Siku ya Wakimbizi Duniani 20 Juni 2023: Kauli Mbiu: Matumaini Mbali na Nyumbani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 20 Juni inaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani na kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya kwa mwaka 2023 ni “Matumaini mbali na nyumbani.” Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR., zinaonesha kwamba, idadi ya wakimbizi kwa mwaka 2022 ilikuwa ni milioni 110. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 18 Juni 2023 kwa uchungu mkubwa amesema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani huku kukiwa na wakimbizi na wahamiaji zaidi ya 80 waliozama na kufa maji baharini huko Pylos nchini Ugiriki, idadi ya watu waliopoteza maisha inaendelea kuongezeka na kwamba, waliokolewa ni watu 104 wakati ambapo mashua kutoka Libya ilikuwa imebeba abiria 750, wengi wao wakiwa ni wakimbizi na wahamiaji kutoka Siria, Pakistani na Misri. Kumbe zaidi ya wakimbizi 600 hawajulikani mahali walipo. Hii ni ajali mbaya zaidi kutokea, ukiacha ile iliyotokea mwezi Aprili 2015. Tayari watu kumi na moja wametiwa pingu kwa shutuma za kujihusisha na biashara haramu ya binadamu pamoja na vitendo vya jinai.
Mashirika ya misaada kwa wakimbizi yamezitupia lawama nchi za Ugiriki, Malta na Italia kwa kushindwa kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuokoa maisha ya wakimbizi na wahamiaji hawa. Kimsingi, “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018” unapania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Ingawa Mkataba huu hauzifungi kisheria nchi husika, lakini ni muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa kama chombo cha rejea katika mchakato wa kudumisha uhai na haki msingi za binadamu. Kumbe, haki msingi za binadamu pamoja na mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake ni mambo muhimu sana. Baba Mtakatifu aliwakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji wote waliofariki dunia pamoja na kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti zaidi ili maafa kama haya yasijitokeze tena kwa siku za baadaye.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wakimbizi wanawakilisha roho bora zaidi ya kibinadamu. Wanahitaji na wanastahili kuungwa mkono na kupewa mshikamano wa kutosha na wala sio mipaka iliyofungwa na hivyo kulazimika kurudi nyuma walikotoka. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, zaidi ya watu milioni mia moja wanaoishi katika nchi zinazokumbwa na migogoro, kinzani na mipasuko ya kijamii; mateso, njaa pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi wamelazimika kuyahama makazi na nchi zao ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Waathirika wakuu ni watoto na wanawake wanaolazimika kufanya safari ngumu, huku wakikabiliwa na vitendo vya unyanyasi, unyonyaji, ubaguzi na ukatili mkubwa. Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani ni ukumbusho kwa Jumuiya ya Kimataifa kwamba, inawajibu wa kuwalinda na kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji, kwa kuwapatia msaada wa kutosha, makazi na kuwasaidia kujenga upya maisha yao, kwa kutoa kipaumbele kwa utu, heshima na haki zao msingi. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kunahitajika msaada mkubwa kwa nchi zinazowakaribisha wakimbizi na wahamiaji kadiri ya Mtakaba wa Kimataifa juu ya wakimbizi na wahamiaji; kwa kuongeza fursa za elimu bora zaidi, makazi yenye staha, huduma bora za afya na ulinzi wa kijamii sanjari na kuongeza ari na nguvu zaidi katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani, ili hatimaye, wakimbizi waweze kurejea makwao salama salimini. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuunganisha matumaini ambayo wakimbizi wanayabeba nyoyoni mwao, kwa kuunganisha ujasiri wao pamoja na fursa wanazohitaji katika kila hatua ya maisha yao.