Ujumbe wa Papa Francisko Kwenye Mkutano wa Kimataifa Kuhusu Ajira: Haki Jamii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Haki jamii lazima iwe msingi wa mpito wa Kimataifa kuelekea ajira zenye haki na endelevu zaidi kwa wote amesema Katibu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa njia ya video kwenye ufunguzi wa mkutano wa Kimataifa wa ajira ulioanza Jumatano tarehe 15 Juni na kuhitimishwa tarehe 16 Juni 2023 mjini Geneva, nchini Uswis. Mkutano huu wa siku mbili wa Shirika la Kazi Duniani, ILO, unalenga kufahamisha pendekezo lake la muungano wa kimataifa wa haki jamii inalenga kupunguza na kuzuia ukosefu wa usawa. "Ulimwengu uko katika wakati wa kufanya maamuzi. Sera za leo kuhusu mabadiliko ya tabianchi, vitisho kwa usalama wa kimataifa, juu ya mshikamano wa kijamii na zaidi, zitaunda mustakabali wetu, wa watoto na wajukuu wetu.” Amesema Guterres. Kwa hivyo, Mkutano huu unatoa fursa "kutafuta suluhu ambazo zitafanya mustakabali huo kuwa wa haki zaidi, usawa, endelevu na shirikishi", ameongeza. Mkutano umejadili jukumu muhimu la haki jamii katika kuunda ulimwengu endelevu zaidi na wenye usawa na umejadili kuhusu mikakati ya kuongezeka na kuunganishwa vyema kwa hatua za pamoja ili kuendeleza haki kijamii na kuhakikisha uwiano wa sera. Mkutano huu umekuwa ni jukwaa kwa washiriki kushirikisha maono yao na vipaumbele vya haki jamii na kuonyesha hatua wanazochukua na wanajitolea kuchukua ili kuendeleza haki jamii. Inatarajiwa kwamba matokeo ya Mkutano huu yatafahamisha mijadala katika mabaraza mengine ya kimataifa kuhusu umuhimu na mikakati ya kufikia haki jamii, kama vile, mwaka 2023, Mkutano wa Kilele wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, G20 na mikutano ya kilele ya nchi za BRICS yaani: Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye Mkutano wa Shirika la Kazi Duniani ILO, tarehe 14 Juni 2023 katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amekazia kuhusu dhana ya haki jamii, amani duniani, utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kanuni ya auni mambo msingi katika kukuza na kudumisha haki jamii. Kanisa limekuwa mstari wa mbele kutetea haki msingi, utu na heshima ya binadamu kwa kukazia kwamba, umilikaji wa ardhi, makazi bora na fursa za ajira ni mambo msingi katika Mamlaka Fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” yanayopata chimbuko lake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa. Ardhi, Makazi na Ajira ni vigezo msingi vya haki jamii. Neno haki jamii lilianza kutumiwa na wanafalsafa na wanataalimungu kunako karne 19, likipania kupambana na hali na mazingira mabaya ya kazi viwandani. Mama Kanisa akajizatiti ili kuhakikisha kwamba, anamwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya wafanyakazi. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili mambo msingi yanayofafanuliwa katika Waraka wa Kitume wa “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” ambao kwa mwaka 2023, Kanisa linaadhimisha kumbukizi ya miaka 60 tangu Mtakatifu Yohane XXIII alipouchapisha.
Leo hii kuna umati mkubwa wa watu wasiokuwa na fursa za ajira, kuna watu utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa kutokana na baa la njaa; kuna watu wanafanyishwa kazi za suluba kwa mshahara “kiduchu”; kuna wakimbizi na wahamiaji wanaonyonywa na kudhulumiwa; kuna wakimbbizi na wahamiaji wanaofanyishwa kazi za hatari chafu na zisizo na utu hata kidogo! Ndiyo maana Kanisa linaendelea kujizatiti kutangaza na kushuhudia Injili ya amani duniani inayosimikwa katika msingi wa haki jamii kwa kujikita katika utu, heshima na haki msingi za binadamu, mshikamano na kanuni auni. Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kuna haja kwa nchi mbalimbali kushirikiana katika masuala ya kiuchumi, kiteknolojia na kitamaduni kwa kuhakikisha kwamba, utajiri na rasilimali ya dunia, vinatumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu wote. Kwa njia hii, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo sanjari na ukosefu wa amani duniani! Kanuni auni isaidie kukoleza ushirikiano na mshikamano katika Jumuiya ya Kimataifa, kwa kuendelea kuimarisha sera, mikataba na itifaki mbalimbali zilizowekwa na Jumuiya ya Kimataifa lengo kuu ni kufutilia mbali mifumo mbalimbali ya ubaguzi, umaskini, ghasia pamoja na ukosefu wa haki.
Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI katika hati yake ya kichungaji upendo katika ukweli anazungumzia umuhimu wa maendeleo endelevu ya mwanadamu katika nyakati hizi, kwa kukazia dhana ya ushirikishwaji na mshikamano mambo yanayoongozwa na Kanuni ya Auni. Mwanadamu anapaswa kutumia rasilimali na nyenzo zinazomzunguka kwa ajili ya kujiletea maendeleo endelevu, kama njia ya kujenga amani na utulivu miongoni mwa jamii, kwani ujinga, umaskini na magonjwa ni kati ya mambo yanayopelekea migogoro na kinzani za kijamii.Mafundisho Jamii ya Kanisa yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum.