Tafuta

Kumbukumbu ya mwaka mmoja, tangu Baba Mtakatifu Francisko alipofanya hija ya kitume nchini Canada ili kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa. Kumbukumbu ya mwaka mmoja, tangu Baba Mtakatifu Francisko alipofanya hija ya kitume nchini Canada ili kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa.  (Vatican Media)

Kumbukizi ya Mwaka Mmoja wa Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Canada 2022

Kumbukumbu ya mwaka mmoja, tangu Baba Mtakatifu Francisko alipofanya hija ya kitume nchini Canada, Baraza la Maaskofu Katoliki linaiangalia hija hii ya kitume, baada ya mwaka mmoja. Maaskofu wamekwisha kuandika barua nne za kichungaji mintarafu upatanisho; Baraza limeanzisha Mfuko wa Upatanisho na Wazawa Unaochangiwa na Majimbo 73 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Canada. Kauli mbiu ilikuwa ni kutembea pamoja, ili kudumisha upatanisho wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya 37 ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa nchini Canada kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 30 Julai 2022 ilinogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo hasa lilikuwa ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa; kwa kuzingatia ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Baba Mtakatifu, kwa niaba ya Mama Kanisa aliomba tena msamaha unaopania kuleta mwanga angavu wa hija ya: toba, wongofu wa ndani, matumaini na upatanisho wa Kitaifa. Nia ni kuleta utakaso wa kumbukumbu na hatimaye, kuendelea kujikita katika uinjilishaji wa kina unaosimikwa katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu alikazia kuhusu: Hija ya upatanisho, kumbukumbu ya tamaduni, mila na desturi njema za watu asilia wa Canada, Upatanisho na Uponyaji wa Kitaifa, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini inayosimikwa katika utamadunisho, ili kupyaisha kumbukumbu, unabii, mahusiano na mafungamano ya dhati kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya. Ni katika muktadha wa kumbukumbu ya mwaka mmoja, tangu Baba Mtakatifu alipofanya hija ya kitume nchini Canada, Baraza la Maaskofu Katoliki Canada “Canadian Conference of Catholic Bishops, CCCB”, linaiangalia hija hii ya kitume, baada ya mwaka mmoja. Maaskofu wamekwisha kuandika barua nne za kichungaji mintarafu upatanisho; Baraza limeanzisha Mfuko wa Upatanisho na Wazawa “Indigenous Reconciliation Fund, IRF” Unaochangiwa na Majimbo 73 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Canada. Lengo ni kukusanya kiasi cha dola za kimarekani milioni 30 katika kipindi cha miaka mitano. Tayari miradi 50 imekwisha kutekelezwa kama sehemu ya uponyaji na upatanisho nchini Canada. Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika mkutano wake mkuu ulioadhimishwa Mwezi Juni 2023, lilichapisha Mwongozo utakaotasaidia Majimbo Katoliki Canada kuunda Sera kuhusu takwimu za watu asilia wa Canada.  

Hija ya Papa Francisko Nchini Canada: Upatanisho
Hija ya Papa Francisko Nchini Canada: Upatanisho

Baba Mtakatifu katika hija yake ya Kitume nchini Canada anasema, alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na watu asilia wa Canada, ili kuonesha uwepo na ukaribu wake; masikitiko na machungu yaliyotanda katika sakafu ya moyo wake kwa nyanyaso, dhuluma na mauaji ya kimbari yaliyotendwa na Wakristo na kati yao wakiwemo Wakatoliki dhidi ya watu asilia wa Canada. Taasisi hizi za kidini zilishirikiana kwa karibu sana na Serikali za kikoloni kuwanyanyasa watu asilia wa Canada. Familia ya Mungu nchini Canada imeanza mchakato wa safari ambayo Mama Kanisa alikwisha ianzisha kitambo pamoja na watu asilia wa Canada, kwa kutembea pamoja, kama kauli mbiu ya hija ya 37 ya Kimataifa nchini Canada ilivyokazia. Baba Mtakatifu anasema, hii ni safari ya kutembea pamoja: uponyaji na upatanisho; kwa kutambua madhara yaliyotendeka katika historia; kuwasikiliza wahanga, ili hatimaye, kwa kuongozwa na dhamiri adilifu, waweze kujikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na mwelelekeo mpya wa mawazo. Lakini pamoja na dhuluma na nyanyaso walizowatendea watu asilia wa Canada, ndani ya Kanisa kuna waamini waliosimama kidete, wakaonesha ujasiri wa kutangaza na kushuhudia: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wakajifunza tamaduni, lugha, mila na desturi zao njema kama sehemu ya mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu kati ya watu asilia wa Canada. Inasikitisha kuona kwamba, katika mchakato wa utamadunisho kuna baadhi ya waamini walikwenda kinyume cha tunu msingi za Kiinjili, utu na heshima ya binadamu.

Upatanisho na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Upatanisho na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 28 Julai 2022 aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu na upatanisho wa Kitaifa nchini Canada katika Madhabau ya Kitaifa ya Mtakatifu Anna wa Beaupré: “Sainte Anne de Beaupré.” Hii ilikuwa ni fursa ya kutafakari na kukutana tena na watu asilia wa Canada, ili kumshukuru Mungu kwa zawadi hii ya kutembea pamoja. Akiwa nchini Canada, Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kutembelea Edmonton katika maadhimisho kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria, 26 Julai 2022, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Jumuiya ya Madola “Commonwealth Stadium”, huko Edmonton, Canada na kuhudhuriwa na umati wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za Canada. Katika muktadha wa hija yake ya kitume nchini Canada, Baba Mtakatifu alikazia mambo makuu mawili yanayopaswa kuzingatiwa. Waamini watambue kwamba, wao ni watoto wa historia inayopaswa kulindwa na kudumishwa, hatimaye, kuirithisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Pili watambue kwamba, wao ni wadau muhimu sana katika kuandika historia ya maisha na utume wao ambayo kimsingi bado haijaandikwa, kwani wao ni chemchemi ya maisha, tayari kumkaribisha Kristo Yesu, ili kutangaza na kushuhudia uwepo wake angavu kati pamoja nao! Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 28 Julai 2022 alikutana na kusali Masifu ya Jioni na: Wakleri, watawa, majandokasisi pamoja na wahudumu wa shughuli za kichungaji nchini Canada, kwenye Kanisa kuu la Notre-Dame, Jimbo kuu la Quèbec “Notre-Dame de Québec.” Katika mahubiri yake alikazia kuhusu umuhimu wa majiundo na malezi ya Kipadre, furaha ya Kikristo, mitazamo hasi katika ulimwengu mamboleo; baadhi ya changamoto za kichungaji ni pamoja na: kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko akiwa mjini Iqaluit, Jimbo Katoliki la Churchill, Canada, alikutana na kuzungumza kwanza kwa faragha na baadhi ya wanafunzi waliosoma kwenye shule za makazi ya watu asilia wa Canada. Katika hotuba yake, aliwaomba tena msamaha kwa makosa na udhaifu ulioneshwa na wamisionari wa Kanisa Katoliki katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho.

Dominika ni siku ya kutangaza na kushuhudia Ufufuko wa Kristo Yesu
Dominika ni siku ya kutangaza na kushuhudia Ufufuko wa Kristo Yesu

Sasa ni wakati wa kujizatiti katika mchakato wa uponyaji na upatanisho wa Kitaifa, na kuendelea kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, ndugu zao na historia yao katika ujumla wake. Waendelee kutembea kifua mbele katika mwanga wa maisha unaowawezesha kuwa huru, kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya sanjari na kusima kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Baada ya kuomba msamaha, hatua ya pili ilikuwa ni kunogesha mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Dominika, Siku ya kwanza ya Juma, ni njia ya upatanisho, inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo angavu wa Kristo Yesu Mfufuka, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini hata katika mazingira ambamo hakuna tena chembe ya matumaini. Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu yake azizi, kiwe ni chanzo na kilele cha maisha ya waamini. Kristo apewe nafasi ya kushirikiana na waja wake: maisha, udhaifu na matumaini yao, ili aweze kuwanyanyua tena; kuwaganga na kuwaponya, hatimaye, kuwapatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Na wao wakisha kupatanishwa na Mungu wageuke na kuanza kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upatanisho na amani katika jamii inayowazunguka. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, Kristo Yesu ndiye amani, chanzo cha upatanisho na ushirika kati yao, ili waweze kuwa wamoja kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Rej. Efe 2: 14. Kumbe, kuna haja pia ya kusimama kidete kutangaza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Julai 2022 alikutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wawakilishi wa watu asilia wa Canada pamoja na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi na Mashirika ya Kimataifa nchini Canada. Hotuba ya Baba Mtakatifu ilijikita zaidi katika nembo zinazopatikana kwenye bendera ya Canada. Baba Mtakatifu alikazia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; athari za ukoloni na umuhimu wa uinjilishaji unaosimikwa katika utamadunisho, unaozingatia na kuheshimu haki msingi za binadamu.

Ukoloni wa Kiitikadi na madhara yake
Ukoloni wa Kiitikadi na madhara yake

Baba Mtakatifu aligusia mifumo mbalimbali ya ukoloni, lakini hasa ukoloni wa kiitikadi na madhara yake katika maisha ya watu. Amewahimiza watu wa Mungu nchini Canada kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia na jamii katika ujumla wake. Changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo ni pamoja na: Ukosefu wa amani, athari za mabadiliko ya tabianchi na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Mchango wa watu asilia wa Canada katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi bila kusahau athari za ongezeko la idadi ya maskini na wahitaji zaidi. Mchakato wa utamadunisho upewe msukumo wa pekee, ili kujenga na kudumisha ushirika kati ya viongozi wa Kanisa na watu asilia wa Canada. Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi wote nchini Canada kwa kufanikisha hija yake ya kitume miongoni mwao. Baba Mtakatifu anasema, wazee wana ndoto na vijana wana unabii. Vijana ni manabii wa siku za usoni, alama ya matumaini kwa siku za baadaye. Lakini wazee ni chimbuko la historia na kamwe hawawezi kuchoka kuendelea kuota ndoto na kurithisha uzoefu na mang’amuzi yao kwa vijana wa kizazi kipya, bila kuwa ni kizingiti kwa maisha yao ya sasa na yale ya mbeleni. Katika hotuba yake, aliwaomba tena msamaha kwa makosa na udhaifu ulioneshwa na wamisionari wa Kanisa Katoliki katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho. Sasa ni wakati wa kujizatiti katika mchakato wa uponyaji na upatanisho wa Kitaifa, na kuendelea kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, ndugu zao na historia yao katika ujumla wake. Waendelee kutembea kifua mbele katika mwanga wa maisha unaowawezesha kuwa huru, kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, aliguswa sana kiasi cha kujisikia vibaya kutokana na shuhuda mbalimbali zilizotolewa na watu asilia wa Canada. Vijana na wazee wanapaswa kukita maisha yao katika majadiliano kati ya kumbukumbu na unabii, kama kielelezo cha ushirika na upatanisho wa Kitaifa. Watu wote wa Mungu nchini Canada wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa wa ujenzi wa dunia inayosimikwa katika mshikamano na udugu wa kibinadamu; kwa kupenda, kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, huku haki na amani vikidumishwa na wote.

Hija ya Kitume Canada
26 July 2023, 16:09