Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa Ajili ya Amerika ya Kusini, CAL pamoja na viongozi wakuu wa Taasisi za huduma ya upendo waliokuwa wanakutana mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa Ajili ya Amerika ya Kusini, CAL pamoja na viongozi wakuu wa Taasisi za huduma ya upendo waliokuwa wanakutana mjini Vatican. 

Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini: Kielelezo Makini Cha "Diakonia" Huduma Kwa Watu wa Mungu

Tume ina dhamana ya kushughulikia kiuchumi miradi ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili. Tume inaitwa kuwa ni kielelezo makini cha “Diakonia” yaani huduma inayoonesha ile hali ya kujali na huduma inayotolewa na Papa pamoja na kusaidia Kanisa kukabiliana na changamoto za dharura, Baba Mtakatifu anashukuru kwa ushirikiano wa Tume hii pamoja na taasisi mbalimballi za huduma ya maendeleo kwa ajili ya Kanisa Amerika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa Ajili ya Amerika ya Kusini, CAL pamoja na viongozi wakuu wa Taasisi za huduma ya upendo waliokuwa wanakutana mjini Vatican kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 23 Juni 2023. Kutangaza na kushuhudia Injili ni dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima. Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote: kiroho na kimwili. Upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii. Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni sehemu ya Katiba mpya ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Katiba hii inadokeza umuhimu wa wongofu wa kimisionari sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, mambo msingi yanayoweza kulisaidia Kanisa kuonesha wazi Uso halisi wa Kristo Yesu kwa njia ya utendaji wa Sekretarieti kuu ya Vatican na mchakato wa uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa kwa wakati huu.

Maafisa wa Tume ya KIpapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini
Maafisa wa Tume ya KIpapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, baada ya kusikiliza maoni mbalimbali alitambua na kuamua kwamba,  maono angavu ya kichungaji ya Papa Pio XII ya kuunda Tume ya Kipapa kwa Ajili ya Amerika ya Kusini, CAL kunako mwaka 1958 yaendelezwe na kupyaishwa mintarafu maisha na utume wa Makanisa mahalia. Kwa sasa Tume ina dhamana na utume wa kushughulikia kiuchumi miradi ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili. Tume inaitwa kuwa ni kielelezo makini cha “Diakonia” yaani huduma inayoonesha ile hali ya kujali na huduma inayotolewa na Baba Mtakatifu pamoja na kusaidia Kanisa kukabiliana na changamoto za dharura, Baba Mtakatifu anashukuru kwa ushirikiano wa Tume hii pamoja na taasisi mbalimballi za huduma ya maendeleo kwa ajili ya Kanisa Amerika ya Kusini.   Baba Mtakatifu anakaza kusema, kila moja ya taasisi za Kanisa la Amerika ya Kusini ina asili na utume wake, lakini taasisi zote hizi zinapaswa kufanya kazi kushirikianana na kushikamana, changamoto ya kugundua kila siku ule mshangao wa na shukrani; imani ya Kikkristo ni kielelezo cha uhakika wa urafiki na Mwenyezi Mungu, anayewatangulia katika utendaji wao, anayewaelimisha na kufuatana nao kwa karibu zaidi. Kipengele halisi cha asili cha msaada wa Kanisa ni upendo wa Kristo Yesu unaowahimiza, upendo unaowatangulia na kuwaalika kumtangaza na kumshuhudia Mwenyezi Mungu, asili ya wema wote na Kristo Yesu, ndugu yao mpendwa ambaye amewakomboa na Roho Mtakatifu anayeliongoza na kulitegemeza Kanisa; Roho Mtakatifu ndiye anayeunda ushirika na kuwaongoza watu wote kuelekea kwenye utimilifu wake. Rej, 2Kor 5:13-20.

Wajumbe wa Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Amerika ya Kusini.
Wajumbe wa Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Amerika ya Kusini.

Baba Mtakatifu anasema, Mtakatifu Paulo, kwa mfano, alijulikana kuwa ni mtu msomi, mwenye uwezo na ufanisi mkubwa hivyo “alishikwa na Kristo Yesu ( Flp 3:12 ) na kutokana na kutafakari kwa Yule ambaye “alimpenda na kujitoa nafsi yake kwa ajili yake” (taz. Wagalatia 2:20) usemi  huu wa “upendo wa Kristo” unapata maana yake yote ya kweli. Kristo anawahimiza waja wake kumwilisha upendo katika uhalisia wa maisha yao” (2Kor 5:14). Mtume Paulo anagundua kwa mshangao kwamba maisha yake hayawezi kuendelea kuwa sawa. Baada ya makabiliano ya kibinafsi aliyokuwa nayo njiani kuelekea Damesko kila kitu kikawa jibu la muda mrefu kwa upendo wa Kristo, ambao ukawa ndani yake ni nguvu, ujasiri na ushujaa. Kweli Paulo Mwalimu na  Mtume wa Mataifa akahisi kuhimizwa na upendo huo, hata kusema "Ole wangu ikiwa sitaihubiri Injili!" (1 Wakorintho 9,16). Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa kusema Amerika ya Kusini inahitaji msaada wa mshikamano; yaani msaada wa kuinjilisha maeneo ya kijiografia na yaliyopo. Msaada wa kukidhi mahitaji ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii pamoja na kukuza ushirikiano wa udugu wa kibinadamu na mshikamano na taasisi pamoja mashirika yote ya misaada ya Kanisa Katoliki, ili kukamilishana na kusaidiana na watu wote.

Papa Tume ya Amerika ya Kusini
24 June 2023, 14:17