wazee! Vijana wa kizazi kipya ndio wahusika wakuu wa maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni kwa 2023.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yanaanza kutimua vumbi huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na vijana mbalimbali anapenda kuwaambia kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda jinsi walivyo hata katika udhaifu wa mwili na hali yao ya dhambi, Mwenyezi Mungu ni Baba wa wote pasi na ubaguzi na kwamba, anaangalia uwezekano wa kuandaa Siku ya Watoto Duniani, inayopaswa kuandaliwa na wazee! Wahusika wakuu wa maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni ni vijana wenyewe katika tofauti zao msingi na kwamba, lengo kuu ni kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Mungu. Mwenyezi Mungu anatembea na waja wake katika safari ya maisha yao, kwa wadhambi anawashika mkono na kuwainua ili waweze kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuendelea na safari ya maisha yao. Mwenyezi Mungu anawapenda waja wake jinsi walivyo na wala hakuna sababu ya mtu awaye yote kukatishwa wala kujikatia tamaa ya maisha. Kati ya vijana wanaojadiliana na Baba Mtakatifu ni Edward na Valerij, hawa wamekamatwa mara nyingi na kufungwa gerezani kwa sababu ya vitendo vya uhalifu kutokana na hali ya umaskini inayowandaama baada ya kulelewa kwenye nyumba ya watoto yatima! Vijana hawa wana matumaini ya kubadilika na kuwa watu wema zaidi baada ya kumaliza adhabu yao kifungoni.

Vijana wako njiani kuelekea Portugal
Vijana wako njiani kuelekea Portugal

Baba Mtakatifu anawaambia vijana hawa kwamba, maisha kimsingi yana pande mbili, wema na ubaya wa moyo! Mwenyezi Mungu yuko tayari kuwashika mkono na kuwanyanyua kwa neema na baraka zake, kwa toba na wongofu wa ndani: Kamwe maisha hayawezi kutupiliwa mbali kwa dhambi na makosa yanayotendwa na binadamu. Wakati mwingine, makosa yanawapatia waamini nafasi ya toba na wongofu wa ndani, tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Kuna kijana Ariana ambaye kutokana na matatizo na changamoto za afya, alikuwa amejikatia tamaa kiasi cha kutamani kifolaini, lakini alipomshirikisha Baba Mtakatifu Francisko safari ya maisha yake, moyo wake ukajawa na furaha kwa sababu lengo kuu la maisha ni kukutana na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anamshauri Ariana kuhakikisha kwamba, anajipatia tiba muafaka, kwa sababu kila mwanadamu anabeba ndani mwake madonda makubwa ya kimwili na kisaikolojia! Yote haya yanapaswa kupewa tiba muafaka. Kwa upande wake, Agustina na vijana kutoka Argentina wanamlalamikia Mungu kwa kuwatelekeza na kuwasukumia kwenye umaskini na hivyo kukosa ari na mwamko wa kusonga mbele. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kutoka Argentina kwamba, licha ya umaskini wa hali na kipato lakini wameshinda Kombe la Dunia. Hii ni changamoto kwa vijana kujizatiti zaidi katika hija yao kamwe wasithubutu kusimama na kuanza kulalama!

Mungu anawapenda waja wak jinsi walivyo
Mungu anawapenda waja wak jinsi walivyo

Kwa upande wake Valeria mwalimu wa dini shuleni analisikitia Kanisa kwa malumbanano, shutuma na mapambano yaliyomo ndani mwake. Angependa kuona Kanisa ambalo linasimikwa katika ukweli na uwazi na wala si Kanisa linalojifungia katika undani wake na kuanza kujitafuta; Kanisa ambalo liko karibu na waamini wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hili ni Kanisa linalotoka nje kwenda kuinjilisha. Ni kweli wakati mwingine ndani ya Kanisa kuna mashindano kati ya makundi, hali inayohatarisha ushirika wa Kanisa, lakini ukuu wa Kanisa unajionesha katika utofauti wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kumsikiliza Giuseppe ambaye amezamisha maisha yake katika michezo ya video kiasi hata cha kushindwa kukutana na hatimaye kuonana na jirani. Baba Mtakatifu anasema, hii ni hatari kwa sababu kijana kama Yosefu atachoka na hatimaye kujikatia tamaa. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kuwaalika vijana wote kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, atalifanyia kazi wazo la Kanisa kuwa na Siku ya Watoto Ulimwenguni. Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu Francisko siku hii itapendeza ikiwa kama itaandaliwa na wazee! Hili ni wazo jema!

Siku ya Vijana Ulimwenguni

 

26 July 2023, 15:23