Tafuta

Kuna baadhi ya vijana kutokana na sababu mbalimbali hawataweza kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni huko Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno kati yao ni kijana Edna ambaye ni mgonjwa hawezi kitandani. Kuna baadhi ya vijana kutokana na sababu mbalimbali hawataweza kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni huko Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno kati yao ni kijana Edna ambaye ni mgonjwa hawezi kitandani. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Edna Ambaye Ni Mgonjwa Sana Hawezi Kitandani

Kijana Edna ambaye kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa ambao pole pole unamfanya “kuanza kuchungulia kaburi” na kwamba, hajui lini atakutana na Kristo Yesu, Hakimu mwenye huruma na mapendo, lakini kwa uhakika anasema, bado kitambo kidogo tu! Edna ametumia fursa hii, kumwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko na ikamfikia tarehe 22 Juni 2023 na kuamua kuijibu kwa kumtumia ujumbe kwa njia ya video, kwani Edna alitamani sana kumwona mubashara!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023, yananogeshwa na kauli mbiu “Maria akaondoka kwa haraka” Lk 1:39. Kimsingi hii ni hija ya maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini lakini hasa zaidi vijana wa kizazi kipya, kuguswa na moyo wa unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa wengine kama alivyofanya Bikira Maria kwa kumtembelea binamu yake Elizabeth. Safari hii ya Bikira Maria inafungua macho ya waamini ili kuangalia historia ya wokovu, kwa wanawake hawa wawili, wanavyopokea na kukumbatia upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao na inavyopenyeza katika historia ya mwanadamu na hivyo kumkirimia furaha ya Injili. Baba Mtakatifu anawataka vijana kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaosimikwa katika huduma ya upendo! Kwa kawaida pale ambapo kijana anaanguka, utu wake pia unaanguka; anapoinuka, anauinua pia utu wa watu wengine ulimwenguni kote. Hii ni nguvu maridhawa ambayo iko mikononi mwa vijana. Hata leo hii, Mwenyezi Mungu anapenda kuwaambia vijana “Inuka” ujumbe mahususi ambao utawasaidia vijana kujiandaa kwa nyakati na kuwa tayari kuandika kurasa mpya katika historia ya mwanadamu, jambo ambalo linahitaji: nguvu, hamasa na ari kubwa, ili kuinuka, tayari kuwa shuhuda wa mambo hayo aliyoyaona. Mtume Paulo ambaye alilitesa na kulidhulumu Kanisa anashuhudia kuhusu nuru angavu kutoka mbinguni na sauti ya Kristo Yesu aliyemwita kwa jina lake, kiasi cha kutubu na kumwongokea, akabahtika kuwa ni chombo cha uinjilishaji kwa watu wa Mataifa.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni 2023
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni 2023

Kuna baadhi ya vijana kutokana na sababu mbalimbali hawataweza kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni huko Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno kati yao ni kijana Edna, mwenye umri wa miaka kumi na saba, ambaye kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa ambao pole pole unamfanya “kuanza kuchungulia kaburi” na kwamba, hajui lini atakutana na Kristo Yesu, Hakimu mwenye huruma na mapendo, lakini kwa uhakika anasema, bado kitambo kidogo tu, kadiri ya utabiri wa madaktari. Kijana Edna ametumia fursa hii, kumwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko na ikamfikia tarehe 22 Juni 2023 na kuamua kuijibu kwa kumtumia ujumbe kwa njia ya video, kwani Edna alitamani sana kumwona Baba Mtakatifu. Anaishi kipindi hiki cha mateso na mahangaiko ya ndani, kwa amani na utulivu pamoja na tabasamu la kukata na shoka, kama mashuhuda wanavyosimulia hali yake wale wanaomfahamu kutoka katika Parokia ya Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe Padre na Shahidi wa Mwanga wa Imani. Kijana Edna anasema, kila mara anapomwona Baba Mtakatifu Francisko akiongea kwenye Luninga anafurahia sana, kiasi cha kujisahau kwamba ni mgonjwa hali inayomzuia kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni huko Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. Amemwandikia barua Baba Mtakatifu Francisko ili kuonesha jinsi alivyo muhimu kwake binafsi na familia yake. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video, anamshukuru na kumpongeza kwa amani na utulivu alionao moyoni mwake. Amani hii ni kama mbegu iliyopandwa katika nyoyo za watu wengi na inaonekana na kushuhudiwa na wale wanaomzunguka.

Maandalizi ya Siku ya 38 ya Vijana Duniani 2023
Maandalizi ya Siku ya 38 ya Vijana Duniani 2023

Baba Mtakatifu amemhakikishia kwamba, anaendelea kumsindikiza katika safari ya ugonjwa wake kwa njia ya sala na sadaka yake na kumwangalia Kristo Yesu anayewasubiri kuwapokea miokononi mwake. Edna alimwomba Baba Mtakatifu kusali na kumwombea naye Baba Mtakatifu amemwomba Edna kumsindikiza kwa sala zake katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anamwombea ili Kristo Yesu aweze kumkirimia nguvu ya kuweza kukabiliana na safari hii na mwishoni, amempatia baraka zake za kitume! Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amewaandikia ujumbe watu wanaojitolea kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni huko Lisbon, nchini Ureno na kuwahakikishia kwamba, wataonana Lisbon, hivi karibuni, Mungu akipenda. Baba Mtakatifu anawahimiza mahujaji kushiriki kikamilifu katika maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa moyo wa upendo na ukarimu katika maisha yao. Hii inatokana na ukweli kwamba, ukarimu ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa watu na kamwe watu hawajifunzi kuwa wakarimu kwa kupitia vitabu. Ukarimu unabubujika kutoka katika moyo wa mwamini kwa kutenda, kwa ari na moyo mkuu, mambo ambayo wanapaswa kuyakuza na kuyadumisha katika maisha. Ari na moyo mkuu ni chanzo cha furaha ya kweli!

Papa Edna

 

25 June 2023, 16:11