Tafuta

Kardinali mteule Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafunfundisho Tanzu ya Kanisa anasema, Taalimungu haina budi kukua na kukomaa, ikijikita katika majadiliano Kardinali mteule Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafunfundisho Tanzu ya Kanisa anasema, Taalimungu haina budi kukua na kukomaa, ikijikita katika majadiliano  (Vatican Media)

Kardinali Victor Manuel Fernandes: Kristo Yesu Ndiye Mkombozi wa Ulimwengu!

Kardinali mteule Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafunfundisho Tanzu ya Kanisa anasema, Taalimungu haina budi kukua na kukomaa, ikijikita katika majadiliano miongoni mwa wanataalimungu, sayansi na jamii katika ujumla wake. Huu ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Baraza lina dhamana ya kulinda imani dhidi ya uzushi, kutangaza na kushuhudia Injili kwa njia ya majadiliano ya kweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Lengo mahususi la Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ni kulinda mafundisho ambayo yanatokana na imani ili kutoa sababu za tumaini la Kanisa, lakini sio kama adui anayepinga na kulaani, bali katika ukweli na uwazi, kwa kutenda kwa upole na heshima. Hii ni sehemu ya barua kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko aliyomwandikia Kardinali mteule Víctor Manuel Fernández, aliyemteua hivi karibuni kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Kwa kuzingatia kwamba kwa masuala ya kinidhamu - hasa yanayohusiana na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto wadogo, hivi karibuni, Idara maalum imeundwa na hivyo kujengewa uwezo mkubwa wa kushughulikia nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, jukumu lake kuu kama Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ni kulinda imani, kutangaza na kuishuhudia kama sehemu ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ili mwanga wake uweze kuwa ni kigezo cha kuelewa maana ya uwepo haswa katika maswali yanayoletwa na maendeleo makubwa ya sayansi na jamii. Masuala haya yakikumbatiwa katika muktadha wa utangazaji na ushuhuda wa imani yanakuwa ni vyombo vya uinjilishaji kwa sababu yanaliwezesha Kanisa kuingia katika majadiliano na muktadha wa sasa katika kile ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya mwanadamu.

Taalimungu lazima ijengwe kwenye msingi wa majadiliano.
Taalimungu lazima ijengwe kwenye msingi wa majadiliano.

Ni katika muktadha huu, Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika mahojiano maalum na Kardinali mteule Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafunfundisho Tanzu ya Kanisa anasema, Taalimungu haina budi kukua na kukomaa, ikijikita katika majadiliano miongoni mwa wanataalimungu, sayansi na jamii katika ujumla wake. Huu ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Huu ni mwaliko wa kumwilisha Katiba ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linabeba uzito wa pekee yaani kulinda mafundisho ambayo yanatokana na imani ili kutoa sababu za tumaini la Kanisa. Kulinda imani ya Kanisa inayokua na kukomaa kila kukicha; kulinda imani dhidi ya uzushi na kutoa majibu muafaka badala ya Baraza kujikita katika falsafa ya kulaani tu. Habari Njema ya Wokovu inatangazwa na kushuhudia ule uzuri wa Injili bila kumezwa na malimwengu na hivyo kuleta maana ya pekee kwa wale wanaosikiliza na kushuhudia. Huu ni uinjilishaji unaosimikwa katika majadiliano na tamaduni mbalimbali.

Kardinali Victor Manuel Fernandez
Kardinali Victor Manuel Fernandez

Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume “Mungu ni upendo” "Deus Caritas est"; anasema huu ni waraka ambao kwa sasa ni kama mwongozo wa utekelezaji wa mchakato wa umwilishaji wa matendo ya huruma: Kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya Wakristo. Waraka wa Mungu ni upendo ni endelevu na kamwe hauwezi kupitwa na wakati kwani ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Upendo unabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, Kristo Yesu aliyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu; upendo ambao Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wana umwilisha katika uhalisia wa maisha, kielelezo makini cha imani tendaji! Hii ni imani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu aliye hai; Kristo anayewapenda na kuwaokoa waja wake. Huu ni mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuendeleza taalimungu msingi inayojielekeza kwa ajili ya kutanzaza Habari Njema ya wakovu hadi miisho ya dunia.

Kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu
Kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu

Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa Kardinali mteule anasema, Kanisa linahitaji kukua katika tafsiri ya Neno la Mungu lililofuliwa na kueleweka katika ukweli huo, ili kuweza kuunganishwa na Roho Mtakatifu katika heshima na upendo, mambo yanayoliwezesha Kanisa kukua. Ukuaji huu wenye upatanifu utahifadhi fundisho la Kikristo kwa ufanisi zaidi kuliko utaratibu wowote wa udhibiti. Mama Kanisa anaendelea kuthamini karama ya wanataalimungu na jitihada zao kwa ajili ya tafiti za Kitaalimungu, ili mradi tu, “hawaridhiki na taalimungu inayofanyika mezani na mantiki ya kutaka kutawala kila kitu. Ukweli ni bora kuliko wazo, kumbe, taalimungu inayotilia shaka uweza na ukuu wa Mungu na hasa huruma yake ni hatari sana. Kanisa linahitaji kutangaza na kushuhudia uwezo wa Mungu anayependa, anayesamehe, anayeganga, kuponya na kuwaweka waja wake huru, ili hatimaye, kukuza na kudumisha huduma ya udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anamwomba Kardinali mteule Víctor Manuel Fernández kuhakikisha kwamba, Hati na Nyaraka mbalimbali za Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa zinakuwa ni msaada wa kutosha kitaalimungu, zinapatana na wingi wa Mafundisho ya kudumu ya Kanisa pamoja na kuzingatia Mamlaka Fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” ya hivi karibuni. Mwishoni mwa barua hii, Baba Mtakatifu Francisko anamweka Kardinali mteule Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika maisha na utume huu mpya katika Kanisa.

Taalimungu inasimikwa katika majadiliano na wataalimungu, sayansi na jamii
Taalimungu inasimikwa katika majadiliano na wataalimungu, sayansi na jamii

Baba Mtakatifu amemteua Kardinali Víctor Manuel Fernández, wa Jimbo kuu La Plata nchini Argentina kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na anatarajia kuanza utume huu mpya kati kati ya Mwezi Septemba 2023. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Víctor Manuel Fernández, alizaliwa tarehe 18 Julai 1962 huko Alcira Gigena, nchini Argentina. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 15 Agosti 1986 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Alijiendeleza kwa masomo ya juu na hatimaye akajipatia Shahada ya uzamili katika taalimungu huku akijikita katika Sayansi ya Biblia kutoka Chuo Kikuu cha Gregorian kilichoko mjini Roma na hatimaye, akahitimisha kwa kujipatia Shahada ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Buenos Aires nchini Argentina. Tangu mwaka 1993 hadi mwaka 2000 aliteuliwa kuwa Paroko, Muasisi wa Taasisi ya Majiundo ya waamini walei na Kituo cha Mafunzo ya Waalimu cha “Jesús Buen Pastor” huko Rio Cuarto, Cordoba. Askofu mkuu Víctor Manuel Fernández, amewahi kuwa Mlezi wa Seminari, na Mkurugenzi wa Majadiliano ya Kiekumene na Katekesi. Mwaka 2007 alishiriki katika Mkutano wa V wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, kama mwakilishi wa Mapadre kutoka Argentina na hatimaye, akateuliwa kuwa ni mjumbe wa kuhariri hati ya mwisho ya Mkutano wa CELAM wa mwaka 2007.

Changamoto kubwa ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema!
Changamoto kubwa ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema!

Kati ya mwaka 2008 hadi mwaka 2009 aliteuliwa kuwa ni Dekano wa Kitivo cha Taalimungu Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Cha Argentina na Rais wa Chama cha Wanataalimungu nchini Argentina. Kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2018 aliteuliwa kuwa ni Gambera wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Argentina. Tarehe 13 Mei 2013, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu mkuu. Ameshiriki Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia kati ya mwaka 2014 hadi mwaka 2015. Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina kunako mwaka 2007 likamchagua kuwa Rais wa Tume ya Imani na Tamaduni ya Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina. Mwezi Juni 2018 akasimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la La Plata, nchini Argentina. Alikuwa ni mjumbe wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Mshauri wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki na kwa sasa ni mjumbe wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu baada ya mageuzi yaliyofanywa na Katiba mpya ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Ni mwandishi wa vitabu na makala zaidi 300; vitabu ambavyo vimetafsiriwa katika lugha mbalimbali, kielelezo makini cha msingi wa Kibibla katika maisha na utume wa Askofu mkuu Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa.

Mahojiano Baraza Imani
14 July 2023, 15:34