Jubilei ya Miaka 700 Tangu Mt. Thoma wa Akwino Atangazwe Mtakatifu na Miaka 750 ya Kifo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Thoma wa Akwino, “St. Thomas Aquinas, San Tommaso d’Aquino, anayejulikana kama “Doctor Angelicus; “Angelic Doctor” alizaliwa kunako mwaka 1225 huko Roccasecca, karibu na mji wa Aquino. Akafariki dunia 7 Machi 1274, huko Fossanova, karibu na mji wa Terracina. Akatangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Yohane XXII tarehe 18 Julai 1223 huko Avignon, nchini Ufaransa. Alikuwa ni mtawa Mdominican. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anapenda kuyakumbuka matukio makuu matatu katika maisha na utume wa Mtakatifu Thoma wa Akwino: Miaka 700 tangu alipotangazwa kuwa ni Mtakatifu, Miaka 750 tangu alipofariki dunia na kumbukumbu yake itakuwa ni mwaka 2024 sanjari na miaka 800 tangu alipozaliwa, tukio ambalo litakumbukwa mwaka 2025. Ni katika muktadha wa kumbukizi hizi, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Latina, Sora na Frosinon, kujikita katika tafakari ya kina kuhusu amana na mafundisho ya Mtakatifu Thoma wa Akwino, Dr. Angelicus pamoja na kusali ili kumwomba ili aweze kuwakirimia amana na utajiri huu mkubwa katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Askofu Mariano Crociata wa Jimbo Katoliki la Latina-Terrachina-Sezze-Priverno anasema, tarehe 11 Julai 2023 kutakuwa na Ibada ya Sala itakayoadhimishwa kwenye Abasia ya Fossanova. Sala nyingine itaadhimishwa tarehe 14 Julai 2023. Jumanne tarehe 18 Julai 2023 majira ya saa 12:30 jioni kwa saa za Ulaya, kutaadhimishwa Ibada ya Misa takatifu kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 700 tangu Mtakatifu Thoma wa Akwino alipotangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Yohane XXII tarehe 18 Julai 1223 huko Avignon nchini Ufaransa.
Ibada hii ya Misa Takatifu itaadhimishwa na Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu ambaye ameteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko ili kumwakilisha katika tukio hili adhimu. Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake aliyowaandikia Maaskofu wa Majimbo ya: Latina-Terracina-Sezze-Priverno; Sora-Cassino-Aquino-Pontecorvo pamoja na Jimbo Katoliki la Frosinone-Veroli-Ferentino na Anagni-Alatri anakazia umuhimu wa kutambua kazi ya Roho Mtakatifu anayeliongoza Kanisa katika historia na kwa upande mwingine, jibu la ukarimu kutoka kwa binadamu anayekiri karama za Mungu zinazoboreshwa na neema ya Mungu; Uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika sala, masomo sanjari na utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwambata Kristo Yesu, njia inayowapeleka kwa Baba wa mbinguni. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Maaskofu wa Majimbo hayo yenye historia ya maisha ya Mtakatifu Thoma wa Akwino kwa kuwaongoza watu wa Mungu kwa huruma na upendo, waliobahatika kupata urithi wa fadhila za kiutu, kiasili na kitume za Mtakatifu Thoma wa Akwino. Baba Mtakatifu anapenda kuwaonesha uwepo wake wa karibu kwa waamini wote watakaoshiriki katika matukio ya maadhimisho ya Jubilei mbalimbali za maisha na utume wa Mtakatifu Thoma wa Akwino.
Kumbukizi hii baada ya muda wote huo ni mwaliko wa kutambua kazi za Roho Mtakatifu anayeliongoza Kanisa katika historia na kwa upande mwingine jibu la ukarimu wa mwanadamu unaoshuhudiwa na karama zinazoboreshwa kwa neema ya Mungu. “Grazia non tollit naturam, sed perficit” yaani: “Neema haiondoi asili, bali huikamilisha.” Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, ukweli wa kiimani unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na katika Umungu na Ubinadamu wa Kristo Yesu ni nyenzo muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika sala, masomo, tamaduni na mahubiri yanayotekelezwa na viongozi wa Kanisa, uongozi wa kiraia pamoja na marafiki na wajuani. Mtakatifu Thoma wa Akwino, “Doctor communis” ni amana na utajiri wa Kanisa kwa leo na Kesho, kwani ni mtu aliyekita maisha yake kutafuta ukweli na ufunuo wa Uso wa Mungu, anawafundisha watu wa Mungu kwamba, kimsingi wao ni mahujaji wanaoangazwa na mwanga wa akili kuhusu Fumbo la Kristo Yesu njia inayowapeleka waamini kwa Baba yake wa mbinguni; huu ni mwanga unaoangaza Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Kumbe, waamini wanapaswa kuzama katika kuutafuta ukweli.
Baba Mtakatifu anawaalika wasomi kuendelea kumjifunza Mtakatifu Thoma wa Akwino mintarafu historia na tamaduni za watu wa nyakati zake, ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Majimbo haya ambayo kimsingi yanahifadhi kumbukumbu hai ya maisha na utume wa Mtakatifu Thoma wa Akwino, yanapewa dhamana ya ujenzi wa Jumuiya za Kisinodi, ambazo ziko wazi kwa ukweli wote. Waamini wajitahidi kujenga Kanisa linalosimikwa katika maisha ya kijumuiya yanayoboreshwa na Sakramenti za Kanisa, maadhimisho ya Liturujia, tasaufi na katika huduma makini yaani “Diakonia” kiakili na kitamaduni, kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika ukarimu wa Kiinjili, upendeleo wa pekee, ukitolewa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mtakatifu Thoma wa Akwino ni mtu aliyependa sana ukweli ndiyo maana anaitwa “Mtume wa Ukweli.” Kwa hakika ameacha amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa hususan utakatifu wa maisha, changamoto na mwaliko kwa waamini kujizatiti katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kwa kujiweka chini ya shule ya Mtakatifu Thoma wa Akwino. Maaskofu wanahimizwa na Baba Mtakatifu Francisko kutafuta vyombo na lugha muafaka ili mawazo ya Mtakatifu Thoma wa Akwino yaweze kuwafikia watu wengi zaidi.